Halmashauri
ya Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam imeahidi kuendeleza na
kudumisha miradi iliyoachwa na shirika la Plan International katika
maeneo ya Buguruni na Vingunguti.
Ahadi
hiyo imetolewa leo jijini humo na Katibu Tawala wa Halmashauri hiyo,
Edward Mpogolo alipokuwa akifunga programu ijulikanayo kama Dar – Urban
iliyoanzishwa na shirika hilo ambayo imedumu katika maeneo hayo kwa
miaka 26.
Mpogolo
amesema kuwa shirika hilo limefanya kazi nzuri tangu kuanzishwa kwa
program hiyo kwani imeleta mapinduzi makubwa katika kuimarisha huduma
muhimu kwa wananchi kwa kuboresha sekta mbalimbali zikiwemo za elimu,
afya na ujenzi wa miundo mbinu.
“Toka
mwaka 1992 wamekuwa na sisi wakitusaidia kutuboreshea huduma mbalimbali
na katika kipindi chote hicho wameweza kutujengea shule mbili za msingi,
kutujengea kituo cha Afya cha Buguruni, kuwaelimisha na kuwainua vijana
hivyo tunawaahidi kuisimamia na kuidumisha miradi yote waliotuachia”,
alisema Mpogolo.
Mpogolo
amefafanua kuwa baada ya shirika hilo kujenga shule mbili za msingi za
Vingunguti na Buguruni Moto Mpya mnamo mwaka 2016 ufaulu uliongezeka
kutoka asilimia 49 mpaka asilimia 98 pia tangu walipojenga kituo cha
afya mnamo mwaka 2002 wagonjwa walikuwa 40 mpaka 50 kwa siku lakini kwa
sasa kituo kinapokea wagonjwa kati ya 500 mpaka 600.
Vile
vile katika kuelimisha vijana, Mpogolo amesema kuwa shirika hilo
linajitahidi kuendana na Sera ya Serikali nchini ya kuwasaidia vijana
ambapo wameweza kuelimisha vijana zaidi ya 2,000 na vijana hao
wametumika kuwaelimisha wenzao zaidi ya 29,000 walioweza kujianzishia
shughuli zao binafsi kwa ajili ya kujikimu.
Aidha,
Mpogolo ametoa rai kwa shirika hilo kuendelea kushirikiana na Serikali
katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma muhimu ambazo zitasaidia
kupunguza utegemezi kati yao na kuwafanya waweze kuchangia katika kukuza
uchumi wa nchi.
Kwa
upande wake Meneja Miradi ya Dar – Urban kutoka shirika la Plan
International, Nicodemus Gachu amesema kuwa progamu hiyo inafungwa baada
ya kuhitimisha utekelezaji wa miradi mbalimbali hivyo watahamia katika
maeneo mengine yenye uhitaji.
“Kwa
miaka 26 mradi huu umetumia zaidi ya bilioni 15 katika kutekeleza miradi
mbalimbali ya afya, elimu, ulinzi wa mtoto, ushirikishwaji, elimu ya
afya ya uzazi na uwezeshaji vijana kiuchumi”, alisema Gachu.
Mradi
huo utahamishiwa katika wilaya ya Nkasi iliyopo mkoani Rukwa kwa lengo
kubwa la kumuwezesha mtoto wa kike kupata fursa mbalimbali katika jamii
pamoja na kusaidia maeneo yenye uhitaji katika wilaya hiyo.
Comments