MASAUNI, MKUU WA WILAYA MUHEZA WAFANYA OPARESHENI USIKU KUWASAKA WAHALIFU MSITU WA AMANI MKOANI TANGA


Na Felix Mwagara (MOHA) 
NAIBU Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni ameongozana na Mkuu wa Wilaya ya Muheza, Mkoani Tanga kufanya operesheni ya kuwasaka waharibifu  wa chanzo cha maji cha Mto Zigi ambao unapeleka maji Tanga mjini.
Masauni alifika katika eneo hilo la tukio saa mbili usiku na kujionea maeneo yaliyoharibiwa kwa kuchimbwa mashimo makubwa na wahalifu hao wakidai kuwa wanatafuta madini ya dhahabu. Hata hivyo, hakuna mhalifu aliekamatwa katika eneo hilo wakati wa oparesheni hiyo.

Akizungumza katika eneo hilo lililopo Tarafa ya Amani, wilayani humo jana, Masauni ambaye pia aliambatana na Mbunge wa Jimbo la Muheza, Balozi Adadi Rajabu, alisema Jeshi la Polisi litaendelea kufanya oparesheni katika eneo hilo usiku na mchana kwa kushirikiana na walinzi wa msitu  ili kuwaondoa wahalifu hao haraka iwezekanavyo.
Masauni alisema licha ya Polisi kuendelea kufanya doria katika eneo hilo lakini wanatarajia kufungua kituo cha polisi ili kuongeza ulinzi zaidi katika eneo hilo muhimu ambalo ndio chanzo cha maji kwa sehemu kubwa ya wakazi wa Mji wa Tanga. 
“Tumepanga kuimarisha ulinzi zaidi katika eneo hili kwa kujenga kituo cha polisi ambapo askari wetu watashirikiana na walinzi wa misitu kufanya doria ya kupambana na wahalifu,” alisema Masauni na kuongeza; 
“Kwa habari zisizo rasmi tulizozipata katika vyanzo vyetu, hawa wahalifu wanamtandao mkubwa wakishirikiana na watu mbalimbali wakiwemo wafanyabiashara na hata baadhi ya watumishi wa umma, tutaendelea kufanya uchunguzi huu kwa kina kwa kushirikiana na ofisi ya mkuu wa wilaya ili kuwabaini wahalifu wote haraka iwezekanavyo.” 
Hata hivyo, Masauni alifafanua kuwa, watafanya uchunguzi wa kina kuwachunguza wale wote waliohusika kuwaficha wahalifu iwe askari polisi, iwe mamlaka yoyote nyingine, iwe hakimu au watu wa aina yoyote watachunguzwa. Watanzania tunapaswa tulinde rasilimali za Taifa pamoja na kusimamia ipasavyo. 
Masauni alitarajia kwenda mkoani Kilimanjaro kuendelea na ziara yake lakini mara baada ya kupewa taarifa kuhusu uharibifu mkubwa unaofanywa na wahalifu katika msitu huo wa asili, ndipo akaelekeza safari ya kwenda eneo hilo kwanza kuangalia hali halisi pamoja na kuwasaka wahalifu hao ambao inasemekana wana watu hao wanapoona msafara unakuja katika eneo hilo, wanaambizana na utoweka haraka katika eneo hilo. 
Katika ziara yake ya siku moja mkoani humo, kwa kutembelea mjini Tanga, Wilaya ya Pangani na baadaye akamalizia Wilaya ya Muheza, Masauni alitoa maelekezo mbalimbali kwa Taasisi zilizochini ya Wizara yake hasa  Jeshi la Polisi na Uhamiaji kuakikisha wanaongeza nguvu kubwa ya kuchunguza na kuzidi kuwasaka wahamiaji haramu mkoani humo, na pia aliamuru ujenzi wa Gereza la Muheza kuanza mara moja ili kupunguza msongamano mkubwa uliopo katika Gereza Kuu la Tanga pamoja na mengineyo. 
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya Muheza,  Mhandisi Mwanaasha Tumbo alimshukuru Naibu Waziri huyo kwa kufanya ziara katika wilaya yake, na pia alishukuru kwa kuamuru ujenzi wa Gereza Muheza kuanza mara moja na kuahidi kuyafanyia kazi zaidi maelekezo mbalimbali aliyoyatoa wilayani humo. 

Hata hivyo, Mhifadhi Msaidizi wa Hifadhi hiyo ya Asili, Bob Matunda alisema mara kwa mara wanawakamata wahalifu hao na kuwafikisha katika vyombo vya usalama, na akaahidi kuwa wataendelea kushirikiana kikamilifu na Jeshi la Polisi katika oparesheni mbalimbali za kuwaondoa wahalifu hao katika eneo hilo.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

HATUTOPAKI BASI DHIDI YA YANGA-MOKWENA

“PEMBA SALUTI KWENU” DK. NCHIMBI*