Chaz Baba amejificha kwenye kichaka, ilhali makalio yako nje


NAMFAHAMU vyema na nimekuwa nikifuatilia nyendo zake kwa karibu mwanamuziki nguli wa bendi ya African Stars 'Twanga Pepeta', Charles Gabriel Cyprian 'Chaz Baba' tangu alipotua bendi hiyo akitokea Mchinga Sound.

Wakati huo Mchinga Sound ilikuwa ikimilikiwa na aliyepata kuwa Naibu Waziri wa Habari Utamaduni na Michezo na Naibu Waziri wa Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi na Mbunge wa Jimbo la Mchinga, Mudhihir Mudhihir.

Uhamisho wa Chaz Baba kutoka Mchinga Sounda kwenda Twanga Pepeta ulizua tafrani kubwa kati ya Mudhihir na Mkurugenzi wa Kampuni ya African Stars Entertainment Tanzania (ASET), Asha Baraka, hadi kufikia hatua ya kurushiana makonde Leaders Club.

Tuyaache hayo! Chaz Baba ambaye ni mwimbaji, mtunzi na rapa, alizaliwa mwaka 1981 jijini Dar es Salaam. Alipata elimu ya msingi na sekondari lakini aliishia kidato cha pili mwaka 2004. Shughuli za muziki alianza tangu akiwa masomoni.

Alijiunga na bendi ya Jandaheka ya Bagamoyo na baadaye Less Bandu. Baada ya bendi hizo mbili alijiunga na Stone Musica 'Wajelajela Original'.

Baadaye akaenda Tanga kuanzisha bendi iliyojulikana kwa jina la Fax Jazz. Mambo hayakuwa mazuri, akajiunga na Sot Sound ya Dar es Salaam, baadaye akaenda Mchinga Sound ambako hakukaa sana, akajiunga na Twanga Pepeta, ambayo jana alitangaza rasmi kuachana nayo!

Ajiondoa Twanga

Wakati akitangaza kuiacha Twanga Pepeta leo, Chaz Baba alidai sasa ameamua kuwa mwanamuziki huru wa kujitegemea, na amejiondoa katika bendi hiyo kwa madai ya kukosa mkataba kwa muda mrefu.

Chaz Baba anasema ameamua kuchukua uamuzi huo kwa akili zake timamu kutokana na majukumu ya kifamilia aliyonayo.

Anasema alisaini mkataba wa mwaka mmoja wakati anajiunga na Twanga Pepeta mwaka 2005, lakini baada ya hapo alikuwa akipiga 'deiwaka' kwa kuitumikia bendi kwa mazoea bila ya kuwa na mkataba.

Twanga yakana

Hata hivyo, Meneja wa Twanga Pepeta, Hassan Rehani anasema Chaz Baba alisaini mkataba wa miaka mitano na bendi hiyo hivi karibuni, pia akalipiwa na kodi ya nyumba sh. milioni 2.5, na kwa vile hajafuata taratibu za kuuvunja, watawasilishwa malalamiko yao Mahakama ya Biashara kwa hatua za kisheria.

Rehani anasema wanajua kuna mipango ya chini chini inaendeshwa kuidhoofisha Twanga Pepeta, lakini anabainisha wanaofanya hivyo hawatafanikiwa, na bendi hiyo itazidi kusimama imara.

"Haiwezekani tangu mwaka 2005 Chaz Baba hajapewa mkataba... madai kwamba alikuwa akifanya kazi kama 'Deiwaka' kwa takriban miaka sita si ya kweli... huku ni kukosa fadhila, tena hakuna mwanamuziki aliyelelewa vyema kama Chaz Baba," anadokeza Rehani.

Bendi haitasambaratika

Rapa huyo aliyekuwa miongoni mwa waimbaji mahiri wa bendi hiyo, inawezekana kuondoka kwake likawa pigo kutokana na uhodari wake wa kuimba alipokuwa Twanga Pepeta.

Nyota huyo wa muziki wa dansi nchini anasema anachofanya sasa ni kufanya kazi kwa mikataba na si vinginevyo, hali ambayo itamsaidia kujua haki zake za msingi popote atakapohitajika.

Hata hivyo, mmoja wa wanamuziki wakongwe wa Twanga Pepeta anasema kuondoka kwa Chaz Baba si pengo kubwa, isipokuwa watamkosa kutokana na mazoea waliyokyuwa nayo kwake.

"Kuondoka kwa Chaz Baba hakutaisambaratisha Twanga Pepeta, isipkuwa mazoea tutamkosa kutokana na mazoea, lakini hali itarejea kama kawaida kama ilivyokuwa kwa Ramadhan Masanja 'Banza Stone', Ally Chocky na wengine.

"Hao wanaohangaika kuisambaratisha Twanga Pepeta bado hawajajua kilipo chanzo cha mizizi na shina... wanahangaika bure," anasema mwanamuziki huyo ambaye hakupenda kutajwa jina gazetini.

Anatoa mfano kuwa hata Jumatano iliyopita, Chaz Baba hakwenda kazini Billicanas, lakini mashabiki hawakuhisi kuona pengo lake, kwa vile wanamuziki wengi waliopo wanamudu kuimba sauti yake.

Ameahidiwa gari, mil 17/-

Meneja wa Chaz Baba, Bernard Msemwa, anasema siku chache zijazo, mwimbaji huyo atakwenda nje ya nchi kwa ajili ya mapumziko ya wiki moja ili ajipange upya katika tasnia hiyo ya muziki wa dansi.

Msemwa anaongeza kuwa mwanamuziki huyo yuko huru kujiunga na bendi yoyote ikiwemo Twanga ikiwa kutakuwepo na mkataba tofauti na ilivyokuwa awali.

Hata hivyo, habari kutoka ndani kwa wadau wa karibu na Chaz Baba zimedokeza kuwa msanii huyo ametangaza kuwa mwanamuziki huru kutokana na mipango iliyosukwa na mmiliki wa bendi ya Mashujaa, Hoseah Hopaje 'Maisha' ambaye ni Mhasibu Mkuu wa Shirika la Ndege la Oman 'Oman Air' akishirikiana na Chocky wa Extra Bongo.

Inadaiwa kuwa Maisha na mkewe, Mama Sakina, ambao ni washirika wakubwa wa Mkurugenzi wa ASET inayomiliki Twanga Pepeta, Asha Baraka, ndio wamesuka mipango ya kumng'oa Chaz Baba kwenye bendi hiyo, lengo likiwa ni kuhakikisha anatua Mashujaa ili kuuimarisha bendi hiyo, na ameahidiwa kupewa nafasi ya urais wa bendi.

"Maisha na Mama Sakina wametumia mwanya huo kumuondoa Chaz Baba Twanga Pepeta ili aonekane ni mwanamuziki huru, kisha muda mfupi ujao atatangaza kutua Extra Bongo inayoongozwa na Chocky, na baadaye atahamia Mashujaa.

Kibosho, Kanuti watakiwa

"Chaz Baba amewapa masharti ya kuondoka na baadhi ya wanamuziki Twanga Pepeta wakiwamo wapiga vyombo, Godfrey Kanuti, Hassan Kado, James Kibosho na wanenguaji Asha Said 'Sharapova' na Betty Mwangosi 'Baby Tall'," anadokeza mpasha habari ambaye hakupenda kutajwa jina lake gazetini.

Chanzo hicho cha habari kinadokeza kuwa Chaz Baba ambaye Jumatano usiku hakujumuika na wenzake kazini Billicanas, siku hiyo alikuwa Hoteli ya Holiday Inn ghorofa ya 10 akiwa na Maisha na washirika wake, ambapo alipewa donge nono la sh. milioni 17 na ahadi ya gari aina ya Noah ambalo ndilo ataondoka wakati wowote kuanzia wikiendi hii, kwenda Dubai kulichukua.

Maisha akana

Maisha ambaye awali alikuwa Mhasibu Mkuu wa Shirika la Ndege la Uholanzi (KLM), alipoulizwa kuhusu madai hayo alikanusha na kusema kuwa hahusiki kwa lolote.

"Si kweli kwamba nimehusika na mipango ya kumng'oa Chaz Baba Twanga Pepeta, ingawa Oktoba 2011 alinifuata kunishawishi kwamba ajiunge Mashujaa, lakini nilimkatalia na nikamwambia Asha Baraka habari hizo ili kama hana mkataba wamuandalie... kama ningekuwa na mpango huo nisingemwambia Asha, ningemchukua tangu wakati huo.

"Asha na kaka yake ambaye ni Mwenyekiti wa ASET, Baraka Msiilwa tuliwasiliana nao mapema na niliwaeleza habari za Chaz Baba... si kweli kwamba alikuwa akitakiwa Mashujaa.

"Hata hivyo, bado ana nafasi ya kurudi Twanga Pepeta wakifikia makubaliano na akapewa mkataba na waajiri wake wa zamani.

"Lakini pia hata sisi Mashujaa kama tunaweza kufikia makubaliano na Chaz Baba na ASET wakituruhusu, tunaweza kumchukua," anasema Maisha.

Hata hivyo, mmoja wa mameneja wa Twanga Pepeta, Martin Sospeter anasema mikataba ya wanamuziki wa bendi hiyo haina budi kuheshimiwa, na anamshangaa Chaz Baba kwa kukosa fadhila.

"Kuna wadau wa muziki wanaamini kuwa bila kuibomoa Twanga Pepeta bendi zao haziwezi kusimama imara, ndiyo maana wanahangaika usiku na mchana kuimaliza, lakini hawatafanikiwa asilani," anasema Sospeter.

Sospeter anadokeza kuwa hata wanamuziki wengine wanaotajwa kutaka kuondoka, Kibosho, Kanuti, Kado, Sharapova na Baby Tall, wote wana mikataba isiyopungua miaka mitatu kila mmoja, na anaamini kila mmoja ataheshimu hilo.

Kiongozi wa Twanga Pepeta, Luiza Mbutu anasema wanamtakia kila la heri Chaz Baba huko aendako, lakini akabainisha Twanga Pepeta ni chuo cha mafunzo ambacho waliondoka wanamuziki wengi nguli wakiwamo 'Banza Stone, Chocky na wengine, lakini kila kukicha inazidi kuimarika.

Ciao...

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATANZANIA WATAKAOVAA JEZI ZA MAMELODI AU AL AHLY

ALLY KAMWE AZIMIA KWA MKAPA.

RAIS SAMIA KUZINDUA MKUTANO MKUU WA 79 WA BARAZA LA MICHEZO YA MAJESHI DUNIANI

MIGINGO KISIWA KIDOGO ZAIDI AFRIKA KILICHOGOMBEWA NA UGANDA, KENYA