HUU NDIYO UANAUME...!!!

MKE ALIYEDAI TALAKA KISA HASIRA

Anasimulia mke : Siku moja nilimwomba mume wangu kabla hajaenda kazini aniletee kitu fulani atakaporudi. Nikamkumbusha asisahau kabisa.

Aliporudi jioni kutoka kazini, mikono yake ilikuwa mitupu hakuwa ameniletea nilichomuomba. Nilikuwa nimekasirika tayari, na hasira ilizidi mara nilipomuona hajaleta nilichotaka, licha ya kumbusha asisahau.

Sikuweza kujizuia nilimfokea kwa sauti ya juu na kuanza kugombana naye. Nilikuwa nakasirika zaidi kwa sababu alikuwa kimya, hakunijibu hata neno moja, wala hakuniangalia usoni. Hilo lilinikasirisha zaidi. Mwishowe nikamwambia anipe talaka, na nikasisitiza kwa nguvu.

Lakini hakuonyesha kujali kuhusu ombi langu la kutaka talaka. Aliniacha na kwenda chumba cha kulala. Nikamfuata, nikamshika shati na kumwambia:
"Kama wewe ni mwanaume basi nitupie talaka na uniachie!"

Ghafla uso wake ulibadilika, na nilijua kuwa maneno yangu yamemuumiza sana lakini sikujali.

Akasema:
"Sawa, chukua mtoto wako uende kwa wazazi wako, nitakutumia karatasi ya talaka."

Nikachukua binti yetu mdogo na kurudi nyumbani kwa wazazi wangu. Hali yao kifedha haikuwa nzuri, lakini nilikuwa nimeweka akiba kidogo kutoka matumizi ya kila siku. Nikaendelea kutumia hela hiyo kwa ajili yangu na familia yangu.

Baada ya siku mbili, mume wangu alikuja na kunipa karatasi ya talaka, kisha akaondoka bila kuniachia hata senti kwa ajili ya matumizi ya mtoto wetu.

Nilijisikia kuumia sana. Nikachukua karatasi ile na kuiweka kwenye kabati langu.

Siku kumi baadaye, hela zote nilizokuwa nazo zikaisha. Hali yetu nyumbani ikazidi kuwa mbaya sana. Hakukuwa na chakula hata kidogo jikoni na nilikuwa mjamzito wa miezi saba.

Nikaingia chumbani na nikakumbuka ile karatasi. Kwa hamu na mshangao nikaitoa kabatini, nikafungua na hapo nikapata mshtuko mkubwa zaidi ya nilivyotarajia.

Ndani ya ile karatasi kulikuwa na hela zinazotosha matumizi ya mwezi mzima. Na haikuwa karatasi ya talaka ilikuwa ni barua.

Barua ilisema:

“Mke wangu mpenzi, unaendeleaje wewe na binti yetu mrembo? Nimekukwaza sana. Samahani kwa kutokukuletea ulichoniomba, si kwa sababu nilisahau bali nilikuwa na mpango tutoke wote kula chakula cha mchana na kisha nikununulie kila unachotaka. Lakini nilipoona umeudhika na kukasirika, nilinyamaza si kwa woga, bali kwa hofu usijichoshe, hasa ukiwa mjamzito. Niliamua kujizuia nisijibu maneno yako makali.

Nilikimbilia chumbani kwetu kwa hofu ya kupoteza udhibiti wa hasira zangu na mambo kuwa mabaya zaidi. Uliposema, ‘Kama wewe ni mwanaume, nitupie talaka,’ nilijua neno lile lilinidhalilisha lakini sikumaanisha kuwa kuwa mwanaume ni kutoa talaka kwa hasira.

Ndiyo, maneno yako yalinijeruhi, lakini bado wewe ni mke wangu mpendwa, mama wa watoto wangu.

Mwisho wa barua, nimeweka pesa zitakazotosha kwa matumizi yako ya mwezi mzima ili usihitaji chochote.
Na kama unataka kurudi, karibu sana utapendezesha nyumba yetu.
Na kama bado una hasira nami na unataka kubaki kwa wazazi wako, ni sawa  nitakuheshimu.”

Nilikuwa nasoma barua hii huku machozi yananitiririka. Nilijisikia na majuto makubwa nilielewa kosa langu. Mara moja nikaanza kukusanya vitu vyangu, nikampigia simu mume wangu nikiwa nalia, nikimuomba msamaha kwa yote niliyomtendea.

Alinivunja kwa maneno hayo ya upole na upendo. Yaliyonichoma ndani ya moyo wangu kwa kila herufi.

Baada ya saa moja, mume wangu alipiga hodi mlangoni. Nilimkumbatia kwa nguvu huku nikilia, nikambusu kichwa chake, nikamuomba anisamehe.

Akanipa pesa mkononi kwa ajili ya baba yangu, kisha tukarudi nyumbani.

Tangu siku hiyo hadi leo: sijawahi kumpigia kelele tena, wala kumdai chochote.
Anapotoka, huuliza:
“Unahitaji kitu mke wangu?”
Na mimi humjibu:
“Sitaki chochote, zaidi ya urejee salama ukiwa na afya njema.”

Mafunzo Muhimu Kutoka Katika Hadithi Hii ya Kusisimua na igusacho Moyo:

1.Hasira ni Adui Mkubwa wa Maamuzi Sahihi

👉Mwanamke alikasirika kwa sababu ndogo mumewe kusahau kitu alichoomba. Hasira ilimpelekea kumdhalilisha mumewe na hata kumwomba talaka. Baadaye aligundua kuwa hasira zake zilimfanya atangulize maneno bila kufikiri.

📝Funzo:Kabla hujazungumza ukiwa na hasira, nyamaza. Maneno yenye sumu yakitoka, hayawezi kurudi. Subira ni silaha ya wenye busara.

2.Ukimya si Udhaifu, Bali ni Hekima
👉Mume alikaa kimya alipofokewa, si kwa woga, bali kwa hekima alijua kwamba kujibu kwa hasira kungeharibu ndoa zaidi. Alijizuia ili kulinda nyumba yake.

📝Funzo:Wanaume au wake waliokomaa kiakili, hujua lini wazungumze na lini wakae kimya. Ukimya wakati wa hasira unaweza kuwa wokovu wa ndoa.

3.Mwanamume wa Kweli Hujua Upole Wakati wa Maumivu
👉Alijeruhiwa kwa maneno ya mkewe, lakini bado alimuita “mke wangu mpenzi” na kumtumia hela kwa ajili ya mahitaji yake. Alijua kuwa maumivu hayatibiwi kwa maumivu zaidi.

📝Funzo:Mwanaume wa kweli huonyesha utu wake katika nyakati za jaribio. Kupenda si kulipiza, bali kuvumilia.

4.Usikurupuke Kutaka Talaka kwa Hasira
👉Mke alitaka talaka bila kufikiri, akadhani suluhisho la matatizo madogo ni kutengana. Alipoondoka, ndipo aligundua thamani ya mumewe na kosa lake.

📝Funzo:Talaka ni tiba ya mwisho, si silaha ya mapambano. Jaribu kuelewana kabla ya kuamua kuachana.

5.Thamani ya Mume/Mke Haitokani na Zawadi, Bali na Moyo

👉Licha ya kumwudhi, mumewe alimsamehe, akamwambia anaweza kurudi wakati wowote. Hakuweka masharti wala visasi. Huu ni moyo safi wa kweli.

📝Funzo:Thamani ya ndoa hujengwa na moyo wa msamaha, si kiwango cha mapato wala zawadi.

6.Subira ni Njia ya Amani Katika Ndoa
👉Baada ya tukio hili, mke alijifunza kuwa mvumilivu, hakuomba vitu ovyo, na kila alipoulizwa kama anahitaji kitu, alikuwa akisema:
“Sitaki chochote zaidi ya urudi salama.”

📝Funzo:Subira huleta utulivu wa familia. Kutunza maneno, kuheshimiana, na kushukuru kwa vilivyopo ni mboni ya ndoa bora.

7.Mwandiko wa Upendo Huumiza Zaidi ya Fimbo
👉Barua ya mumewe ilimfanya amwage machozi. Haikumshtaki, haikumlalamikia  bali ilimkumbatia kwa maneno matamu yaliyobeba maumivu na msamaha.

📝Funzo:Maneno ya upole yana nguvu ya kubadilisha moyo uliojaa hasira kuwa wa toba na huruma.

Dua:
"Ee Mola, tujaze subira, utu, na huruma katika maisha yetu ya ndoa. Usituachie katika hasira zetu. Tupe hekima ya kimya na nguvu ya msamaha." 🤲
Ee Mola, tujaalie kuwa miongoni mwa wenye subira.

Na usiache kufuatilia ukurasa wa Sufian Mzimbiri 
Nawapenda kwa ajili ya Allah ❤️



 

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

DUNIA NI KATILI SANA KWA MWANAUME MASIKINI

MWANAUME USIPITWE NA HILI, INASIKITISHA...?!!!

HUYU NDIYE MWANAMKE WA KUOA

DIARRA KIPA BORA TANZANIA

CHINYELE ACHUKUA FOMU KUOMBA RIDHAA YA KUGOMBEA UBUNGE DODOMA MJINI

MAKUNDI YA VILABU VINAVYOSHIRIKI KOMBE LA DUNIA 2025.