SERIKALI YAHIMIZA HALMASHAURI KUBUNI MIRADI YA KIMKAKATI ILI KUJIONGEZEA MAPATO


Serikali imeeleza kuwa Uchukuaji wa baadhi ya vyanzo vya mapato katika halmashauri ulifanyika kwa mujibu wa Sheria ya Bajeti iliyoridhiwa na Bunge ya mwaka 2015 kifungu namba 58 ikiwa na lengo la kuongeza ufanisi wa ukusanyaji na matumizi ya mapato hayo.

Hayo yameelezwa Bungeni Jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) alipokuwa akijibu swali la Msingi la Mbunge wa Viti Maalum Mhe. Suzana Mgonukulima, aliyependekeza itungwe sheria ya kuibana serikali ikiwa haitarejesha fedha zilizotokana na vyanzo vya mapato vilivyopo kwenye Miji, Halmashauri, Manispaa na Majiji zitakazokusanywa na kuwekwa kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali.

Akijibu swali hilo Dkt. Kijaji alisema kuwa kwa mujibu wa kifungu cha 44 cha Sheria ya Bajeti, mgao wa fedha kutoka katika Mfuko Mkuu wa Serikali utazingatia bajeti iliyoidhinishwa, upatikanaji na mtiririko wa fedha, utekelezaji mpango wa ununuzi na mpango wa kuajiri hivyo hakuna Fungu litakaloruhusiwa kufanya matumizi ya aina yoyote mpaka kuwe na fedha za kulipa matumizi husika.

“Usimamizi wa Mapato hayo kwa mujibu ya Sheria ya Bajeti ya Mwaka 2015 Kifungu namba 58 unazingatia mapato kuingizwa kwenye Sheria ya Kuidhinisha Matumizi ya Fedha za Serikali, aliyepewa mamlaka ya kukusanya mapato ya Serikali atawajibika katika ukusanyaji wenye ufanisi, utunzaji wa hesabu, utoaji wa taarifa na kuzuia ufujaji wa mapato”, alisema Dkt. Kijaji. 

Alisema Usimamizi wa mapato na matumizi umebainishwa vizuri na hivyo hakuna haja ya kutunga sheria nyingine ya kuibana Serikali ikiwa haitapeleka fedha kwenye, Miji, Halmashauri, Manispaa na Majiji.

Aidha akijibu swali la nyongezai la Mhe. Mgonukulima kuhusu kutokuwa na usawa katika utoaji wa fedha za maendeleo katika Wilaya, Dkt. Kijaji alisema kuwa tarehe 5 Mei, 2018 Serikali ilizindua Mkakati wa kuziwezesha Mamlaka za Serikali za Mitaa kutekeleza miradi yenye kuchochea upatikanaji wa Mapato ili ziweze kujitegemea hivyo ni vema Halmashauri zikabuni miradi ya maendeleo itakayoongeza mapato.

Akieleza kuhusu utaratibu wa malipo ya Kodi ya Majengo kutoka katika Halmashauri nchini Naibu Waziri Dkt. Kijaji, alisema kuwa Majengo yasiyofanyiwa tathimini yanatakiwa kutozwa kiwango sawa cha Sh. 10,000 na majengo ya juu (ghorofa) yanatakiwa kutozwa kiwango sawa cha Sh. 50,000.

Alisema majengo yaliyofanyiwa tahimini ndiyo yanayoweza kulipiwa kodi zaidi ya kiasi hicho, hivyo wakurugenzi wa Halmashauri wanapaswa kuzingatia utaratibu huo uliowekwa katika ukusanyaji wa kodi hiyo, alieleza Dkt. Kijaji.

Imetolewa na;
Benny Mwaipaja
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Fedha na Mipango

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

HATUTOPAKI BASI DHIDI YA YANGA-MOKWENA

“PEMBA SALUTI KWENU” DK. NCHIMBI*