WATANZANIA WANAMUOMBEA LISSU, WAUAJI WANAKWIDANA 'KWA NINI HAWAKUMUUA!'


Ichukue kama tamthiliya ila nakuhakikishia kuwa hautakuwa mbali na ukweli.
Amini kuwa kipindi hiki Watanzania wakiwa na mshikamano mkubwa wa maombi, wakimpigia magoti na kumsujudia Maulana amponye Tundu Lissu kwa asilimia 100, wauaji waliokuwa kwenye Nissan nyeupe wana wakati mgumu sana.
Walipewa kazi ya kumuua Lissu, wakapewa fedha na rasilimali nyingine zenye kuwezesha mpango wao wa kumtoa roho, mwisho wameishia kumjeruhi tu.
Kwa kifupi ni kuwa 'misheni' ya kumuua Lissu imefeli. Hakuna taarifa mbaya kwa wazee wa Nissan nyeupe kama habari zinazotoka hospitalini Nairobi, zikieleza: "Lissu anaendelea kupona. Anazungumza akitia faraja na matumaini."
Wazee wa Nissan nyeupe hawana kauli kwa aliyewatuma wamuue Lissu, maana anawahoji: "Nimewapa kila kitu ili mtimize lengo la kumuua Lissu lakini mmeshindwa. Lissu ni mzima na anaendelea kupumua."
Watekeleza mauaji nao mbele ya "Bwana wao" aliyewatuma wamuue Lissu, hawana kauli zaidi ya kushangaa na kuulizana: "Sijui kaponaje?"
Walipo wanakaa na kuelekeza maombi yao kwa Lucifer ili Lissu afe akiwa hospitali. Wanashindwa kufahamu kuwa Lucifer ni Shetani tu, hana mamlaka mbele ya Mungu.
Shetani anaweza kuwavuruga binadamu wapumbavu kiasi cha kuwafanya washindwe kumtii Mwenyezi Mungu. Hata hivyo, Shetani hana ujanja mbele ya kinga na kudura za Mwenyezi Mungu.
Wazee wa Nissan nyeupe walifanikiwa kumshambulia Lissu na kumtoboa mwili wake kwa risasi zaidi ya tano, maana hilo ni tendo ndani ya uwezo wao na kwa kibali cha Shetani waliyeamua kutii upotoshaji na uovu wake.
Hata hivyo, walimuamini sana Shetani kiasi cha kusahau kuwa kibali cha mwisho cha kutenganisha nafsi na mwili kipo kwa mmoja tu, Mfalme wa Mbingu na Ardhi. Mfalme wa Nchi na vilivyomo. Mungu Mwenyezi.
Hivyo, wataendelea kuulizana na kushangaana kwa namna Lissu alivyopona. Ila siku akili ikiwakaa sawa na kutambua mwenye mamlaka juu ya roho ya Lissu ni Mungu, wataheshimu, watapiga goti na kuungama.
Kwani wao ni nani? Hata Firauni (Pharaoh), aliposhindwa kila mpango wa kumuua Musa, aliitazama mbingu kwa jicho la unyenyekevu, akakiri kuwa Mungu aliyenadiwa na Musa ndiye Mungu wa kweli.
Kwa uchawi karoge, kwa bunduki yako piga, kwa panga lako charanga, kwa kisu chako choma, mwisho kabisa elewa kwamba kila silaha yenye kuonekana inatosha kutoa uhai wa mtu, hiyo ni sababu tu ya kifo. Hata hivyo, kibali cha nafsi kutoka kwenye mwili wa binadamu kipo kwa Mungu tu!
Muhimu; Kwa idadi ya risasi ambazo zilitoka kwenye bunduki kumlenga Lissu. Kwa idadi ya risasi zilizompata Lissu kisha kupenya ndani ya mwili wake. Na matokeo ya Lissu kubaki hai. Huo ni ujumbe kwamba Mungu hataki Lissu afe. Bado analo jukumu alilompa na hajalikamilisha.
TUANDIKE TAMTHILIYA
Lissu alishambuliwa kwa risasi mchana kweupe, nyumbani kwake, akiwa ametoka bungeni katika kikao cha saa 3:00 asubuhi mpaka saa 7:00 mchana.
Ukiliwaza vizuri tukio hilo, ndipo unaweza kubaini kuwa ilikuwa tamthiliya ya muda mrefu ambayo maudhui yake yalikuwa hayafiki mwisho, hivyo wahusika waliamua liwalo na liwe.
Utanielewa tu; kitendo cha wauaji kumshambulia Lissu nyumbani kwake, mchana kweupe, tena kwenye eneo ambalo liliaminika ni kati ya maeneo salama zaidi mkoani Dodoma, tafsri yake ni stress na panic.
Ndiyo, wale jamaa ni wazi walikuwa wameshamsaka Lissu kwa muda mrefu ili wafanikishe lengo lao lakini wakawa wameshindwa. Hali hiyo bila shaka iliwafanya wapanic na wajae stress, kwa hiyo wakaamua kumshambulia kweupe.
Pengine walishajaribu kumteka Lissu kama alivyotekwa Roma Mkatoliki na wenzake au kama ilivyotokea kwa Ben Saanane. Pengine kila njia waliyoona ni bora zaidi ilishindikana kwa Lissu ndiyo maana waliamua kumshambulia eneo la wazi.
Maelezo ya Lissu kabla hajashambuliwa kwamba alikuwa akifuatiliwa kwa muda mrefu na watu husika, jumlisha kile alichokisema dereva wake, kwa pamoja ni ujazo wa nyama kwenye nadharia kwamba walishamjaribu mara nyingi na katika maeneo tofauti bila mafanikio.
Kwa mazingira hayo ya kutumia muda mrefu bila kufanikisha lengo, wanakutana na presha kali kutoka kwa bosi wao ambaye anawaambia wameshindwa kazi. Nao wakitazama mazingira wanaona ugumu, hivyo wanaamua kumshambulia kweupe, katika eneo lenye ulinzi.
Unapata picha kuwa inawezekana walishajaribu hata kumtegea mwanamke lakini ikashindikana. Walishamvuta kwa hadaa ya pesa ikashindikana. Hivyo wakaamua kujilipua kwa kufanya shambulio hilo ambalo linashangaza kwa namna wahusika walivyokosa hofu.
Mimi nasema kuwa presha huondoa hofu. Unacheza na presha ya kuonekana umeshindwa kazi? Ulishaahidi kuwa kazi ya kumshughulikia Lissu ni ndogo na rahisi, lakini inapita miezi hujafanikiwa. Mwenye kazi anaomba arejeshewe pesa zake, lazima utajilipua tu.
ONA PRESHA BAADA YA TUKIO
Baada ya shambulio, wale jamaa walipokimbia walijua wameshamaliza kazi. Inawezekana kabisa wakiwa njiani wakikimbia baada ya kummiminia risasi nyingi Lissu, walikuwa wakijipongeza kuwa hatimaye walikuwa wamefanikiwa kumuua Lissu.
Waliposikia Lissu anapumua na amepelekwa Hospitali ya Mkoa, Dodoma, pengine walicheka kwa kebehi, wakiamini kuwa isingewezekana kwa Lissu kupona. Walidhani ni kupoteza muda, Lissu angekufa tu.
Inawezekana pia habari za kumpeleka Lissu Nairobi ziliwachekesha sana. Walikaa mkao wa kusubiri tangazo la kifo. Inawezekana pia kuna wakati waliamini Lissu ni marehemu, isipokuwa Chadema waliamua tu kusema uongo kuuhadaa umma wa Watanzania.
Kipindi hiki baada ya Zitto Kabwe, Lazaro Nyalandu, Jaji Mkuu mstaafu, Chande Othman wanapopigwa picha kuwa nao walikwenda kumuona Lissu na kueleza anaendelea kupona, inakuwa habari mbaya sana kwa wauaji wa Nissan nyeupe.
Wanashangaa Lissu kapona vipi? Bosi wao anakuwa mkali kwa sababu alitoa pesa ili Lissu auawe, siyo ajeruhiwe.
Ndiyo maana kipindi hiki Lissu akiendelea na matibabu, Watanzania wakimuombea kwa bidii kubwa ili apone na kurejea nchini salama na kuendelea na majukumu yake kama alivyozoeleka, upande wa pili ni kivumbi na jasho.
Kibano ni kwa nini wameshindwa kumuua Lissu? Nao jawabu lao ni: "Tulimuua kabisa, tunashangaa amepona vipi?"
Ni hapo sasa utaelewa kile alichosema Mkurugenzi wa Vipindi na Uzalishaji wa Clouds Media Group, Ruge Mutahaba kuwa teknolojia na Mungu ni wa kuogopwa sana.
Ndimi Luqman MALOTO

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

DKT NCHIMBI AWAAHIDI MAKUBWA WANANCHI WA KWELA, RUKWA

DKT NCHIMBI ASHIRIKI MAZISHI YA ASKOFU.GACHUMA WA KANISA LA NLGCC

π™‚π˜Όπ™ˆπ™Šπ™‰π˜Ώπ™„ π™†π˜Όπ˜Ύπ™ƒπ™€π™•π˜Ό π™†π™„π˜½π™„π™‰π™‚π™’π˜Ό.