Trump aufuta mkutano kati yake na Kim Jong-un



Rais wa Marekani Donald Trump ameufuta mkutano wa kihistoria kati yake na kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong-un uoliopangiwa kufanyika mwezi ujao.
Amesema uamuzi wake umetokana na "ghadhabu kuu na ukali wa wazi" uliokuwa kwenye taarifa ya karibuni ya Korea Kaskazini.
Bw Trump amesema haingekuwa vyema kuendelea na mkutano huo nchini Singapore Juni 12 kama ilivyokuwa imepangwa.
Kwenye barua kwa Bw Kim, amesema anasubiri sana kwa hamu kukutana naye "siku moja".

Trump amesema nini hasa?

Trump amesema kuwa Marekani ilifahamishwa kuwa Korea Kaskazini ilikuwa imetuma maomba ya kufanyika kwa mkutano huo, lake kwa utawala wake hilo sio muhimu.
Rais huyo wa Marekani ameendelea kusema kwamba alikuwa na matarajio makubwa ya kukutana na kiongozi huyo wa korea kaskazini, lakini kutokana na hasira na uhasama wa wazi uliojitokeza katika taarifa ya hivi karibuni ya korea kaskazini, haoni ni muafaka kwa mkutano huo kuendelea kama ulivyopangwa.
Amesema kwa mujibu wa barua hiyo mkutano huo sasa hautafanyika.
Kinyume na matarajio ya wengi Rais trump amejigamba kuwa licha ya Korea Kaskazini kuzungumzia uwezo na ushawishi wake kuhusiana na silaha za nuklia, taifa la marekani lina silaha nyingi za nyuklia kuliko Korea Kaskazini na ni maombi yake kuwa silaha hizo hazitatumika.
Katika barua hiyo iliyojawa na hisia za machungu na maridhiano, Rais Trump amesema kuwa ni matarajio yake kuwa siku moja watakutana.
Wakati huo huo amemshukuru kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong-un kwa kuwaachiliwa huru raia wa Marekani waliokuwa kizuizini chini ya utawala wake na kusema kuwa Marekani ilifarijika na kitendo hicho.
Trump alimalizia barua yake kwa kusema kuwa Dunia na Korea Kaskazini zimepoteza nafasi muafaka ya kutafuta amani ya kudumu, maendeleo na utajiri.
Utawala wa Pyongyang haujatoa tamko lolote kufuatia uamuzi huo wa marekani.
Tangazo hilo limetolewa saa chache baada ya Korea Kaskazini kukisiwa kuharibu kiwanda chake kikuu cha kufanyia majaribio ya zana zake za nyuklia, kama ishara yania njema kuthibitisha kuwa ipo tayari kushiriki katika mazungumzo ya amani na Marekani, licha ya msukosuko wa hivi karibuni.

Kuharibu mahandaki

Hii leo, waandishi wa kimataifa wa habari, wapatao thelathini, walialikwa kushuhudia zoezi hilo katika eneo la Pungyeri.
Waandishi hao wamesema kuwa waliona mlipuko mkubwa katika maeneo ya milima kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.
Wamesema kuwa maafisa wa Korea Kaskazini walihakikisha kuwa kamera zote zilikuwa tayari kunakili kabla ya milipuko hiyo kuanza.
Ripoti zinasema kuwa mahandaki ambayo yalikuwa yakitumika kufanyia majaribio zana za nyuklia yaliharibiwa
Mwandishi mwingine wa habari amesema pia alishuhudia mnara mmoja wa ulinzi ukianguka.
Hata hivyo hakuna wataalamu huru waliruhusiwa kushuhudia tukio hilo.
Hali hii inaifanya kuwa ngumu zaidi kuthibitisha ikiwa zoezi hilo lilikamilika au kiwanda hicho kinaweza kukarabatiwa.

Kumtusi Mike Pence

Afisa wa cheo cha juu wa Korea Kaskazini alikuwa mapema leo amemlaumu Makamu wa Rais wa Marekani Mike Pence kwa kuwa "mjinga" na kuonya kuwa kutakuwa na maonyeshano ya ubabe wa nyuklia ikiwa mazungumzo yatafeli.
Choe Son-hui alisema Pyongyang haitaweza kuibembeleza Marekani kwa mazungumzo.
Siku za hivi karibuni pande hizo mbili zilikuwa zimeonya kuwa mkutano wa Juni 12 unaweza kuharishwa au kufutwa kabisa.
Korea Kaskazini ilisema itafikiria tena iwapo itahudhuria mkutano ikiwa Marekani itaendelea kusisitiza kuwa iachane na mpango wa silaha za nyuklia.
Rais wa Marekani Donald Trump siku ya Jumanne alisema Korea Kaskazini ndiyo ingetimiza masharti ya kufanyika kwa mazungumzo hayo.
Choe Son-hui amehusika kwenye mazungumzo mara kadha na Marekani kwa karibu miaka kumi iliyopita.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATANZANIA WATAKAOVAA JEZI ZA MAMELODI AU AL AHLY

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

KOCHA BENCHIKHA AMESEPA

MASHUSHUSHU WA MAMELODI WALIKUJA KUTUPELELEZA: HERSI