MWIGULU AKABIDHI AMBULANCE NA KUSISITIZA LISITUMIKE VIBAYA.



Waziri wa Mambo ya ndani na Mbunge wa jimbo la Iramba Mkoani Singida Mwigulu Nchemba akiwasha gari la kubebea wagonjwa (ambulance), katika kijiji cha Urughu tarafa ya Ndago jimbo la Iramba.
Waziri wa Mambo ya ndani na Mbunge wa jimbo la Iramba mkoani Singida Mwigulu Nchemba akizungumza kwenye hafla ya kukabidhi gari la kubebea wagonjwa (ambulance) katika kijiji cha Urughu tarafa ya Ndago jimbo la Iramba.
Mkazi wa kijiji cha Urughu jimbo la Iramba mkoani Singida Jumanne Hatibu akizungumza kwenye hafla ya makabidhiano ya gari la kubebea wagonjwa lililotolewa na serikali kupitia wizara ya afya jinsia, wazee na watoto.

…………………………………..

Waziri wa Mambo ya Ndani na Mbunge wa jimbo la Iramba Mkoani Singida Mwingulu L. Nchemba, amekabidhi gari la kubebea wagonjwa mpya na la kisasa ambalo limetolewa na serikali kupitia Wizara ya Afya, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kituo cha afya cha Ndago kilichopo Wilayani Iramba.

Mwigulu ameagiza gari hilo lisitumike kama taksi au gari la kubebea mkaa, bali litumike kwa kazi iliyokusudiwa ambayo ni kubebea wagonjwa na akina mama wajawazito tu.

Mbunge huyo ameyasema hayo juzi wakati akizungumza kwenye hafla ya kukabidhi ‘ambulance’ hiyo iliyofanyika katika kijiji cha Ndago jimbo la Iramba na kuhudhuriwa na mamia ya wananchi.

Aidha, amesema ni marufuku wagonjwa kuombwa kuchangia mafuta ya ambulance hiyo au gharama yo yote ile, gari hili wagonjwa walitumie bure.

“Gari hilo lipatikane kituoni wakati wote. Liwe na mafuta ya kutosha na dereva awepo. Gari hili ambalo ni la kisasa, litunzwe na kulindwa ili liweze kutumika kwa miaka mingi ijayo”, alisema Mwigulu.

Mbunge huyo ameishukuru serikali ya awamu ya tano chini ya rais Magufuli na waziri Ummy kwa msaada huo ambao utaokoa wapiga kura wake na wananchi kwa ujumla.

Awali mganga mfawidhi wa kituo cha afya cha Ndago, Dkt Lyoce Mgelwa, alisema kituo hicho kinahudumia tarafa nzima ya Ndago yenye wakazi 89,882.

Pia alisema kituo hicho kinapokea wagonjwa wanaopata rufaa katoka kwenye zahanati 10 zilizopo katika tarafa ya Ndago.

Dkt Lyoce alisema msaada huo wa kupatiwa gari la kubeba wagonjwa ambulance, utapunguza kero zinazowakabili wagonjwa wanaopewa rufaa kuchelewa kufika kwa wakati katika hospitali ya wilaya.

“Wagonjwa wanaopewa rufaa watawahishwa hospitali ya wilaya ili kuokoa maisha ya wagonjwa na hasa akina mama wajawazito na watoto chini ya miaka mitano. Upunguzaji wa vifo hivyo, wilaya itakuwa imepiga hatua kubwa kufikia lengo namba nne na tano la maendeleo ya milenia hadi kufika mwaka 2020”, alisema.

Aidha, Dkt Locye ametumia fursa hiyo kuomba wadau mbalimbali kuwaunga mkono katika kukamilisha jengo lao la kulaza wagonjwa (wodi).

“Wananchi wa jimbo la Iramba, tunaendelea kukushukuru wewe mbunge wetu Mwingulu kwa misaada mingi unayoendelea kuitoa kwenye maeneo mbalimbali katika kuboresha huduma za jamii, ikiwemo huduma muhimu za afya”, alisema.

Kwa upande wake Jumanne Hatibu mkazi wa kijiji cha Urughu tarafa ya Ndago alisema kabla ya ujio wa ambulance hiyo kijiji hicho kilikuwa kinakabiliwa na tatizo sugu la usafiri kwa wagonjwa hasa akina mama wajawazito.

“Kijiji chetu kwa miaka mingi tulikuwa tukitegemea usafiri wa basi na lilikuwepo basi moja tu. Likiondoka asubuhi kwenda Singida hakuna tena usafiri kwa siku husika hadi kesho asubuhi. Kwa hiyo kwa wagonjwa na hasa akina mama wajawazito, ilikuwa ni changamoto kubwa. Ambulance hii, itaokoa maisha ya wakazi wa tarafa ya Ndago na maeneo jirani”, alisema Hatibu ambaye ni mlemavu wa miguu.

Wakati huo huo, Mbunge Mwingulu ameahidi kuchangia ujenzi wa wodi ya kituo cha afya Ndago kwa kutoa mifuko mia moja ya saruji.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATANZANIA WATAKAOVAA JEZI ZA MAMELODI AU AL AHLY

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KOCHA BENCHIKHA AMESEPA

MASHUSHUSHU WA MAMELODI WALIKUJA KUTUPELELEZA: HERSI

KOCHA WA AL.AHLY ASEMA YANGA NI TIMU BORA NA NGUMU