NAMPENDA RAIS MAGUFULI




Ni Rais mzalendo kwa nchi yake. Ana uchungu sana kuona watu wanatajirika kwa rasilimali za umma. Ni kiongozi ambaye anataka kuona watu wananufaika kwa jasho halali na siyo upigaji.
Ni Rais jasiri mno. Anaweza kuingia kwenye anga ngumu na kuzitikisa. Kujenga nchi yenye heshima unahitaji kiongozi mkuu mwenye uthubutu kama Magufuli a.k.a John The Iron 'Chuma'.
Ni Rais ambaye yupo tayari kuingia kwenye mgogoro wowote wa ama ndani au nje, mradi tu asimamie kile ambacho anakiamini.
Iwe yupo sahihi au anakosea, ikiwa yeye anajiona yupo sahihi, Rais Magufuli huwa hapindi. Husimamia anachokiamini kwa nguvu zote.
Si mnafiki, si mwoga, si wa nyekundu na njano au nusu kwa nusu, akisema nyekundu, keshokutwa utamkuta na nyekundu yake. Hana ndimi mbili.
NAMPENDA TUNDU LISSU
Siku zote hutafuta makosa ya Serikali na kuyaweka wazi. Hata pale ambapo kila mtu huamini Serikali imepatia na kuishangilia, Lissu akiibuka utampenda tu.
Anafahamu mantiki ya kuwa mpinzani kwa nchi za Afrika hususan Tanzania. Anatambua kuwa yeye si sehemu ya watu wanaopaswa kuiimbia mapambio Serikali inapofanya vizuri. Anajua kuwa uhai wa upinzani ni makosa ya Serikali na Chama Tawala, kwa hiyo anakosoa tu.
Uzuri wa Lissu ni kwamba hakosoi ilimradi aonekane anakosoa, isipokuwa hukosoa kwa hoja na vielelezo yakinifu. Lissu akizungumza, hata kama sauti yake na maneno yake yanakera lakini wewe sikiliza ujumbe, hutaambulia sifuri.
Ukiona Lissu anafungua kinywa ujue amejipanga. Japo yapo maeneo mengi huonekana mpiga kelele lakini ukiona analibebea bango jambo ujue ana hoja za msingi.
Ni faida kubwa kuwa na Lissu katika nchi hii, maana haogopi kukosoa. Haogopi nafasi ya anayemkosoa.
Katika nchi ambayo watu wengi wanaogopa kufunua vinywa vyao kumkosoa Mkuu wa Nchi, angalau sauti ya Lissu itasikika ikikosoa. Akiwa bungeni au nje ya Bunge, msamiati unaoitwa woga, haumo kichwani kwa Lissu.
Unamhitaji Lissu kumfanya mtawala asibweteke. Hata kama mtawala anafanya vizuri, uwepo wa Lissu husaidia kuchokonoa hata makosa madogo yenye kujificha na kuyaweka wazi. Katika nchi ni hasara kubwa kukosa watu wa kuikosoa Serikali.
NAMPENDA ZITTO KABWE
Mwanasiasa muungwana na mzalendo kwa nchi yake. Si mtoa lugha za kushambulia, isipokuwa hujikita katika kujenga hoja zenye kuifaa nchi.
Ni mpinzani lakini Serikali inapofanya sawa husifia. Serikali inapokosea husimama na kukosoa bila woga.
Kila jambo linalofanyika kwa masilahi ya umma hutakosa kauli ya Zitto. Kauli yake inaweza kuwa chanya au hasi kulingana na mapokeo yake.
Tabia yake ya kuisifu Serikali inapofanya vizuri na kuikosoa inapofanya vibaya, humfanya wakati mwingine ajikute anapokea mashambulizi kila upande; kutoka Chama Tawala, vilevile kwa wapinzani wenzake.
Zipo nyakati Zitto hujikuta anatofautiana na wapinzani wenzake pale anapoona hawapo sawa. Ndiye mpinzani anayeongoza kwa kushambuliwa na wapinzani wenzake, wakati huohuo akishambuliwa na watu wa utawala.
Ni mwanasiasa mwenye maono makubwa. Hoja zake si za kukosoa tu, isipokuwa hukosoa, husahihisha na kuelekeza njia ya kufikia jawabu.
Akisimama bungeni huwa hasemi "Serikali imeshindwa", bali husema " Serikali inatakiwa ifanye haya ili ifanikiwe", daima hutoa hoja zenye thamani kubwa. Hutoa hoja za dhahabu. Zitto si mlalamikaji, ni mtoaji wa ufumbuzi kisha husherehesha ufumbuzi wake.
Wakati mwingine hoja zake na namna ambavyo huzitoa kwa uchambuzi wa kina, huwafanya watu waone anajifanya anajua. Kiukweli Zitto ni fundi hasa katika kujenga hoja.
Muogope sana Zitto akizungumzia jambo baada ya kitambo japo kifupi. Hapo ujue tayari ameshasoma na ameshakuwa na pointi nyingi kichwani.
Unamhitaji Zitto kwa ajili ya kupata sura ya pili, maana anapokosoa sura ya kwanza, huja na uchambuzi wa kina kuhusu faida za sura ya pili. Ndiye kiongozi mwenye hoja mbadala.
Ni tunu kwa nchi kuwa na Zitto Kabwe. Ni kiongozi ambaye huwa hafichi hisia zake. Akiumizwa huwa hanyamazi.
HITIMISHO
Tunamhitaji Rais Magufuli kwa nafasi yake na utashi wake wa kizalendo.
Tunamhitaji Lissu kwa jicho lake la kuyasaka makosa ya Serikali na kuyaweka wazi.
Tunamhitaji Zitto kwa maono mapana na hoja mbadala zenye tija kwa taifa.
Mwisho kabisa, Rais Magufuli, Lissu na Zitto wote ni Watanzania na wanaipenda sana nchi yao. Hilo ndilo ambalo naliona kwa wote hao.
Rais Magufuli anataka mabadiliko makubwa kwenye nchi ili taifa linufaike kwa rasilimali zake, hii ni kwa sababu Rais Magufuli anaipenda sana Tanzania yake.
Lissu anakosoa mbinu ambazo Rais Magufuli anazitumia kwa sababu anaona zinaweza kuigharimu nchi. Lissu anajua kuwa nchi haiwezi kubeba gharama bila yeye kuathirika. Hii ni kwa sababu Lissu anaipenda sana Tanzania yake.
Zitto anatoa hoja za utatuzi wa changamoto za sekta ya madini, akisahihisha hatua za Rais Magufuli kwa sababu anaamini kwamba Rais Magufuli hapaswi kuachwa peke yake kwenye vita hii ya uchumi kupitia madini ya Tanzania. Hii ni kwa sababu Zitto anaipenda sana Tanzania yake.
Nawapenda sana hawa wazalendo wa nchi hii. Kila mmoja ana nia njema. Ni vizuri kusikilizana na kukopeshana kama siyo kuazimana mawazo ili kufikia mafanikio ya pamoja kama nchi.
Tanzania haina malaika, kwamba akifanya jambo asikosolewe hata kama ni jema kiasi gani. Wanaokosoa nao ni Watanzania wazalendo. Vema kusikilizana. Mwisho kabisa wote wanaipenda Tanzania.
Wasioipenda Tanzania wote wapo kimya, hawana maoni, wala hawawezi kuingia kwenye malumbano, maana wanaogopa 'kuamsha dude', wakifunua vinywa watakumbushwa usaliti wao kwa nchi na wizi waliofanya.
Kila mtu aachwe huru kutoa maoni yake. Nchi inawahitaji Rais Magufuli, Lissu na Zitto kwa wakati mmoja.
Ndimi Luqman MALOTO

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

HATUTOPAKI BASI DHIDI YA YANGA-MOKWENA

“PEMBA SALUTI KWENU” DK. NCHIMBI*

DKT NCHIMBI AWAAHIDI MAKUBWA WANANCHI WA KWELA, RUKWA