SAKATA LA LISSU, ZITTO NA STORI YA MCHAWI KUJISHTUKIA MSIBANI


Kwa tamaduni za Kitanzania, kiapo cha kukatazana kuzikana ni kikali, kikubwa na cha mwisho. Tafsiri yake ni kukunjiana nafsi mpaka kuingia kaburini. Ni kiapo kinachomaanisha muendelezo wa chuki hata baada ya kifo.
Pale mtu anapothubutu kutamka maneno ya kujenga ukuta na mwenzake hata wakati wa kuzikana, aliye pembeni hushituka na kuonya, "jamani msifike huko." Kiapo cha kutozikana ni chenye uthibitisho wa chuki na uadui uliopitiliza.
Kiapo cha kutozikana ni tamko la jumla na la mkato, kwamba "tusijuane kwa shida na raha." Hapo ndipo kwenye tatizo, maana inawezekana kutofautiana kwa mambo mbalimbali lakini uhusiano wa kijamii huendelea na matukio muhimu huwaleta watu pamoja.
Katika sayansi ya jadi na imani zake kwa maana ya uchawi na ushirikina kwa jumla, wachawi au waliotengeneza jambo lililochukua uhai wa marehemu, huwa wenye kujitoa zaidi msibani ili kuifanya jamii isiwahisi vibaya. Ushiriki wao mkamilifu hufunika dhana mbaya juu yao.
Ukifika msibani ukiwa unajitenga na kujiweka pembeni au usipofika kabisa. Kipindi mgonjwa akiugua maradhi ambayo wenye sayansi yao wanaita ni mkono wa mtu, halafu wewe ukawa mbali. Kwa mazingira ya pande hizo mbili lazima utatuhumiwa kuhusika.
Hivyo basi, katika mazingira ambayo inaonekana mtu amekufa katika mazingira asilia (natural death) bado watu hushikana uchawi, je inapotokea marehemu kifo chake kimetokana na shambulio la kimwili?
Utaona pia sababu ya watekelezaji wa mauaji kupitia magenge yao ya uhalifu au wauaji wa kukodi (assassins) na wakuu wao, ndani ya jamii zao huonesha pande zao nzuri za kibinadamu na kushiriki vema kijamii katika matukio ambayo wao wenyewe huyatenda.
Ushiriki wao mzuri kijamii huwaweka mbali na dhana mbaya dhidi yao. Tena anaweza kutokea mtu akamtuhumu mhusika lakini kwa namna mtuhumiwa alivyoonesha utu katika jambo husika, watu hukataa na kumgeuzia kibao aliyetoa tuhuma.
UTU NI TABIBU
Kuna jambo unaweza kulifanya likakuokoa na lawama ambayo ingekuhusu. Vilevile kuna maneno ukitamka au lipo tendo ukitenda, litakuingiza kwenye hatia wakati hujaweka mkono wako. Onesha utu kila wakati ili ukufae.
Nyakati hizi ambazo nchi inapita vipindi vyenye utata mkubwa, matukio ya watu kushambuliwa yanashika kasi. Anapoibuka mtu anayeshabikia au kukejeli shambulio alilofanyiwa mtu, huyo anakuwa hana anachokitafuta zaidi ya lawama au kutuhumiwa kuhusika.
Tafsiri ya pamoja kuhusu watu wenye kudhihaki majanga ambayo wanakutana nayo wenzao ni ukosefu wa utu. Na hapa ndipo Watanzania walipofikia katika kuonesha Utanzania wao. Mtu anapigwa risasi, wenye kujiita wapinzani wake wanakejeli.
Mtu anapatwa na janga la nyumba yake kuteketea kwa moto, wanaibuka watu kumsimanga na kudhihaki tukio hilo. Unajiuliza utu na Utanzania asili ulipo. Kejeli za vipindi vya matatizo zina tafsiri mbaya kuliko viapo vya kutozikana.
Kufikia hapo ndiyo kusema kuwa Watanzania kwa sababu za kisiasa, wamekuwa na uadui mkubwa kuliko wa wale wenye kuapizana kutozikana. Kwamba Taifa limefikia kwenye kiwango kikubwa kabisa cha ukosefu wa utu.
Hali sasa ni kuwa ukipatwa na matatizo, kabla ya kuguswa watu wanatazama kwanza wewe ni nani? Ukiwa ni chama tofauti na chake wanaanza kukejeli, ukiwa ni chama chao ndipo wataonesha utu, ikiwemo kukupa pole na kuangalia namna tofauti za kukufariji.
Nchi inagawanyika mno kwa sababu za kufanya siasa chafu. Tofauti za vyama na itikadi hazipaswi kuingiza ganzi ya utu kwenye mioyo ya watu. Upendo na ushirikiano wa kijamii, haupaswi kupunguzwa na tofauti za kisiasa kwa namna yoyote ile.
TUKIO LA LISSU
Septemba 7, mwaka huu, Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu, alipigwa risasi takriban 32, ikielezwa kuwa zaidi ya risasi tano ziliingia mwilini mwake na kumjeruhi vibaya. Ni tukio ambalo bila kupepesa macho kusudio lake lilikuwa roho ya Lissu.
Lissu alifanyiwa shambulio hilo mchana, nyumbani kwake akiwa anajiandaa kushuka kwenye gari. Lissu alikuwa anatoka bungeni baada ya kumalizika kwa kikao cha saa 3:00 asubuhi mpaka saa 7:00 mchana.
Kwa sasa Lissu anaendelea na matibabu hospitalini Nairobi, Kenya. Hali yake inaelezwa siyo ya kuridhisha ingawa anaendelea kupata nafuu taratibu. Ni kipindi ambacho Watanzania wanatakiwa kuungana kumuombea ili apone na kurejea nchini.
Maombi kwa Lissu ni kutokana na ukweli kuwa waliomshambulia walikuwa na makusudi ya kutekeleza rekodi mbaya sana kwa nchi. Hata sasa nchi imechafuka lakini ingekuwa mbaya sana kama wangefanikiwa. Tanzania ingehesabika kuwa Taifa ambalo wanasiasa wa upinzani hawapo salama.
Kwa mtu ambaye yupo chama tofauti na kile cha Lissu anaweza kudhani walengwa ni wapinzani. Hata hivyo, inatakiwa kukumbushana kwamba wahusika halisi wa shambulio la Lissu hawajulikani na malengo yao hayafahamiki.
Hivyo, haitakiwi kufurahia au kuchukulia mchezomchezo tukio la Lissu. Badala yake inatakiwa kuwaza kwa kina huku kila mmoja akijiuliza maswali mengi. Si kujiuliza na kupata majibu, la! Kujiuliza kwa shabaha ya kupanua ubongo kuhusu jambo husika.
Mwana CCM mwenye kukipenda chama chake, anatakiwa kuchukizwa sana na tukio la Lissu kwa sababu chama chake ndicho chenye kutawala nchi, kwa hiyo mtu yeyote mwenye kutekeleza tukio lenye kuhatarisha amani ya nchi huyo haitakii mema CCM.
CCM ndicho chama ambacho kiliomba na kupewa dhamana ya kuilinda nchi katika mipaka yake na usalama wa raia mmoja mmoja. Sasa kitendo cha watu kutekwa na kushambuliwa kwa risasi mchana kweupe ni kutaka kuonesha CCM imeshindwa kazi.
Inapotokea sasa mtu ambaye ameshambuliwa au kutekwa ni kiongozi, hapo inakuwa dhahiri watu wanataka kuitia doa Serikali, kwamba kama viongozi tu hawalindwi, je wananchi wa kawaida? Utaona kuwa CCM wanapaswa kuwa wakali hasa.
Wanapoibuka wana CCM na kusema tukio la Lissu si la mara ya kwanza, maana yake wanataka kutengeneza tafsiri mbili. Moja ni mbaya sana kwa jamii, nyingine ni kukichafua chama chao. Mshangao ni kuwa mamlaka za juu za chama hazijaamka kukemea.
Tafsiri ya kijamii ni kuwa wanataka Watanzania waone tukio la Lissu ni kawaida. Na hapo ndipo kwenye kosa kubwa mno. Watanzania hawajazoea kuona mashambulizi ya kuwindwa watolewe roho. Iweje sasa waambiwe maneno kuwa Lissu si wa kwanza?
Ni tafsiri mbaya kwa sababu inatengenezwa taswira kuwa siku nyingine likitokea jambo lingine watu waseme ni kawaida, kwamba watu wameshazoea matukio ya raia kushambuliwa na kuuawa. Bila shaka anayesema tukio la Lissu si la kwanza, halijamtokea yeye.
Tafsiri ya pili ni mbaya kwa chama chao. Kwamba CCM ambacho kina dhamana ya dola, kinaona kawaida watu kushambuliwa kwa risasi kama ilivyotokea kwa Lissu. Kwamba chama kinashindwa kuongoza dola vizuri ili wananchi wawe salama.
Mbaya zaidi ni kejeli. Mtu kashambuliwa, ana maumivu makali. Nchi ipo kwenye hofu. Unaobuka na kutoa orodha ya watu walioshambuliwa kwa risasi na kuuawa, halafu unasema la Lissu si la kwanza. Ni ukosefu wa utu.
Ni hapo wanaturejesha kwenye stori ya mchawi msibani. Anajitenga na anajishtukia. Akiulizwa kwa nini unajitenga? Anajibu: "Wasije kusema nimemuua marehemu."
Hadithi za kubishana aliyelipia ndege ya kumpeleka Lissu Nairobi hazikuwa na sababu yoyote. Hata hivyo, zikafanywa kuwa sehemu ya mjadala wakati kilichotakiwa zaidi ni kujielekeza kuhakikisha Lissu anapata huduma bora na anapona.
TUKIO LA ZITTO
Septemba 16, mwaka huu, Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe, alipata ajali ya nyumba yake kuteketea kwa moto. Baada ya tukio hilo, watu wakaibuka na kukejeli kuwa ni matokeo ya kisomo cha albadili na wengine walisema Zitto alichoma nyumba yake mwenyewe.
Kweli kabisa, mtu anakaa na kufikiria kuwa Zitto anaweza kuchoma moto nyumba yake na kuiteketeza kabisa kwa lengo la kujitafutia umaarufu wa kisiasa? Mbona watu wamefika mahali pabaya kiasi hicho?
Utu hakuna kabisa. Muda ambao inatakiwa watu watafakari kuhusu matukio mfulilizo yanayoikumba nchi kwa sasa. Mara mashambulizi ya risasi, wengine wanatekwa na sasa nyumba ya mbunge inaungua moto, lakini watu wanakejeli.
Watanzania wenye kuendekeza mizaha kwenye mambo mazito kwa nchi. Wanaotumikia chuki katika matukio ambayo yanapaswa kuwaunganisha, hiyo ni alama kwamba nchi yao inaweza kuharibika wakati wao wakiwa wanang'ang'ana na misimamo ya hovyo.
Kama huwezi kumhurumia mtu kwa hasara aliyopata baada ya nyumba yake kuteketea kwa moto, unataka lini uoneshe huruma kwake? Hujui hasara kiasi gani amepata wewe unamdhihaki. Hicho ni kipimo tosha kuwa ubinadamu umetoweka.
TUFIKE TAMATI
Nyakati za matatizo ni zenye kuleta watu pamoja na kudumisha uhusiano mwema. Haitakiwi matatizo yaongeze ufa wa kijamii, badala yake matatizo ya upande mmoja hupunguza mifarakano na kukaribisha hali ya kuhurumiana.
Katika uhusiano wa kijamii, adui anaposherehekea kifo au janga la hasimu wake, moja kwa moja hukaribisha hali ya kutafsiriwa kuwa yeye ni mhusika. Anapoibua visa kipindi hasimu wake yupo matatizoni hukaribisha mashaka zaidi.
Inapotokea adui yupo kwenye majanga kisha hasimu wake akawa mstari wa mbele kutoa ushirikiano, huonesha mfano mwema kwamba pamoja na tofauti zote, lakini unapohitajika ushirikiano wa kijamii huwa mstari wa mbele.
Lissu anaumwa, kipindi hiki Serikali na CCM kwa jumla, wanayo nafasi ya kuonesha utu wema kwa kujitoa hasa kuhakikisha anapewa huduma bora na ulinzi madhubuti. Waoneshe kweli kuwa nao wanaumizwa na yaliyomkuta Lissu.
Kitendo cha Serikali kufanya visa mara haitahusika na matibabu ya Lissu nje ya mfumo wa kupitia Hospitali ya Taifa, Muhimbili, mara inaweka masharti yasiyo ya lazima kuweza kumtibu Lissu, kinakaribisha dhana mbaya. Ile dhana ya msibani ambayo nimeshaieleza.
Mara watu wenye kuvaa fulana za kumuombea Lissu wanakamatwa na polisi. Watu wanaokusanyika kumuombea Lissu wanakamatwa. Wenye kwenda hospitali kuchangia damu kuonesha kuguswa kwao na tukio la Lissu nao wanakamatwa. Hiyo yote ni kukaribisha dhana mbaya. Ile dhana ya msibani.
Watu wakimuombea Lissu inawauma nini? Fulana za kumuombea Lissu zinawaumiza kwa lipi? Ni mambo ambayo yanapofanyika yanakaribisha dhana mbaya. Ile dhana ya msibani ambayo nimeshaieleza.
Wiki mbili Lissu yupo hospitali Nairobi lakini hakuna kiongozi wa Serikali wala Bunge aliyemtembelea kuonesha ushirikiano. Kujitenga huko kunakaribisha ile dhana mbaya. Ile dhana ya msibani ambayo nimeshaieleza.
Mara Jaji Mkuu, Profesa Ibrahim Hamisi Juma, anaibuka na kuelezea masuala ya upelelezi wa Lissu, kwamba yatafanywa na vyombo vya ndani. Unajiuliza Jaji Mkuu alipatwa na nini mpaka aanze kuzungumzia mambo yasiyomhusu?
Upelelezi ni kazi ya Serikali. Jaji Mkuu ni kiongozi wa Mahakama. Anatakiwa kusubiri mashitaka mahakamani ndipo mhimili anaouongoza utafsiri sheria kwa jinsi ushahidi utakavyowasilishwa na kutoa uamuzi. Jaji Mkuu kuzungumzia upelelezi na kutoa hitimisho wakati haumhusu, inakaribisha dhana mbaya.
Hakuna siku ambayo nilijisikia vibaya kama nilipomuona Jaji Mkuu mstaafu, Chande Othman, alipokwenda kumtembelea Lissu hospitalini Nairobi. Ni kweli Lissu ni ofisa wa mahakama, lakini Lissu aliumia katika mazingira ya Bunge. Spika au naibu wake imeshindikana kabisa kwenda Nairobi?
Lissu ni Rais wa Jamii ya Wanasheria Tanganyika (TLS), hivyo yeye ni kiongozi wa mawakili (maofisa wa mahakama), Jaji Mkuu wa sasa, anafahamu kuwa kiongozi wa maofisa wa mahakama yake tukufu ana hali mbaya. Hata kwenda japo siku moja na kugeuza?
Nakumbusha kuwa kujitenga kwenye msiba au janga la mwenzako ni kukaribisha dhana mbaya. Ile dhana ya msibani ambayo nimeshaieleza.
Ndimi Luqman MALOTO
LikeShow more reactions
Comment

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

HATUTOPAKI BASI DHIDI YA YANGA-MOKWENA

“PEMBA SALUTI KWENU” DK. NCHIMBI*

DKT NCHIMBI AWAAHIDI MAKUBWA WANANCHI WA KWELA, RUKWA