WAKUU WA MIKOA KANDA YA ZIWA VICTORIA WAKOSOA VIKALI TABIA YA WANASIASA KUIPAKA MATOPE DHAMIRA NJEMA YA SERIKALI KUPAMBANA NA UVUVI HARAMU
NA JOHN MAPEPELE, MWANZA
WAKUU
wa mikoa inayozunguka Ziwa Victoria wamekosoa vikali tabia ya baadhi ya
wanasiasa kuipaka matope dhamira njema ya Serikali ya kupambana na
uvuvi haramu ulioshamiri katika ziwa hilo na kutaka viongozi wa aina
hiyo kutangaza masilahi yao kwenye eneo la uvuvi kabla ya kuwashambulia
viongozi wanaosimamia zoezi hilo kwa misingi ya kisheria.
Wakizungumza
kwenye kikao cha tathmini ya operesheni sangara awamu ya pili
iliyowahusisha Wakuu wa Mikoa,Wakuu wa Wilaya, Makatibu Tawala wa Mikoa,
Wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya, Makamanda wa Polisi wa mikoa na
Wakuu wa Idara ya Usalama wa Taifa wa mikoa yote inayozunguka Ziwa
Victoria jijini Mwanza jana viongozi hao wametaka hatua zaidi
zichukuliwe ili kunusuru rasilimali hizo muhimu kwa maendeleo ya Taifa.
Mkuu
wa Mkoa wa Simiyu, Antony Mtaka alielezea kuchukizwa na tabia inayoanza
kuota mizizi ya baadhi ya viongozi wa kisiasa kuipaka matope dhamira
nzuri ya Serikali ya kukabiliana na uvuvi haramu na kutaka viongozi wa
aina hiyo watangaze masilahi yao kabla ya kuanza kuwashambulia viongozi
wanaosimamia operesheni hiyo inayotekelezwa kwa mujibu wa sheria .
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina akihutubia hadhara ya kikosi kazi cha watu 260 alichokiunda kwa ajili ya operesheni Sangara 2018 na Wakuu wa Mikoa mitano inayozunguka Ziwa vicktoria wakati wa mkutano wa kufanya tathimini ya Operesheni hiyo. Picha na John Mapepele
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina akihutubia hadhara ya kikosi kazi cha watu 260 alichokiunda kwa ajili ya operesheni Sangara 2018 na Wakuu wa Mikoa mitano inayozunguka Ziwa vicktoria wakati wa mkutano wa kufanya tathimini ya Operesheni hiyo. Picha na John Mapepele
Viongozi
wakuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi waliokaa wakiwa katika picha ya
pamoja na makamanda wakuu wa Operesheni Sangara 2018 (waliosimama)
wakati wa mkutano wa kufanya tathimini ya Operesheni hiyo.
“Viongozi
wanaopinga operesheni ya kupambana na uvuvi haramu ni muhimu watangaze
kwanza masilahi yao kuhusu eneo la uvuvi ili wasiendelee kuchafua
taswira za viongozi wanaosimamia wizara hii”alisema Mtaka.
Naye
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongela alisema kumekuwepo na dhana
zinazojengeka kwamba viongozi wa mikoa inayozunguka Ziwa Victoria
hawaungi mkono mapambano ya kukabiliana na uvuvi haramu operesheni jambo
ambalo alisema ni upotoshaji mkubwa na kwamba Serikali ya mkoa iko
mstari wa mbele na kuwabana watendaji wa ngazi zote watakaobanika
kufadhili uvuvi haramu.
Alisema
ni muhimu operesheni hiyo iwe endelevu na kubainisha kuwa suala la
uvuvi haramu haliwezi kumalizika kama hakuna dhamira ya dhati miongoni
mwa wasimamizi wa sheria na kwamba uongozi wa mkoa huo hautakubali
kuendelea kuwa na watumishi wazembe wataoshindwa kusimamia suala hilo.
Kwa
upande wake Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina alitangaza kuanza
kwa awamu ya tatu ya Operesheni Sangara yenye lengo la kupambana na
uvuvi haramu katika Ziwa Victoria sambamba na kutangaza operesheni
katika maziwa yote na kuagiza viongozi wakuu wa mikoa na wilaya
kuwachukulia hatua kali viongozi wa chini wanaobanika kujihusisha na
kufadhili uvuvi haramu.
Viongozi
wakuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi waliokaa wakiwa katika picha ya
pamoja na sekretarieti ya Operesheni Sangara 2018 (waliosimama) wakati
wa mkutano wa kufanya tathimini ya Operesheni hiyo.
Pia
alitangaza kuunda kanda mpya ya udhibiti na usimamizi rasilimali za
uvuvi katika wilaya za Ukerewe na Sengerema huku akiunda ofisi mpya ya
Kanda jijini Mwanza itakayokuwa inaratibu shughuli zote katika kanda
hizo saba ili kuongeza usimamizi madhubuti wa rasilimali hizo.
Aidha
Mpina aliongeza kuwa katika awamu ya tatu ya operesheni hiyo itahusisha
pia Mahakama zinazotembea ili kuweza kutoa hukumu huko huko ziwani hali
itayowezesha kuondokana kabisa na uvuvi haramu.
Aidha
aliwataka watu wote wanaopinga operesheni ya uvuvi haramu wasome
takwimu ili kujua ukubwa wa tatizo katika Ziwa Victoria ambapo jumla ya
watuhumiwa 3,284 wamekamatwa kujihusisha na uvuvi haramu huku samaki
wasioruhusiwa kilo 326,751 , mabondo kilo 5,142 zilikamatwa zikitoroshwa
kwenda nje ya nchi na nyavu haramu 566,497 nazo zilikamatwa na
kuteketezwa. Pia magari 257, mitumbwi 1278 , pikipiki 269 na injini za
mitumbwi 564 vilikamatwa vikihusishwa na makosa ya uvuvi haramu.
Alisema
katika baadhi ya maeneo ya Bushengere wilayani Ukerewe wazazi
wamewaonya watoto wao kutotumika na mafisadi kwenye uvuvi haramu kwani
wakikamatwa wao ndio wanaopata tabu na kutelekezwa ambapo wameweka
azimio la kukataa kutumika tena kwenye jambo hilo.
Alisema
kutokana na operesheni hizo zinazoendelea za kupambana na uvuvi haramu
hadi kufikia mwezi Disemba mwaka huu watu wote wanaopinga na hata
kuwaombea mabaya viongozi wa operesheni watapata aibu kubwa kwani idadi
ya samaki itaongezeka huku akitoa wito kwa viongozi wa ngazi zote wenye
mapenzi mema na nchi kuunga mkono vita hiyo kwa manufaa ya Taifa.
Katibu
Mkuu Uvuvi, Dk. Yohana Budeba alisema wizara hiyo imejipanga kikamilifu
kuhakikisha sekta ya uvuvi inatoa mchango mkubwa katika pato la Taifa
na kwamba operesheni hiyo itaendelea hadi pale uvuvi haramu utakapokoma.
Mkuu
wa Wilaya ya Busega, Tano Mwera alisema wamekuwa wakipokea malalamiko
mengi kuhusu operesheni hiyo lakini kila walipofuatilia kupata ushahidi
wa malalamiko hayo waliukosa jambo ambalo wamebaini kuwa ni njama za
makusudi za kutaka kuhujumu nia njema ya Serikali ya kupambana na
kutokomeza uvuvi haramu.
Kamanda
Mkuu wa operesheni hiyo kutoka Ofisi ya Rais (TAMISEMI), Hassan
Shelukindo alisema katika operesheni hiyo jumla ya watuhumiwa 22
wakiwemo wenyeviti wa vijiji na vitongoji na viongozi wa BMU wamefungwa
jela huku wengine 17 mashauri yao yakiwa yanaendelea Mahakamani kwa
makosa ya kujihusisha na uvuvi haramu.
Shelukindo
alisema pia watumishi 6 walikuwa kwenye operesheni hiyo waliondolewa
kwa makosa mbalimbali ikiwemo ukiukwaji wa maadili ya kazi ambapo
watumishi hao watachukuliwa hatua za kinidhamu na taasisi zao huku jumla
ya sh. bilioni 7.5 zikikusanywa kutokana na faini pamoja mauzo ya
mabondo,samaki na kayabo.
Comments