Simba Wasafiri na Niyonzima Kigali


DAR ES SALAAM: WAKATI kiungo mchezeshaji wa Yanga, Haruna Niyonzima akitarajiwa kurudi nyumbani kwao Kigali, Rwanda kwa ajili ya kwenda kusheherekea Sikukuu ya Idd El Fitri, mabosi wa Simba wamepanga kupanda ndege kumfuata nyota huyo kwa ajili ya kumsainisha mkataba.
Hiyo, ikiwa ni siku moja ipite tangu kiungo huyo akutane na viongozi wa Yanga kwa ajili ya kufanya mazungumzo ya kumuongezea mkataba mwingine wa kubaki Jangwani.
Mnyarwanda huyo, hivi karibuni ilielezwa kuwa tayari amesaini mkataba wa miaka miwili kuichezea Simba kwenye msimu ujao wa Ligi Kuu Bara.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumatano, kiungo huyo siku yoyote kuanzia leo anatarajiwa kurejea Rwanda na familia yake kwa ajili ya kusherehekea sikukuu hiyo.
Mtoa taarifa huyo alisema, kutokana na mazungumzo waliyofanya na kiungo huyo kufikia muafaka viongozi wa Simba wamekubaliana na Niyonzima kumfuata Rwanda ili kukamilisha usajili huo.
Aliongeza kuwa, makubaliano waliyoafikiana ni kusaini mkataba wa miaka miwili kwa dau la Sh milioni 70 huku akilipwa mshahara wa Sh milioni 5 kwa kila mwezi kwa kipindi chote atakachoichezea Simba.
“Niyonzima tumefikia naye makubaliano mazuri ya kusaini mkataba wa kuichezea Simba kwenye msimu ujao na mkataba huo atausaini akiwa nyumbani kwao Kigali.
“Atasaini mkataba huo baada ya kukubaliana kwenye dau la usajili analolihitaji ambalo ni shilingi milioni 70 na mshahara wa shilingi milioni 5 atakaouchukua kwa kipindi cha miaka miwili atakayoichezea Simba.
“Alikuwa tayari kusaini mkataba huo hivi sasa lakini aliomba muda wa kuzungumza na klabu yake ya Yanga, hivyo amewatajia ofa yake na wanaonekana kushindwana,” alisema mtoa taarifa huyo.
Alipotafutwa Niyonzima kuzungumzia hilo alisema: “Nikwambie ukweli, nikiri kabisa Simba walinifuata kwa ajili ya mazungumzo ambayo hayakufikia muafaka mzuri kwani niliomba muda kwa ajili ya kuipa nafasi klabu yangu ya Yanga ambayo nipo kwenye mazungumzo nayo.
“Lakini hizo taarifa za mimi kusaini Simba au Yanga si kweli, ninashangaa kila siku jambo jipya linaibuka kuwa mimi nimesaini mkataba wa kuichezea Simba kitu ambacho siyo sahihi.
“Tangu tetesi zisambae nikwambie ukweli, sijalala usiku kutokana na usumbufu wa simu ninazozipokea kutoka kwa viongozi na mashabiki wa Yanga.
“Ili kukwepa usumbufu huu, nimeamua kuondoka na familia yangu kurudi nyumbani Rwanda ili nikapumzishe akili yangu,” alisema Niyonzima.
Mwandishi Wetu | Championi
0

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MATOKEO YA DARASA LA SABA 2013 YATOKA, YAPO HAPA ... YAONE HAPA KWA NJIA RAHISI KABISA

MATOKEO YA DARASA LA SABA YATANGAZWA

HIVI NDIVYO BIASHARA YA NGONO NAMNA INAVYOTIKISA MOROGORO: SEHEMU YA PILI.

MBUNGE MOLLEL AITAKIA NAMAINGO MAFANIKIO MEMA 2019

JIONEE WAREMBO KUMI WA NGUVU AFRIKA MASHARIKI

HIZI NDIO DALILI ZA VVU KWA WATOTO WADOGO

ANGALIA PICHA WADADA HAWA WALIVYOPIGWA