SERIKALI YAPATA MKOPO WA SHILINGI BILIONI 34 KUTOKA MFUKO WA MAENDELEO YA KIUCHUMI WA KUWAIT


Na Benny Mwaipaja, WFM, Dodoma


Serikali ya Kuwait kupitia Mfuko wa Maendeleo wa Kiuchumi wa Kuwait (Kuwait for Arab Economic Development Fund), na Serikali ya Tanzania zimetiliana saini  rasimu ya mkataba wa  kuipatia Tanzania mkopo wenye masharti nafuu wa dola milioni 15.3, sawa na zaidi ya shilingi bilioni 34, kwa ajili ya mradi wa  kilimo cha umwagiliaji katika Bonde la Luiche, mkoani Kigoma,  lenye ukubwa wa  hekta 3,000.

Rasimu hiyo ya Mkataba imesainiwa na Kiongozi wa ujumbe wa wataalamu na Mshauri wa Masuala ya Kilimo wa Mfuko wa Maendeleo ya Kiuchumi wa Kuwait,  Dkt. Abdulrida Bahman na  kwa upande wa Tanzania ikisainiwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Khatibu Kazungu, mjini Dodoma.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb)  amesema hatua hiyo imfikiwa baada ya timu ya wataalamu kutoka Kuwait kutembelea eneo la mradi mkoani Kigoma na kuridhishwa na umuhimu wake kiuchumi kwa wananchi wa mkoa huo na taifa kwa ujumla.
 “Mradi huo una umuhimu mkubwa kwa watanzania kwa kuwa wataweza kuwa na kilimo cha umwagiliaji cha Mpunga na Mbogamboga kwa mwaka mzima badala ya kilimo cha msimu cha kutegemea mvua, na katika siku zijazo Kigoma itakua miongoni mwa mikoa inayozalisha mchele kwa wingi”, alisema Dkt. Mpango.
Dkt. Mpango amesema kuwa Serikali ya Tanzania na Kuwait zitatia saini mkataba rasmi wa mkopo huo wenye masharti nafuu ifikapo mwishoni mwa mwezi Juni mwaka huu ili mradi huo uanze kutekelezwa ili kuongeza kipato cha wananchi na  kuwa na uhakika wa chakula.
Amesema Nchi ya Kuwait imekuwa ikiisaidia Tanzania katika kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo ya ukarabati wa Hospitali ya Mnazi mmoja, Zanzibar kwa kiasi cha dola za Marekani milioni 13.6 sawa na shilingi bilioni 31.
"Kwa upande wa Tanzania Bara wametoa mkopo nafuu wa shiingi bilioni 115 kwa ajili ya kuboresha barabara ya Chaya hadi Nyahua (km 85) kwa kiwango cha lami ambayo ni muhimu kwa kuwa inaunganisha mikoa ya Magharibi mwa Tanzania" aliongeza Dkt. Mpango
Miradi mingine ambayo  nchi hiyo imeonesha nia ya kuisaidia nchi, ni pamoja na ujenzi wa jengo la abiria katika Uwanja wa Ndege wa Mwanza, uboreshaji wa barabara ya kutoka Morogoro hadi Dodoma na ujenzi wa barabara za mzunguko za kuingia na kutoka mjini Dodoma ambazo zitasaidia kuondoa msongamano wa magari yanayopita katikati ya mji huo kutokana na kuongezeka kwa idadi ya watu na vyombo vya moto baada ya Makao Makuu ya Serikali kuhamia Dodoma.
Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Mpango ameishukuru nchi ya Kuwait kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Kiuchumi wa Kuwait, kwa nia yake njema na thabiti katika kusaidia nchi ya Tanzania kutekeleza kwa mafanikio miradi ya Maendeleo ya kiuchumi katika nia yake ya kupata maendeleo Stahiki.
Kwa upande wake Kiongozi wa ujumbe wa wataalamu na Mshauri wa Masuala ya Kilimo wa Mfuko wa Maendeleo ya Kiuchumi wa Kuwait, Dkt. Abdulrida Bahman, ameishukuru Serikali ya Tanzania kupitia Waziri wa Fedha na Mipango kwa ukarimu pamoja na Idara ya Taifa ya Umwagiliaji kwa ushirikiano mzuri katika hatua za kufanikisha utekelezaji wa mradi wa umwagiliaji  wa Bonde la Luiche, Mkoani Kigoma.
“Tumetembelea eneo la mradi kwa takribani wiki mbili tumejionea uzuri wa nchi hii na fursa zilizopo, hii ni nchi tajiri na inaweza kuwa tajiri kuliko Kuwait kwa kuwa kila kitu kinachoweza kufanya nchi hii iwe tajiri kipo”.Alieleza Dkt. Bahman.
Amesema mradi huo wa umwagiliaji hautakuwa wa mwisho kupewa fedha na mfuko huo bali utaendelea kusaidia kutekeleza miradi mingine mingi kama ilivyokuwa ikifanya, kutokana na ushirikiano mzuri, wa kihistoria, na wa muda mrefu kati ya nchi hizo mbili.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango (SERA), Dkt. Khatibu Kazungu (kushoto) na Kiongozi wa ujumbe wa wataalamu na Mshauri wa Masuala ya Kilimo wa Mfuko wa Maendeleo ya Kiuchumi wa Kuwait (Kuwait for Arab Economic Development Fund), Dkt. Abdulrida Bahman, wakibadilishana rasimu ya mkataba wa mkopo wa dola milioni 15.3 za Marekani, kwa ajili wa kujenga mradi wa kilimo cha umwagiliaji maji katika Bonde la Luiche, mkoani Kigoma,

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

HATUTOPAKI BASI DHIDI YA YANGA-MOKWENA

“PEMBA SALUTI KWENU” DK. NCHIMBI*