Wajue Wagombea wanane watakaowania urais Kenya Agosti


  • 30 Mei 2017
Kituo cha kusajili wapiga kura Kenya Januari 18, 2017Haki miliki ya pichaAFP
Image captionUchaguzi mkuu utafanyika tarehe 8 Agosti nchini Kenya
Tume Huru ya Uchaguzi Kenya (IEBC) imewaidhinisha wanasiasa wanane ambao watawania urais katika uchaguzi mkuu Agosti mwaka huu.
Walioidhinishwa ni pamoja na Rais Uhuru Kenyatta wa chama cha Jubilee ambaye atakuwa anawania kuongoza nchi hiyo kwa muhula wa pili, na kiongozi wa muda mrefu wa upinzani Bw Raila Odinga ambaye anawania urais kwa mara ya nne.
Bw Odinga, aliyehudumu kama waziri mkuu katika serikali ya muungano ya Rais Mwai Kibaki kati ya 2008 na 2013, anawania urais chini ya umoja wa vyama vya upinzani kwa jina National Super Alliance (NASA).
Katika uchaguzi huo wa tarehe 8 Agosti, kutakuwa na wagombea wanne pia ambao ni wagombea huru (hawana vyama).

Abduba Dida

Anawania urais kupitia chama cha Alliance for Real Change (ARK) na muungano wa Tunza Coalition.
Alikuwa mwalimu wa shule ya upili ya Lenana jijini Nairobi.
Hii ni mara yake ya pili kuwania urais baada ya mwaka 2013 ambapo alipata kura 52,848 na kumaliza wa tano.

Cyrus Jirongo

Ni mwanasiasa na mfanyabiashara ambaye ni mara yake ya kwanza kuwania urais.
Anawania kupitia chama cha United Democratic Party (UDP).
Alipata umaarufu kisiasa mwaka 1992 alipokuwa katika kundi la vijana wa chama cha KANU, Youth for KANU 1992 waliokuwa wakimfanyia kampeni Rais Daniel arap Moi wakati wa uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi mwaka huo.

Ekuru Aukot

Anawania urais kupitia chama cha Thirdway Alliance Kenya (TAK), na ni mara yake ya kwanza kuwania urais.
Alihudumu kama katibu katika Kamati ya Wataalamu waliosaidia kutunga Katiba Mpya ya Kenya ambayo iliidhinishwa na kuanza kutekelezwa mwaka 2010.
Asili yake ni Kapedo, Turkana kaskazini magharibi mwa Kenya na amejitangaza kama mtu anayeleta mwamko mpya katika uongozi nchini Kenya. Amekuwa pia akitetea makabila madogo.

Japhet Kaluyu

Ni mgombea huru ambaye amerejea nchini Kenya hivi majuzi kutoka Marekani. Amejieleza kama mwalimu, mshauri na mwandishi ambaye ana uzoefu wa kufanya kazi Wall Street. Anasema amebobea katika utafiti katika sekta ya afya na msomi.
Ni mara yake ya kwanza kuwania urais.

Joseph Nyagah

Ni mwanasiasa wa muda mrefu nchini Kenya ambaye alihudumu kama waziri wa vyama vya ushirika chini ya Rais Mwai Kibaki, na baadaye akawa mshauri wa Rais Kenyatta.
Babake, Jeremiah Nyagah, alikuwa waziri wakati wa utawala wa mwanzilishi wa taifa la Kenya Jomo Kenyatta.
Bw Nyagah, ambaye alikuwahi kuwakilisha Kenya katika Umoja wa Ulaya, alihudumu kama mbunge wa eneo la Gachoka, Kaunti ya Embu mashariki mwa Kenya kabla ya kuteuliwa waziri.
Anasema ndiye pekee anayeweza kutatua matatizo yanayoikumba Kenya, kutokana na uzoefu wake katika uongozi. Akihojiwa na runinga ya NTV baada ya kuidhinishwa, alidokeza kwamba aliacha kazi yake ya kuwa mshauri wa rais baada ya kugundua kwamba ushauri aliokuwa anaoutoa haukuwa unafuatwa.

Prof Michael Wainaina

Yeye ni mgombea huru ambaye amekuwa mhadhiri wa fasihi katika Chuo Kikuu cha Kenyatta.
Amekuwa mkosoaji mkuu wa mfumo wa sasa wa kisiasa Kenya na pia mchanganuzi wa siasa.
Anasema aliamua kuwa mgombea huru kwa sababu vyama haviwapi nafasi vijana na wanawake.

Raila Odinga

Bw Raila OdingaHaki miliki ya pichaAFP/GETTY
Ni kiongozi wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM) ambaye anawania chini ya muungano wa vyama vya upinzani kwa jina National Super Alliance (NASA).
Aliwahi kuhudumu kama waziri mkuu wa kwanza wa Kenya, wadhifa ulioundwa kufuatia Mkataba wa Kitaifa ulioafikiwa kumaliza ghasia za baada ya uchaguzi mwaka 2007-2008, ambapo aligawana mamlaka na Rais Mwai Kibaki.
Ni mara yake ya nne kuwania urais Kenya. Mwaka 2013, akiwa bado na mgombea wake wa sasa Makamu wa Rais wa zamani Kalonzo Musyoka, alishindwa na Rais Uhuru Kenyatta. Alipinga matokeo hayo mahakamani lakini mahakama ikatupilia mbali kesi hiyo.

Uhuru Kenyatta

Anawania kwa muhula wa pili kupitia chama cha Jubilee Party ambacho asili yake ni muungano wa Jubilee wa vyama vya TNA na URP alioutumia kushinda urais mwaka 2013.
Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya
Ni mwanawe mwanzilishi wa taifa la Kenya Mzee Jomo Kenyatta.
Mgombea wake mwenza ni Bw William Ruto kutoka eneo la Bonde la Ufa la Kenya.
Wawili hao wanawaomba wapiga kura kuwachagua tena kuendeleza maendeleo ambayo wanaamini serikali yao imetekeleza katika kipindi cha miaka minne ambayo wamekuwa madarakani.
Bw Kenyatta aliwania urais mara ya kwanza 2002 dhidi ya Mwai Kibaki kupitia chama kilichokuwa kinatawala wakati huo, chama cha KANU cha Rais Moi aliyekuwa anaondoka madarakani baada ya kuongoza kwa miaka 24.
Alishindwa na akawa kiongozi wa upinzani na kwa pamoja na Bw Odinga wakafaulu kupinga Katiba Mpya iliyopendekezwa mwaka 2005. Mwaka 2007, alimuunga mkono Rais Kibaki uchaguzini.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATANZANIA WATAKAOVAA JEZI ZA MAMELODI AU AL AHLY

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KOCHA BENCHIKHA AMESEPA

MASHUSHUSHU WA MAMELODI WALIKUJA KUTUPELELEZA: HERSI

KOCHA WA AL.AHLY ASEMA YANGA NI TIMU BORA NA NGUMU