𝗡𝗔𝗜𝗕𝗨 𝗪𝗔𝗭𝗜𝗥𝗜 𝗔𝗜𝗧𝗔𝗞𝗔 𝗲-𝗚𝗔 𝗞𝗨𝗜𝗠𝗔𝗥𝗜𝗦𝗛𝗔 𝗨𝗦𝗛𝗜𝗥𝗜𝗞𝗜𝗔𝗡𝗢 𝗡𝗔 𝗦𝗘𝗞𝗧𝗔 𝗕𝗜𝗡𝗔𝗙𝗦𝗜

 

NAIBU Waziri Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Deus Clement Sangu (Mb), ameitaka Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) kuimarisha ushirikiano na sekta binafsi, ili kuongeza wigo wa ajira kwa vijana wabunifu kwenye eneo la TEHAMA.

Mhe. Sangu ametoa rai hiyo hivi karibuni, wakati akifunga programu ya awamu ya tano ya mafunzo kwa vitendo (practical training) pamoja na mafunzo kazini (internship) kwa mwaka wa fedha 2024/2025, inayoendeshwa na e-GA kupitia Kituo chake cha Utafiti, Ubunifu na Uendelezaji wa Serikali Mtandao (e-GovRIDC) jijini Dodoma.

“Naipongeza e-GA kwa kazi nzuri mnayofanya ya kukuza vipaji na kuongeza uwezo kwa vijana katika matumizi ya TEHAMA, lakini pia nawashauri kuimarisha ushirikiano na sekta binafsi ili kutoa fursa kwa wanafunzi wanaoshiriki mafunzo kwa vitendo pamoja na mafunzo kazini katika kituo hiki kupata fursa za ajira “, alisema Mhe. Sangu.

Alibainisha kuwa, ushirikiano kati ya e-GA na sekta binafsi utaongeza tija katika kukuza na kuimarisha tasnia ya TEHAMA, na hivyo kuongeza fursa za ajira kwa vijana na hatimaye kupunguza changamoto ya ajira kwa taifa.

Itakumbukwa kuwa hivi karibuni, baadhi ya taasisi binafsi zikiwemo Benki na Kampuni za Simu za Mkononi, zilitembelea kituo hicho na kuonesha nia ya kusaini Mkataba wa Makubaliano ya ushirikiano (MOU) katika masuala ya elimu, utafiti, na ubunifu wa TEHAMA, ikiwa ni hatua inayolenga kuimarisha ushirikiano kati ya e-GA na taasisi hizo.

“Nimetembelea miradi ‘projects’ mbalimbali zinazoendelea katika kituo hiki na nimeona kazi kubwa ambayo e-GA mnaifanya ya kuwaandaa vijana wetu, ili waweze kuendana na mabadiliko ya teknolojia mpya zinazoibukia kama vile Akili Mnemba ‘Artificial Intelligence- AI’, ‘Machine Learning, ‘Blockchain’ na Sarafu ya Kidijitali ‘Digital Currency’ na nimeona jinsi vijana wetu walivyo na uwezo mkubwa katika maeneo hayo”, alisema Mhe. Sangu.

Aidha, aliipongeza e-GA kwa kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha vijana wanajifunza teknolojia mpya zinazoibuka duniani, ili waweze kufanya bunifu mbalimbali za TEHAMA ikiwa ni pamoja na kutengeneza mifumo ya kielektroniki kupitia teknolojia hizo itakayosaidia kuongeza ufanisi wa utendaji kazi Serikalini na utoaji wa huduma kwa wananchi.

“Mafunzo haya mnayoyatoa yanawasaidia wanafunzi kuongeza ujuzi na uzoefu katika kuzielewa teknolojia mpya ili kuchochea maendeleo na mageuzi makubwa ya Serikali ya kidigitali, na hivyo kuwa na kizazi chenye ujuzi wa kutosha kuhusu TEHAMA na hatimaye kushiriki katika kuijenga Serikali ya Kidijitali”, alifafanua Mhe. Sangu.

Alibainisha kuwa, Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi na kuijengea uwezo Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), ili kuhakikisha matumizi ya TEHAMA Serikalini yanazidi kuimarika sambamba na kuandaa vijana mahiri katika TEHAMA ili washiriki katika ujenzi wa Serikali ya Kidijitali.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa e-GA Mhandisi Benedict Ndomba, aliahidi kuendeleza na kuimarisha ushirikiano na sekta binafsi, pamoja na kuwajengea uwezo vijana katika TEHAMA ili kutoa fursa kwa vijana kuonesha uwezo wao katika TEHAMA na kuweza kushindana katika soko la ajira duniani.

“e-GA itaendeleza ushirikiano na sekta binafsi pamoja na Vyuo Vikuu mbalimbali ili kuwajengea uwezo vijana katika eneo la TEHAMA, lakini pia kuwawezesha kushindana katika soko la ajira duniani na kwa kufanya hivyo, tutakuwa tumesaidia kupunguza changamoto ya ajira nchini”, alisisitiza Ndomba.

Akizuzungumza kwa niaba ya wanafunzi walioshiriki program hiyo, Bw. Philemon Mbunda ambaye pia ni mwanafunzi wa mwaka wa tatu kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), ameishukuru e-GA kwa kupata fursa ya kushiriki katika programu hiyo ambayo imewasaidia kuongeza ujuzi na uzoefu katika kuzifahamu teknolojia mpya zinazoibukia.
“Tumekuwa hapa kwa muda wa wiki kumi na tumejifunza mambo mengi kuhusu teknolojia zinazoibukia na namna tunavyoweza kuzitumia katika kubuni mifumo mbalimbali itakayoleta tija kwa taifa letu, tunaahidi kuwa mabalozi wazuri na kuhakikisha elimu tuliyoipata hapa tunaiendeleza kwa vitendo”, alisema Bw. Philemon.

Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), huendesha programu ya mafunzo kwa vitendo kila mwaka ambapo, huchukua vijana kutoka vyuo mbalimbali ndani na nje ya nchi ili kuwajengea uwezo katika TEHAMA na kuweza kushindana katika soko la ajira, ambapo kwa mwaka wa fedha 2024/2025 wanafunzi 65 kutoka Vyuo Vikuu 12 walishiriki programu hiyo kwa muda wa wiki 10.



Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

𝗠𝗕𝗢𝗪𝗘 𝗔𝗦𝗜𝗧𝗜𝗦𝗛𝗔 𝗠𝗔𝗔𝗡𝗗𝗔𝗠𝗔𝗡𝗢 𝗬𝗔 𝗖𝗛𝗔𝗗𝗘𝗠𝗔 𝗬𝗔 𝗧𝗔𝗥𝗘𝗛𝗘 𝟮𝟯.

KAMATI YA UWT KUTOA MSAADA WA KISHERIA NCHINI

KIKOSI CHA CBE KIMEWASILI ZENJI KUVAANA NA YANGA

YANGA YAWASILI SALAMA ETHIOPIA

DEMU KAMA ANAFANYA KAZI HIZI KUWA MAKINI NAE.

MAYELE AIMWAGIA SIFA LUKUKI YANGA