SOMA USIA BOMBA WA LUQMAN KWA MWANAWE WENYE MANUFAA KWA WOTE

MY CHERISHED SON, CAPTAIN AARIZ
Pokea salamu zenye upendo mnyoofu kutoka kwa mimi baba yako. Leo ukiwa unatimiza umri wa miaka 6, imempendeza Mungu niseme nawe japo kidogo.
Nafurahi unakua vizuri, naifurahia akili yako, naburudishwa na utundu wako, nahamasishwa na talanta zako. Wewe ni zawadi kubwa sana ambayo Mungu amenitunuku. Nakuahidi kukutunza kwa akili, moyo na mikono.
Unaishi hii dunia kwa mwaka wa sita sasa, nakuombea uishi zaidi. Umekuwa rafiki yangu siku zote, urafiki wenye upendo mkubwa. Nilikuwa nawe bega kwa bega tangu ukiwa tumboni mwa mama yako, nipo nawe hata sasa na tutaendelea kumbatana, maana wewe ni mimi mdogo.
Captain Aariz, ulilia ulipoguswa na hali ya hewa ya dunia kwa mara ya kwanza, kisha nilipokupakata na kukulaza kitandani kwa mara ya kwanza, uso wangu ulijaa tabasamu kwa ujio wako. Palepale nikasema wewe jina lako ni AARIZ, yaani mwanaume mwenye kuheshimika.
Captain Aariz, wewe ni mkazi wa hii dunia ambayo pia inaitwa ulimwengu, ndani ya ulimwengu wanaishi walimwengu, na katika walimwengu utayaona ya walimwengu kwa walimwengu.
Haya ya walimwengu kwa walimwengu ndiyo ambayo yalifanya nimuombe Mungu sana akunusuru na visa vya walimwengu mara tu nilipokushika kwa mara ya kwanza. Visa vya walimwengu vinaumiza sana. Ni suala la wakati tu, walimwengu watakuumiza tu, walimwengu hawaepukiki. Walimwengu ni kama maji!
Mimi ya walimwengu nayajua ndiyo maana nakusikitikia. Walimwengu wanaweza kukuumiza katika riziki zako, mapenzi yako na hata ujamaa wako. Hata hivyo, nilisema kuwa acha walimwengu wakuumize, ndivyo nawe utakuwa imara. Chuma kikishapitishwa kwenye moto mkali, hutoka kikiwa imara zaidi.
Captain Aariz, duniani kuna maadui. Watakuja kwa njia tofauti. Wapo watakaokuja kama marafiki, wengine kwa chuki ya wazi, hawatakosekana watakaolazimisha uadui nawe kwa sababu ya wivu. Nitakuandaa mwanangu.
Vilevile kwa vile kuna maadui na marafiki wapo, watakuja na utajumuika nao. Hata hivyo, adui mkubwa kuliko aina zote za maadui ni rafiki mnafiki. Rafiki aliye mnafiki huyo ni msaliti na anaweza kuuza wakati wowote. Nitakuandaa ujichunge.
Tafadhali sana Captain Aariz, naomba sana uwe mkweli. Ukweli utakujengea heshima na kuaminika. Jijengee sifa ya kuwa msimamisha ukweli. Hata hivyo, si kila uongo ni dhambi, ila nakuusia mwanangu, usiwe muongo-muongo, ni sifa mbaya mno.
Captain Aariz, hii dunia inakutaka uwakabili kwa ulaini wale watu ambao ni laini. Na uwakabili kwa ugumu wale wote ambao ni wagumu. Ukiwakabili kwa ugumu watu laini, utakuwa kituko! Ukiwakabili kwa ulaini watu wagumu, utachanwachanwa! Nitakufundisha kubadilika kulingana na mazingira.
Jiepushe sana na maisha ya chuki na visasi. Si kila jambo baya kwako lazima liamshe chuki au kila uliloumizwa utake matokeo kinyume kwa yule aliyekutendea. Hata hivyo, simaanishi uchekecheke hovyo pale unapoumizwa. Nitakujenga kuvikabili vishindo vya walimwengu na mzani wa kusamehe.
Ukishakuwepo duniani, akili yako ifanye kazi zaidi. Usije kuwa bendera fuata upepo au mtu wa mkumbo, hapana! Hiyo haitakuwa tafsiri ya jina lako. Jina lako linakutaka ujiamini, hivyo akili yako ikuongoze kuliko upepo. Ukiweza simama peke yako kwa jambo unaloliamini, hata kama kila mtu anakupinga.
Captain Aariz, utalinda heshima yako kama utatambua kuwa mahitaji ya kuishi duniani ni Upendo, Imani na Ujasiri. Na utambue yale ambayo ukitendewa yatakuumiza, basi na yenyewe usimtendee mwenzako. Hakuna binadamu aliyeumbwa na moyo wa plastiki.
Kataa wizi na aina yoyote ya udanganyifu. Amini kuwa Sh1,000 unayoivujia jasho ina heshima kubwa kuliko Sh1 bilioni ya udanganyifu. Amini katika kutafuta, amini katika kuishi kupitia jasho halali. Kwa vile bado nipo hai, nitazidi kukuelewesha.
Captain Aariz, siku zote za maisha yako hakikisha Mungu anakuwa wa kwanza. Usije kumshirikisha au kumlinganaisha Mungu na chochote. Mungu ni mmoja na ukiwekeza maisha yako kwake hakika hutaanguka. Utateleza lakini atakushika mkono usianguke, kisha atakuinua. Mungu ni mkuu wa kila kitu, hivyo unapomtegemea, maana yake unajiegemeza kwa asiyeshindwa na chochote.
Mpende mama yako, yeye ni shujaa wako. Nayajua mateso yake wakati wa safari yako ya kuja duniani. Ndiyo, hakuna mwingine anayejua kuliko mimi. Nilikuwa mlinzi wa karibu zaidi, niliyewalinda na kupambana kwa ajili yenu kipindi chote mkiwa wawili ndani ya mwili mmoja. Usije kuthubutu kumkosea adabu mama yako.
Captain Aariz, upendo wangu kwako na namna ninavyokujali, huakisi pia upendo na heshima kwa mama yako, maana bila yeye mimi nisingeitwa baba. Hivyo, mama yako pia ni shujaa wangu, kwani ametuunganisha kikamilifu.
Mwisho nakuomba umpende kila mtu na umheshimu kila aliye mbele yako. Duniani ulikuja bila chochote lakini milango ya kuingia kwenye vyumba vya mafanikio ipo hapahapa. Tambua kuwa funguo za milango hiyo zimeshikwa na watu. Wakati mwingine watu wenye funguo hizo huonekana hawana thamani.
Siku zote ishi ukiwa mnyenyekevu na usiwe mchokozi. Dunia haitaki mikogo hii. Siku ya kwanza utakapotoa machozi ya ukubwani, kitakuwa kipimo chako cha kwanza cha kutambua tafsiri ya walimwengu kwa walimwengu.
Nakupenda sana Captain Aariz Nyambo. Nikiwa hai, basi tutapepesuka na kuimarika pamoja. Hata hivyo, niwepo au nisiwepo, chagua kuwa mtu bora kila siku.
Narudia tena, nakupenda sana Captain Aariz Nyambo. Nakutakia heri katika siku yako hii ya kuzaliwa. HAPPY BIRTHDAY MY SON CAPTAIN AARIZ NYAMBO.
Ndimi baba yako.
Luqman MALOTO

0

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

HIVI NDIVYO BIASHARA YA NGONO NAMNA INAVYOTIKISA MOROGORO: SEHEMU YA PILI.

ANGALIA PICHA NDEGE KUBWA YA ABIRIA DUNIANI ILIYOANZA SAFARI NDEFU ZAIDI!

WAPENZI WANASANA WAKIFANYA MAPENZI GESTI

LICHA YA UZURI WAKE MWANADADA ELIZABETH MICHAEL a.k.a LULU SI MALI KITU MBELE YA RAY, AMKWEPA KUOGOPA AIBU.

IJUE HISTORIA YA UHASIMU WA KOREA KASKAZINI NA MAREKANI

KWA HERI KAMANDA WETU ABBAS KANDORO

YANGA SC WAANZA KAZI AFRIKA LEO…WANAKIPIGA NA U.S.M. ALGER SAA 4:00 USIKU ALGERIA

NCHI YA URUSI NDIYO NCHI INAYOONGOZA KWA KUWA NA UBORA WA ELIMU NA VYUO DUNIANI.

DC MJEMA AONJA ADHA YA MAFURIKO AKIKAGUA ATHARI ZA MAFURIKO ILALA