MAGURI AIPELEKA TAIFA STARS NUSU FAINALI COSAFA


Na Mwandishi Wetu, RUSTERNBURG
BAO pekee la mshambuliaji Elias Maguri limetosha kuipeleka Tanzania Nusu Fainali ya michuano ya Kombe la COSAFA Castle baada ya kuwalaza wenyeji 1-0 jioni ya leo Uwanja wa Royal Bafokeng, Rusternburg.
Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Olivio Saimone wa Msumbiji aliyesaidiwa na Matheus Kanyanga wa Namibia na Jackson Pavaza wa Namibia, Maguri alifunga bao hilo dakika ya 18 kwa shuti la mahesabu baada ya pasi ndefu ya kiungo Muzamil Yassin, Stars ikitoka kushambuliwa.
Tanzania sasa itamenyana na Zambia Jumatano katika Nusu Fainali, wakati Afrika Kusini wanaangukia kwenye michuano ya Plate, inayohusisha timu zilizotolewa hatua ya Robo Fainali.

Elias Maguri amefunga bao pekee Taifa Stars ikiilaza Bafana Bafana 1-0 na kwenda Nusu Fainali ya Kombe la COSAFA Castle leo

Kocha Salum Mayanga alimuanzisha kwa mara ya kwanza kiungo Raphael Daudi Luth na akacheza vizuri, kabla ya kuumia dakika ya 84 na kutolewa kwa machela, huku nafasi yake ikichukuliwa na Salmin Hoza dakika nne baadaye.
Sifa za ushindi wa leo ni kwa timu nzima katika kile kilichoonekana kucheza kwa kufuata maelekezo ya benchi la Ufundi, lakini zaidi safu ya ulinzi leo ilicheza kwa utulivu wa hali ya juu na kumlinda vizuri kipa Aishi Maula aliyefanya kazi nzuri ya kuokoa michomo kadhaa ya hatari.
Bafana Bafana walicharuka mno ndani ya dakika 10 za mwisho, lakini bado Taifa Stars walitulia na kuhimili vishindo vyao hatimaye kumaliza na ushindi wa 1-0. 
Huu ulikuwa mchezo wa tatu kihistoria kuzikutanisha nchi hizo, mbili na mara ya kwanza kabisa katika Kombe la COSAFA.
Mechi mbili zilizopita Bafana chini ya kocha Pitso Mosimane iliilaza 1-0 Tanzania, bao pekee la Siyabonga Sangweni Mei 14, mwaka 2011 Uwanja wa Taifa baada ya Oktoba 26, mwaka 2002, Tanzania kushinda kwa penalti 4-3 baada ya sare yab 0-0 kwenye Kombe la CECAFA Castle.
Kikosi cha Afrika Kusini; Boalefa Pule, Thendo Mukumela, Innocent Maela, Lorenzo Gordinho, Mario Booysen, Lehlogonolo Masalesa, Cole Alexander, Riyaad Norodien/Lebogang Maboe dk77, Jamie Webber, Liam Jordan na Judas Moseamedi/Mohau Mokate dk60.
Tanzania; Aishi Manula, Shomary Kapombe, Gardiel Michael, Salim Mbonde, Erasto Nyoni, Himid Mao, Muzamil Yassin, Raphael Daudi/Salmi Hoza dk89, Thomas Ulimwengu/Msuva dk49, Elias Maguri na Shiza Kichuya/Hamim Karim dk90.
0

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MATOKEO YA KIDATO CHA PILI, DARASA LA SABA YATANGAZWA ZANZIBAR

HIVI NDIVYO BIASHARA YA NGONO NAMNA INAVYOTIKISA MOROGORO: SEHEMU YA PILI.

ZAIDI YA WANANCHI 500 KUSHIRIKI MAFUNZO YA MKIKITA YA KILIMO CHA PAPAI SALAMA

MKIKITA YATOA OFA KWA KILA HEKA YA PAPAI SH. MIL. 2 KUTANDAZA MIUNDOMBINU YA UMWAGILIAJI

WATEJA WA NSSF DAR WATIMULIWA KWA MTUTU WA BUNDUKI

KAMISHNA MARIJANI AZINDUA CHAMA CHA WAFUGAJI MBWA TANZANIA (TCA)

PICHA:NYOKA AINA YA CHATU AUWAWA KANISANI BAADA YA KUKUTWA NYUMBANI KWA MFANYABIASHARA MAARUFU JIJINI ARUSHA AKISADIKIWA KWA IMANI ZA KISHIRIKINA

MATOKEO YA DARASA LA SABA YATANGAZWA