Mahakama kutoa hukumu kesi ya Nguza Viking na mwanaye Papii Kocha Tanzania


Mahakama ya Afrika na Haki za Binadamu (AfCHPR) inatoa hukumu katika kesi iliyowasilishwa na wanamuziki Nguza Viking maarufu Babu Seya na mwanaye, Johnson Nguza 'Papii Kocha' dhidi ya serikali ya Tanzania katika mahakama hiyo.
Wawili hao waliwasilisha rufaa katika mahakama hiyo mwaka 2015 kupinga hukumu ya kifungo cha maisha iliyokuwa imetolewa dhidi yao.
Walikuwa wanatumikia kifungo cha maisha jela kwa kuwabaka wasichana 10 wa shule waliokuwa na kati ya umri wa miaka 6 na 8 mwaka 2003.
Walikuwa wametumikia kifungo cha miaka 13 kufikia wakati wa kupewa msamaha
Babu Seya ambaye ni miongoni mwa wafungwa 1,821 waliosamehewa na Rais John Magufuli siku ya Uhuru wa Tanganyika mnamo 9 Desemba, 2017.
Wengine 8157 walipunguziwa adhabu zao.
Wawili hao ndio walioimba kibao maarufu cha 'Seya' na walikuwa kati ya wafungwa 61 waliokuwa wamehukumiwa kufungwa maisha au kunyonga ambao walinufaika kutokana na msamaha wa rais.
Haki miliki ya picha Ikulu
Image caption Nguza Viking na wanawe walipokutana na Magufuli
Hukumu katika kesi yao ilikuwa imepangiwa kusomwa Jumatano wiki hii lakini baadaye ikaahirishwa hadi leo.
Mahakama hiyo kupitia ujumbe Facebook imesema hukumu itaanza kusomwa mwendo wa saa tano saa za Afrika Mashariki.
Hatua ya Dkt Magufuli kuwasamehea wawili hao ilishutumiwa na watetezi wa haki za watoto na wanawake.
Kate McAlpine, mkurugenzi wa shirika la Community for Children Rights lenye makao yake Arusha aliambia BBC wakati huo kwamba alikuwa "ameshtushwa lakini hakushangazwa" na hatua ya rais huyo. Alisema hatua hiyo ilionesha 'uelewa mdogo' wa kiongozi huyo kuhusu masuala ya udhalilishaji wa watoto.
Alilinganisha hatua hiyo na tamko la Rais Magufuli kwamba wasichana wanaoshika mimba hawafai kuwa shuleni.
"Huwa hafahamu vyema mambo, hasa yanayohusu watoto kama waathiriwa. Wasichana wanaoenda shule hushika mimba kwa sababu mara nyingi ni waathiriwa wa udhalilishaji," alisema Bi McAlpine.

Wakishinda watadai fidia?

Kwa kuwa wawili hao walishasamehewa na rais, uwezekano wao kuchukuliwa hatua iwapo hukumu ya kifungo dhidi yao itadumishwa ni mdogo sana.
Hata hivyo, iwapo watapatikana bila hatia, kuna uwezekano huenda wakawasilisha kesi wakitaka walipwe fidia kwa kipindi ambacho walikaa gerezani.

Ilikuwaje hadi tukafika hapa?

Nguza Viking na wanawe watatu walikuwa wamehukumiwa kifungo cha maisha jela kwa makosa ya kuwabaka na kulawiti watoto.
Mwaka 2010 rufaa yao ilisikilizwa na 30 Oktoba Majaji Nathalia Kimaro, akisaidiana na Mbarouk Mbarouk na Salum Masati katika Mahakama ya Rufaa wakawaachilia huru Nguza Mashine na Francis Nguza baada ya kuwapata bila hatia.
Babu Seya na mwanaye Papii Kocha walipatikana na hatia na hivyo kuendelea kutumikia adhabu ya kifungo cha maisha jela.
Majaji walisema kuwa kuna uthibitisho kuwa warufani hao wawili waliwabaka watoto wa shule ya msingi mwaka 2003.
Kesi hiyo iliwashtua mashabiki wa mwanamuziki Viking nchini Tanzania, na kanda nzima ya Afrika Mashariki.
Mwanamuziki huyo mwenye kuimba nyimbo za rhumba, ambaye ni mzaliwa wa DRC, ameishi Tanzania kwa miaka mingi na kuwa na mashabiki wengi.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

HATUTOPAKI BASI DHIDI YA YANGA-MOKWENA

“PEMBA SALUTI KWENU” DK. NCHIMBI*