Waziri Lukuvi Kupewa Tuzo ya Uwajibikaji na Utendaji Bora


Na Jonas Kamaleki- MAELEZO.

Viongozi wa Dini wanajiandaa kumpa tuzo Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. William Lukuvi kwa utendaji mzuri uliojaa ubunifu na uwajibikaji.

Hayo yameelezwa katika mahojiano maalum jijini Dar es salaam na Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Maadili na Haki za Binadamu kwa Jamii ya Dini zote Tanzania, Askofu William Mwamalanga.

Askofu Mwamalanga amesema kuwa Waziri Lukuvi amekuwa kiongozi imara katika kufuatilia masuala yanayohusu ardhi ikiwemo utatuzi wa migogoro ambayo imedumu kwa muda mrefu.

“Lukuvi ameing’arisha Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuendana na kasi ya Rais John Pombe Magufuli, hakika amevaa viatu vya Magufuli, hivyo tumeamua kumpa tuzo maalum kwa ajili utendaji wake”, alisema Askofu Mwamalanga.

Ameeleza kuwa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imefanya jambo zuri kwa kutoa elimu ya ardhi kiasi kwamba karibu kila mtu amefahamu matumizi ya ardhi na umuhimu wake.

Askofu Mwamalanga amesema kuwa ardhi imefanywa kuwa lulu na kufanya sura mpya ya ardhi kuonekana ambapo takriban asilimia 85 ya Watanzania wameiona kuwa ni mali.

Mhe. Lukuvi amewapa nafasi ya kwanza wananchi kuliko Sheria jambo ambalo limewafanya Watanzania kujisikia kuwa wanathaminiwa na Serikali yao, aliongeza Askofu Mwamalanga.

Kiongozi huyo wa Dini amesema kuwa Mhe. Lukuvi ni mfano wa kuigwa na mawaziri na viongozi wenzake kwa uchapakazi wake. Amesema kuwa ni Waziri ambaye anawashirikisha watendaji waliochini yake katika maamuzi mbali mbali, hivyo anastahili kupewa tuzo.

“Tumepanga kumpa tuzo Waziri Lukuvi kwa kuzingatia yafuatayo: Kuiweka ardhi mikononi mwa watanzania, kuonyesha kuwa ardhi ni chanzo kikuu cha uchumi wa watu na utatuzi wa migogoro ya ardhi hasa iliyodumu kwa muda mrefu”, alisema Askofu Mwamalanga. 

Migogoro hiyo ni kama vile mgogoro wa kijiji cha Mabwegere, Mkoani Morogoro, mgogoro wa Chasimba, jijini Dar es Salaam na migogoro mingine mingi katika mikoa ya Arusha, Mbeya, Kigoma, Tanga na Mwanza.

Askofu Mwamalanga amesema Kamati yake imewasiliana na Taasisi mbalimbali za Serikali na binafsi ili watoe mapendekezo ya tuzo ambayo anastahili kupewa Mhe. Lukuvi kwa utendaji kazi wake mzuri. 

Amezitaja baadhi ya Taasisi hizo kuwa ni Vyuo Vikuu vya Umma na Binafsi, Marais wastaafu na mawaziri wakuu wastaafu, Vyama vyote vya siasa ambavyo kwa ujumla wake vimeonyesha kutambua mchango wa waziri Lukuvi.

Baada ya kupokea mapendekezo na kuyafanyia kazi ndipo itatangazwa siku ya kutoa tuzo hiyo kwa Mhe. Lukuvi, alisema Askofu Mwamalanga.

Tangu Waziri Lukuvi aiongoze Wizara ya ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi mwisho mwa uongozi wa awamu ya Nne hadi sasa, 

mabadiliko yenye tija katika wizara hiyo yameonekana. Migogoro mingi ya ardhi imetatuliwa, utoaji wa hati za viwanja umerahisishwa na huduma kwa wateja imeboreshwa.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

HATUTOPAKI BASI DHIDI YA YANGA-MOKWENA

“PEMBA SALUTI KWENU” DK. NCHIMBI*