WAZIRI MKUU KASSIM MAJALIWA AFUTARISHA CHATO , AKIWA NJIANI AZUNGUMZA NA WANANCHI WA KIGONGO FERI



 Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akishiriki  katika swala ya magaharibi katika  futari iliyoandaliwa na Waziri Mkuu mjini  Chato, mkoani Geita, Juni 21, 2017.  (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
 Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akifuturu pamoja na Askofu Mussa Magwesera wa Kanisa la African Inland Church (AIC)  Dayosisi ya Geita (kushoto) na Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Geita, Alhaj Yusuph Kabaju(kulia) katika futari iliyoandaliwa na Waziri Mkuu kwa niaba ya Rais John Pombe Magufuli, mjini  Chato, mkoani Geita  Juni 21, 2017. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akisalimiana na Askofu Mussa Magwesera wa Kanisa la African Inland Church (AIC), Dayosisi ya Geita katika futari iliyoandaliwa na Waziri Mkuu kwa Niaba ya Rais John Pombe Magufuli  mjini  Chato mkoani Geita  Juni 21, 2017. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
 Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza  na wananchi wa eneo la Kigongo feri Wilaya ya Misungwi, wakati aliposimama kwa muda akiwa njiani kuelekea Chato kwa ziara ya siku mbili  Juni 21, 2017.  (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
 Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akisalimiana na Mkuu wa Mkoa wa Geita,Meja Jenerali Mstaafu,  Ezekiel Kyunga wakati alipowasili mjini Chato mkoani Geita  Juni 21, 2017 kwa ziara ya siku mbili mkoani humo. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)


*Ahimiza nyumba za ibada zisitumiwe vibaya 

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewaomba waumini wa dini za Kiislamu na Kikristo nchini wahakikishe nyumba zao za ibada hazitumiki kuleta migogoro. 

Ametoa ombi hilo jana usiku (Jumatano, Juni 21, 2017) wakati akizungumza na mamia ya waumini wa dini za Kikristo na Kiislamu pamoja na viongozi wa dini walioshiriki ibada ya futari wilayani Chato, mkoani Geita. 

Akizungumza na waumini hao kwa niaba ya Mheshimiwa Rais, Dk. John Pombe Magufuli, Waziri Mkuu alisema Mheshimiwa Rais alishapanga kufika Chato ili kushiriki nao ibada ya iftar lakini ametingwa na majukumu ya kitaifa akaona ni vema amtume yeye ili amwakilishe.

“Mheshimiwa Rais alishapanga kuja Chato kufuturu pamoja na wana-Chato lakini kadri siku zinavyozidi kwenda anajikuta anabanwa na majukumu mengi ikiwemo kukutana na wageni wa kimataifa, kwa hiyo akaona ni vema nije kumwakilisha katika shughuli hii,” alisema.

“Mheshimiwa Rais anawaombea heri katika siku zilizobakia za mfungo wa Ramadhan ili mmalize salama na Mungu akijalia muweze kusherehekea pamoja, na pia anawatakia heri wale watakaoendelea na sita tushawal.”

Akisisitiza kuhusu amani na utulivu nchini, Waziri Mkuu alisema: “Hatupendi kusikia kuwa msikiti fulani wamechapana viboko kwa sababu ya kugombea uongozi au kwenye kanisa fulani waumini wamepigana wakigombea mchungaji wao.”

“Tutumie nyumba zetu za ibada kudumisha amani na mshikamano wetu. Napenda niwahakikishie kuwa Serikali yenu chini ya Rais John Pombe Magufuli itaendelea kuheshimu dini zote.”

Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuwakumbusha waumini hao kwamba mwezi mtukufu wa Ramadhan ni wa toba kwa kila muumini. “Huu mwezi mafundisho yake yanasisitiza amani, uvumilivu na kusameheana. Nipende kuwasihi kwamba tuendelee kudumisha utulivu tulionao,” aliongeza.

“Nipende kusisitiza kwenu wana-Geita na wana-Chato kwamba jukumu kubwa mlilonalo ni kuendelea kumuombea Mheshimiwa Rais ili Mwenyezi Mungu amjalie afya njema, busara na uongozi wa kimungu katika maamuzi yake. Niwasihi ndugu zangu Waislamu na Wakristo, tuendelee kuwaombea viongozi wote wa kitaifa kila siku ili wafanye kazi kwa kuongozwa na Mungu,” alisema.

Awali, akisoma risala mbele ya Waziri Mkuu, Katibu wa BAKWATA Wilaya ya Chato, Sheikh Ally Moto alisema wanamshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuwapa fursa ya kuweza kushiriki ibada ya iftar pamoja na watoto yatima na wajane.

Alisema wanaunga mkono jitihada zinazofanywa na Serikali ya awamu ya tano na ili kudumisha amani wilayani humo, waumini wa Kiislamu na Kikisto wameunda Kamati ya Amani ya wilaya hiyo inayojulikana kama Interfaith Committee. 

Naye Mbunge wa Chato ambaye pia ni Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk. Medard Kalemani alisema anamshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuandaa futari hiyo ambayo imejumuisha wana Chato kutoka pembe nne za wilaya hiyo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti Mwenza wa Kamati ya Amani ya Mkoa wa Geita, Askofu Mussa Magwesera wa Kanisa la African Inland Church (AIC), Dayosisi ya Geita alitoa shukrani kwa Mheshimiwa Rais Magufuli na kuwapongeza viongozi wakuu wa kitaifa kutokana na utendaji wao unaogusa mioyo ya Watanzania.

“Ninyi wote watatu ni viongozi ambao Mungu amewaweka kuongoza nchi yetu. Katika miezi hii 18, mmefanya mambo makubwa, ni imani yetu kuwa ataendelea kuwaongoza katika utendaji kazi wenu,” alisema.

Akitoa shukrani, Sheikh wa Mkoa wa Geita, Sheikh Yusuph Kabaju ambaye pia ni Mwenyekiti Mwenza wa Kamati ya Amani ya Mkoa huo, alimshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuwapa fursa wana-Geita kujumuika pamoja katika futari hiyo na kuahidi kudumisha amani ya Tanzania.

“Tunakushukuru kwa kutuunganisha wana Geita katika futari hii japo umeamua kufanyia ibada hii hapa Chato. Maneno ya Quran tukufu yanasema malipo ya waliofunga anayapata pia yule aliyefuturisha waliofunga,” alisema.

Sheikh Kabaju pia alisoma dua ya kumuombea Mheshimiwa Rais Magufuli pamoja na viongozi wa kitaifa. Pia aliombea amani kwa ajili ya Taifa la Tanzania.



IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU, 

ALHAMISI, JUNI 22, 2017.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

HATUTOPAKI BASI DHIDI YA YANGA-MOKWENA

“PEMBA SALUTI KWENU” DK. NCHIMBI*