HATIMAYE TSHITSHIMBI AWASILI KAMBINI YANGA PEMBA


Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
HATIMAYE kiungo Papy Kabamba Tshishimbi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), leo amewasili kisiwani Pemba kuungana na wachezaji wenzake wapya wa klabu ya Yanga kwa maandalizi ya mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya mahasimu, Simba SC Jumatano Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Yanga, Dissmas Ten ameiambia Bin Zubeiry Sports – Online leo kwamba Tshishimbi aliingia kambini jana baada ya kukamilisha taratibu zote za msingi zilizomchelewesha kuungana na wenzake mapema. 
“Tshitshimbi alichelewa kidogo kwenda Pemba kutokana na taratibu za muhimu ambazo ilibidi lazima azikamilishe kwanza na baada ya hapo ameondoka jana kwenda kambini,”amesema Ten.
Papy Kabamba Tshishimbi amewasili kisiwani Pemba leo kuungana na wachezaji wenzake wa Yanga kwa maandalizi ya mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Simba Jumatano Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 27 ambaye inaaminika ndiye mrithi wa Mnyarwanda, Haruna Niyonzima aliyekwenda kwa mahasimu Simba, amesaini mkataba wa miaka miwili kutoka Mbabane Swallows ya Swaziland.
Yanga ilivutiwa na Tshishimbi baada ya kumuona akiichezea Swallows katika mchezo wa Kombe la Shirikisho la Soka Afrika mapema mwaka huu Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
Baada ya hapo ikamfuatilia kwenye mchezo wa marudiano Swaziland ambao aliingoza Mbabane Swallows kuichapa Azam 3-0 na kusonga mbele. Tangu hapo, Yanga imekuwa na mawasiliano na mchezaji huyo kwa lengo la kumsajili, ndoto ambazo zimetimia.    
Tshitshimbi anakuwa mchezaji wa sita wa kigeni wa Yanga kati ya saba wanaotakiwa kwa mujibu wa kanuni za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara baada ya kipa Mcameroon, Youthe Rostand, Wazimbabwe, kiungo Thabani Kamusoko na mshambuliaji Donald Ngoma na washambuliaji Mrundi Amissi Tambwe na Mzambia Obrey Chirwa.
Yanga inataka kuziba nafasi ya saba kwa kusajili beki wa kati kuziba pengo la Mtogo, Vincent Bossou aliyeondoka pia baada ya kumaliza mkataba kufuatia kuitumikia klabu huyo kwa misimu miwili. 

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATANZANIA WATAKAOVAA JEZI ZA MAMELODI AU AL AHLY

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

KOCHA BENCHIKHA AMESEPA

MASHUSHUSHU WA MAMELODI WALIKUJA KUTUPELELEZA: HERSI