Bobali aomba fedha za barabara ziongezwe Lindi

Hamidu Bobali 

NA MWANDISHI WETU
MBUNGE wa Jimbo la Mchinga, mkoani Lindi, Hamidu Bobali (CUF), ameiomba Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kuongeza fedha za ujenzi wa barabara katika mkoa huo kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2017/18.
Bobali aliyasema hayo jana wakati akichangia kwenye mjadala wa bajati ya wizara hiyo iliyowasilishwa Aprili 23 na Waziri Profesa Makame Mbarawa bungeni Dodoma.
Alisema wizara hiyo imetengewa takribani theluthi moja ya bajeti yote ya nchi huku Mkoa wa Lindi ukitengewa Sh. Mil  800 kwa ajili ya utengenezaji na ukarabati wa kilomita kilomita 629 fedha ambazo ni kidogo.
Mbunge huyo alisema asilimia kubwa ya miundombinu ya barabara katika mkoa huo zimeharibika katika kipindi kifupi hali ambayo inaonesha kuwa ubora haukuzingatiwa wakati wa ujenzi na kwamba fedha zilizotengwa hazitoshi.
“Mkoa una barabara zenye urefu wa zaidi ya kilomita 629 umetengewa Sh. Mil 800 lakini mikoa yenye barabara zenye kilomita 400 zimetengewa fedha nyingi hii sio sawa naomba waziri aliangalie,” alisema.
Alisema kwa sasa mkoa huo umepata fursa nyingi za kiuchumi kama kilimo cha korosho, ufuta na mazao  hivyo upo umuhimu wa uwepo barabara zenye ubora zinazoweza kupitika mwaka mzima.
Bobali alisema kutokana na mvua ambazo zimenyesha kwa hivi karibuni barabara ya Lindi hadi Dar es Salaam imejaa mashimo ambayo yanasababisha ajali na uharibu wa magari ya mizigo.
Aidha, mbunge huyo aliomba serikali kupandisha hadhi barabara ya Chikonji, Nangalu hadi Milola yenye urefu zaidi ya kilomita 100 kutoka halmashauri, ili iweze kuhudumiwa na Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads).
Halikadhalika Bobali ameomba Serikali kuhakikisha kuwa mfumo mawasiliano kwa wote unatekelezwa katika vijiji vyote jimboni hapo.
“Katika bajeti nimepata vijiji viwili na vijiji zaidi ya 15 vikibakia naomba hili lifanyiwe kazi,” alisema.
Alitaja baadhi ya vijiji ambavyo havina mawasiliano ni Mputwa, Kiwawa, Namkongo, Mvuleni, Ruvu, Namwangala, Kijiweni na vingine.
Aidha, Bobali ameitaka wizara hiyo kuhakikisha kuwa viwanja vya ndege nchini vinawekewa taa ili vifanye kazi saa 24 tofauti na ilivyo sasa ambapo vinafanya kazi saa 12.
Alisema hakuna faida ambayo itapatikana kama ndege zinazonunuliwa kwa gharama kubwa na kufanya kazi mchana pekee kama vile hakuna amani.
Bobali alisema ni vema jitihada zikaongezwa katika kuboresha miundombinu mbalimbali ambayo inakamilisha mchakato wa usafiri wa anga.
Mwisho

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

HATUTOPAKI BASI DHIDI YA YANGA-MOKWENA

“PEMBA SALUTI KWENU” DK. NCHIMBI*