4x4

MAXIMO AMPIGIA DEBE MWAKALEBELA URAIS TFF

MAXIMO AMPIGIA DEBE MWAKALEBELA URAIS TFF

KOCHA wa zamani wa Tanzania, Taifa Stars , Marcio Maximo
KOCHA wa zamani wa Tanzania, Taifa Stars Mbrazili, Marcio Maximo amemtaja rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) anayestaili kuchukua nafasi ya Jamal Malinzi kuwa ni Fredrick Mwakalebela. Kauli hiyo, aliitoa ikiwa ni siku moja kabla ya uchaguzi huo wa TFF ufanyike kesho Jumamosi mkoani Dodoma.

Maximo alionekana kutoa mapendekezo hayo kupitia video akimzungumzia Mwakalebela. Katika video hiyo, Maximo alisikika akisema: “Binafsi rais anayefaa kwa hivi sasa TFF ni Mwakalebela kutokana na utendaji wake kazi. “Nakumbuka Mwakalebela alikuwa katibu kipindi cha rais Tenga (Leodegar) ambaye ni rais bora kabisa aliyeweza kuliongoza vema shirikisho hilo.

“Hivyo, kutokana na ubora huo wa Tenga ninaamini Mwakalebela atakuwa anaiga utawala bora kupitia kwa Tenga aliyeweza kuliendesha shirikisho hilo kwa mafanikio, ninawashauri wapiga kura wamchague Mwakalebela,” alisikika Maximo aliyewahi kuifundisha Yanga. Alipotafutwa Mwakalebela kuzungumzia hilo alisema: “Mimi binafsi ninashukuru kwa sapoti kubwa aliyonipa Maximo katika kipindi hiki cha uchaguzi.

“Niseme kuwa Maximo nilizungumza naye hivi karibuni kabla ya kuamua kuchukua nafasi ya kugombea urais TFF, alinishauri nichukue fomu kutokana na kujua vema utendaji wangu. “Alinambia kuwa, atakuwa tayari kunipa ushauri katika masuala ya kiufundi kama nikifanikiwa kushinda nafasi hii ya urais,” alisema Mwakalebela.
Post a Comment