MTIBWA SUGAR YAISHIKISHA ADABU SINGIDA UNITED , YAICHAPA 3 - 0 NAMFUA


Na Mwandishi Wetu, SINGIDA
TIMU ya Mtibwa Sugar imeichapa Singida United kwa mabao 3-0 katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara jioni ya leo Uwanja wa Namfua mjini Singida.
Ushindi huo unaifanya Mtibwa Sugar ifikishe pointi 30 baada ya kucheza mechi 21 na kuendelea kukamata nafasi ya sita, nyuma ya Singida United yenye pointi 36 kufuatia kucheza mechi 33.
Mabao ya Mtibwa Sugar inayofundishwa na mchezaji wake wa zamani, Zuberi Katwila yamefungwa na Kelvin Sabato, Salum Kihimbwa na Hassan Dilunga.
Sabato alifunga bao la kwanza dakika ya 21 kwa shuti la mpira wa adhabu lililotinga nyavuni moja kwa moja, kabla ya Khimbwa kufunga la pili dakika ya 53 akimalizia pasi nzuri ya Dilunga, ambaye naye alifunga bao la tatu dakika ya 71 kwa penalti.
Penalti hiyo ilitolewa baada ya beki Roland Msonjo wa Singida United ya kocha Mholanzi, Hans van der Pluijm, kumchezea rafu kiungo Salum Kihimbwa kwenye eneo la hatari.
Katika mechi nyingine ya Ligi Kuu leo, Mbao FC imelazimishwa sare ya 0-0 na Lipuli FC ya Iringa Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza.
Kwa sare hiyo, Mbao FC inabaki kwenye eneo la hatari ya kushuka daraja, ikifikisha pointi 20 baada ya kucheza mechi 23 na kuendelea kukamata nafasi ya 14 katika ligi ya timu 16, mbele ya Njombe Mji FC yenye pointi 18 za mechi 22 na Maji Maji FC pointi 16 za mechi 22.
Lipuli FC yenyewe inayofundishwa na wachezaji wake wa zamani wa Simba SC, Suleiman Matola na Amri Said inafikisha pointi 28 baada ya kucheza mechi 23 na kuendelea kukamata nafasi ya saba, ikiwa juu ya Mbeya City na Ruvu Shooting ya Pwani zenye pointi 25 kila moja baada ya kucheza mechi 22 pia. 

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATANZANIA WATAKAOVAA JEZI ZA MAMELODI AU AL AHLY

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

KOCHA BENCHIKHA AMESEPA

MASHUSHUSHU WA MAMELODI WALIKUJA KUTUPELELEZA: HERSI