SERIKALI ‘YAMTUMBUA’ MALINZI WA BMT


WAZIRI wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe amesitisha uteuzi wa Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Dioniz Malinzi na Wajumbe wake wote na kuiagiza Sekretarieti kuendelea na kazi kwa kushirikiana na Serikali.
Akizungumza na Waandishi wa Habari leo ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO) mjini Dar es Salaam, Dk. Mwakyembe amesema kwamba amevunja Baraza hilo baada ya kuona mapungufu mengi.
Amesema kwamba amebaini changamoto nyingi kwenye baraza hilo zinazotokana na utendaji mbovu wa baadhi ya viongozi wa BMT, akiwemo Mwenyekiti, Malinzi na Wajumbe wake.
Dioniz Malinzi amevuliwa Uenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) na Serikali
Mwakyembe amesema kuwa sekretarieti ya baraza hilo inayoongozwa na Kaimu Katibu Mkuu, Mohammed Kiganja itaongoza shughuli zote za kiutendaji kwa kushirikiana na serikali hadi pale utakapofanyika uteuzi wa Mwenyekiti na wajumbe wengine.
Dkt. Mwakyembe amesema katika mapitio aliyoyafanya amegundua kuwa kuna ubabaishaji mkubwa unaofanywa katika sekta ya michezo, ikiwemo viongozi wa michezo kushika zaidi ya nyadhifa moja, ushiriki wa wanamichezo nje ya nchi bila ya kuitaarifu BMT na mapromota wa mchezo wa ngumi kuandaa mapambano bila ya kusajiliwa.
Dkt. Mwakyembe pia alisema amegundua kuwa chaguzi za vyama vya michezo kugubikwa na ubabe na rushwa, Katiba na kanuni za vyama vya michezo kukosa uhakiki, kubaini upungufu kuhusu masuala ya fedha, tuhuma za rushwa, ubadhilifu, upendeleo, maamuzi ya kibabe na kutofatiliwa na kufanyiwa kazi ipasavyo.
Aidha ameongeza kuwa uongozi wa Malinzi ulichangia kudumaza mwenendo wa michezo nchini kutokana kutofuatilia mambo ya msingi na badala yake kufanya ubabaishaji kwenye maamuzi sahihi kwenye vyama vya michezo na klabu.
Dk. Mwakyembe alisema Serikali ilitarajia BMT ingepata ufumbuzi juu ya migogoro mbalimbali ya vyama vya michezo, mapromota na klabu za michezo nchini, lakini haikutenda haki ambapo ilijikita zaidi kwenye maslahi binafsi.
Amesitisha uteuzi wa viongozi hao kwa kuwa serikali ya awamu ya tano inahitaji mikakati mipya na nguvu mpya kwenye sekta ya michezo ili kupata maendeleo.
Haya yanatokea, wakati aliyekuwa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi,  mdogo wa Dioniz yuko rumande katika gereza la Keko pamoja na Katibu wa TFF, Selestine Mwesigwa na Mhasibu, Nsiande Isawafo Mwanga walipelekwa rumande Keko Juni 29 baada ya kusomewa mashitaka 28 ya kughushi na kutakatisha fedha kupitia akaunti ya TFF iliyopo katika banki ya Stanbic, Dar es Salaam.
Walirudishwa Mahakamani Julai 3, ambako walinyimwa dhamana tena na kurejeshwa rumande hadi Julai 17, upepelezi wa kesi yao utakapokamilika.
Katika mashitaka hayo, 25 yanakwenda moja kwa moja kwa Rais wa shirikisho hilo, Malinzi akidaiwa kughushi michakato mbalimbali ya kifedha, huku matatu yakiwahusu wote na Katibu wake na Mhasibu wake Nsiande Isawafo Mwanga.

0

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MATOKEO YA KIDATO CHA PILI, DARASA LA SABA YATANGAZWA ZANZIBAR

HIVI NDIVYO BIASHARA YA NGONO NAMNA INAVYOTIKISA MOROGORO: SEHEMU YA PILI.

ZAIDI YA WANANCHI 500 KUSHIRIKI MAFUNZO YA MKIKITA YA KILIMO CHA PAPAI SALAMA

MKIKITA YATOA OFA KWA KILA HEKA YA PAPAI SH. MIL. 2 KUTANDAZA MIUNDOMBINU YA UMWAGILIAJI

WATEJA WA NSSF DAR WATIMULIWA KWA MTUTU WA BUNDUKI

DIAMOND AITWA NA NYOTA YAJAA GOMS

KAMISHNA MARIJANI AZINDUA CHAMA CHA WAFUGAJI MBWA TANZANIA (TCA)

PICHA:NYOKA AINA YA CHATU AUWAWA KANISANI BAADA YA KUKUTWA NYUMBANI KWA MFANYABIASHARA MAARUFU JIJINI ARUSHA AKISADIKIWA KWA IMANI ZA KISHIRIKINA