4x4

MTANGAZAJI AZAM TV, FATNA RAMOLE ALIYEKUWA HAJULIKANI ALIPO KWA SAA 48, APATIKANA


Saa kadhaa baada ya kuanza kusambaa kwa taarifa za kupotea kwa mtangazaji wa Runinga ya Azam TV, Fatna Ramole, ikidaiwa kwamba alikuwa hajulikani alipo kwa zaidi ya saa 48, hatimaye mwanadada huyo amepatikana akiwa kwenye moja ya hospitali za jijini Dar es Salaam, akipatiwa matibabu kwa kile kilichoelezwa kwamba alipata ajali mbaya.
Mtu wa kwanza kutoa taarifa za kupotea kwa mwanadada huyo, alikuwa ni ndugu yake aitwaye Lulu Ramole ambaye alituma ujumbe uliokuwa ukisomeka kwamba dada yake ametoweka kwa zaidi ya saa 48 na hajulikani alipo, akaomba yeyote aliyekuwa na taarifa za mahali alipo, atoe taarifa.
Saa kadhaa baadaye, taarifa hizo zilikuwa zimesambaa kwa kasi kubwa kwenye mitandao ya kijamii, kila mmoja akitaka kujua nini kimetokea. Katika kuchimba kwa kina, mtandao huu uliwasiliana na mmoja kati ya wafanyakazi wenzake Fatna kutaka kujua nini kimetokea.
Mmoja kati ya wafanyakazi wa Azam TV aliyeomba hifadhi ya jina lake, alisema Fatna amepatikana akiwa anatibiwa kwenye hospitali moja jijini hapa baada ya kupata ajali mbaya juzi, maeneo ya Bamaga, Karibu na Chuo cha Ustawi wa Jamii ambapo alijeruhiwa sehemu mbalimbali za mwili wake na kupelekwa hospitali.
“Katika ajali aliyoipata, inaonesha kuna watu walimuibia simu pamoja na vitu vyake vingine maana kwa mara ya mwisho simu yake inaonekana ilikuwa Makongo. Tunamshukuru Mungu kwamba yupo salama, tunaomba msambaze taarifa kwa watu wengine kwamba Fatna amepatikana na alikuwa amepata ajali,” alisema.
Tunaendelea kuzifuatilia taarifa hizi kwa karibu, tutazidi kuwajuza kitakachojiri.
Post a Comment