Na Zainab Nyamka, Globu ya jamii
SHIRIKISHO
la Mpira Kikapu Tanzania(TBF) imetangaza rasmi tarehe ya mashindano ya
kikapu ya FIBA Zone V U18 (Wanawake na Wanaume ) kuwa yanatarajiwa
kuanza June 17 hadi 22 2018 hapa Jijini Dar Es Salaam, Tanzania.
Rais
wa TBF Pharess Magesa amesema matarajio yao ni kuwa mmoja kati viongozi
wetu wakuu wa nchi ndyie atakuwa mgeni rasmi wa mashindano hayo na
yatarushwa mubashara (live) siku zote za mashindano na vituo vyote
vikubwa vya TV na Radio ambavyo wametuma maombi.
Magesa
amesema gharama za maandalizi ya timu zetu mbili za Taifa na gharama
za kuandaa mashindano haya ni kubwa, na tayari kuna wadau
wameshajitokeza kutoa ahadi na wengine wameshasaidia.
"Hadi
sasa hivi TBF ina upungufu wa takribani Sh.milioni 100, kati ya hizo
Sh.milioni 60 ni za kuandaa mashindano na Sh.milioni 40 ni za kuweka
timu zetu 2 za wanawake na wanaume kambini na kununua vifaa vya michezo
zikiwemo Jersey za kucheza na za mazoezi, truck suits, viatu, socks,
mipira na madawa,"amesema Magesa.
"Pia,
tuna mahitaji mengi ili kufanikisha matengenezo ya uwanja wa ndani wa
Taifa (indoor) ukiacha kuvuja paa na kukatika kwa umeme ambako
kutadhibitiwa na msaada ulitolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul
Makonda,"amesema.
Katika
uwanja huu wa Taifa bado kunahitajika matengenezo ya mfumo wa taa na
vifaa vya umeme, mabomba, vyoo na mfumo wa maji, mabenchi ya kukalia,
mfumo wa kutoa na kuingiza hewa (ventilation), na rangi ya kupaka ndani
na nje ili kuweka mazingira ya uwanja yawe ya kuvutia.
Uwanja
wa ndani wa Taifa utatumika kwa mashindano haya ya U18 June na pia
baadae utatumika kwa mashindano ya kutafuta Klabu Bingwa wa Kikapu FIBA
Zone V yanayotarajiwa kufanyika mwezi Septemba, 2018 hapa hapa Dar Es
Salaam.
Ameelezea,
kuna gharama za usafiri, posho na malazi ya Kocha wa Kigeni ambaye
anatoka Minneapolis, Marekani, Coach Matthew McCollister ambaye
anatarajia atafika nchini walau majuma 2 kabla ya kuanza mashindano haya
ili kuzinoa timu zetu 2 kwa kushirikiana na jopo la makocha Wazalendo
wakiongozwa na Coach Bahati Mgunda.
"Tunatarajia
mashindano ya FIBA Zone V U18 yatakayofanyika mwezi ujao yatashirikisha
timu za Taifa 24, za wanawake na wanaume, kutoka nchi 12 za Misri,
Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Ethiopia, Eritrea, Djibouti, Sudan,
Somalia, Sudani Kusini na wenyeji Tanzania. Bingwa wa mashindano haya
atapata nafasi ya kushiriki mashindano ya kutafuta bingwa wa Afrika
(Afrobasket 2018) baadae mwaka huu,"amesema.
Rais
TBF amesema wanatarajia kutakuwa na wageni takribani 400 kutoka nchi
mbali mbali ikiwa ni pamoja na maofisa kutoka FIBA, waandishi na wadau
kutoka nchi husika.
Ametoa
mwito kwa wapenzi wote wa michezo nchini, Serikali, taasisi za umma na
binafsi, wafanyabiashara, wanasiasa, wafanyakazi na wananchi wote kwa
ujumla kujitokeza na kushirikiana na TBF kufanikisha maandalizi
mashindano haya ili ikiwezekana vikombe vyote vibaki nchini na kuzipatia
nafasi timu zetu za Tanzania kushiriki Mashindano makubwa ya Kikapu ya
FIBA Afrika.
Ameomba
tumuunge mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John
Magufuli kwa kila mtu kuwajibika katika eneo lake, kujenga Tanzania ya
viwanda ili kusaidia ukuaji wa uchumi na hatimaye kuifanya nchi yetu
kuwa na uchumi wa kipato cha kati haraka zaidi ya ilivyotarajiwa.
Ameongeza
"Michezo ni moja ya viwanda vikubwa vinavyotengeneza ajira nyingi za
moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja kama tutafanya uwekezaji
sahihi. Mchezo wa kikapu ni mchezo pekee nchini unaopendwa na watu wengi
wa rika na jinsia zote kwa usawa. Hivyo basi kusaidia mchezo huu
utakuwa umefanya sehemu kubwa ya kusaidia jitihada za Serikali za
kusaidia na kuendeleza vijana wetu na kuchangia katika maendeleo ya
Taifa letu kwa ujumla,".
Comments