Madaktari bingwa kumfuata Pinda

MGOMO wa madaktari umeingia sura mpya baada ya madaktari bingwa wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), kuunda kamati ya watu watano itakayokutana na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
Hata hivyo, taarifa za ndani zimedai kuwa wamepanga kuipa Serikali saa 48 kutoa tamko litakalofanya wenzao warejee kazini vinginevyo nao watagoma.

Hatua hiyo ilifikiwa jana katika kikao cha dharura cha saa tatu kilichoitishwa na Mkurugenzi wa MNH, Dk Marina Njelekela kwa lengo la kukusanya maoni ya namna ya kufanya ili kulipatia ufumbuzi tatizo hilo.

Afisa Habari Mwandamizi wa MNH Aminael Aligaesha aliwaambia waandishi wa habari kwamba, madaktari hao bingwa wanataka kwenda kumuona Pinda ili wamweleze hali ilivyo na kumshauri namna ya kulipatia ufumbuzi suala hilo.
“Madaktari bingwa wanakwenda kumuona Waziri Mkuu ili kumweleza ukweli kuhusu hali ilivyo katika hospitali hii. Hali halisi ya Muhimbili inajulikana tangu kuanza mgomo kwani huduma zote za tiba zimezorota na madhara makubwa yametokea, ” alisema Aligaeshi.

Habari za ndani kutoka kwenye kikao zimedai kuwa madaktari hao pamoja na kumweleza waziri mkuu kuhusu hali halisi, wanatarajia kuwasilisha madai mbalimbali ikiwamo la mahitaji yao yatakayowezesha kuboresha huduma za afya na msimamo huo wa kutaka suluhu ili wenzao warudi kazini ndani ya saa 48.

Mmoja wa madaktari aliyehudhuria mkutano huo ambaye hakutaka kutajwa jina lake gazetini, alitaja mahitaji hayo kuwa ni vifaa vya kufanyia kazi, dawa na maslahi yao zikiwamo posho na stahiki nyingine.

“Waziri Mkuu Pinda ndiye aliyetoa tamko la kuwataka madaktari kurejea kazini mara moja huku akiwafuta kazi wasiorejea, sisi tunataka kwenda kumuona na kumweleza hali ilivyo hivi sasa kuwa ni mbaya, pia tunatarajia kumwasilishia madai yetu yote,” alisema daktari huyo.

Mkutano huo ni wa kwanza kuwahusisha madaktari bingwa tangu kuanza kwa mgomo huo Januari 23 mwaka huu na pia kutolewa kwa tamko la Waziri Mkuu Pinda Januari 29, ambalo liliwataka madaktari wote kurudi kazini na kutangaza kuwafuta kazi wote ambao wangekaidi.

Tangu kutolewa kwa tamko hilo la serikali hali ya utoaji huduma katika MNH na Taasisi ya Mifupa (MOI), imeendelea kuwa mbaya na kusababisha athari kwa wagonjwa ikiwemo vifo.

Tughe yatoa tamko
Wakati mgomo huo ukizidi kutikisa hospitali kuu nchini, Chama cha Wafanyakazi wa Serikali Kuu na Afya (Tughe) jana kimetoa tamko la kuitaka serikali kukutana na kamati teule ya madaktari na wauguzi haraka iwezekanavyo ili kunusuru maisha ya watanzania.

Naibu Katibu Mkuu wa Tughe Taifa, John Sanjo aliwaambia waandishi wa habari katika hospitali ya Muhimbili kwamba, mgomo huo una madhara makubwa kwa jamii na wanaoathirika ni wananchi wa kipato cha chini.
“Tughe inaunga mkono madai yote ya madaktari na wafanya kazi wote wa sekta ya afya kwa sababu madai hayo ni haki yao ya msingi,” alisema Sanjo na kuongeza:

“Chama kinataka serikali kuanza mazungumzo na Kamati Teuli ya Madaktari haraka iwezekanavyo na mara mazungumzo hayo yatakapoanza, chama kinawaomba madaktari walio kwenye mgomo kurejea kazini.”

Serikali yakwama
Katika hatua nyingine, ahadi ya waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dk Hadji Mponda kuwa angepeleka madaktari 80 kutoka wizarani kwake ili kuongeza nguvu MNH na MOI, imekwama baada ya uongozi wa hospitali hiyo kuthibitisha kwamba, hadi jana hakuna daktari aliyeletwa.

Msemaji wa hospitali MNH, Aligaeshi aliwaambia waandishi wa habari kwamba, hadi jana madaktari walioripoti ni15 ambao ni kutoka Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).

Juzi, Waziri Mponda aliwaambia waandishi wa habari kuwa wizara imeamua kuwapeleka madaktari 80 katika hospitali hiyo kutoka wizarani, ili washirikiane na wa JWTZ kutoa tiba katika hospitali hiyo.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATANZANIA WATAKAOVAA JEZI ZA MAMELODI AU AL AHLY

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KOCHA BENCHIKHA AMESEPA

MASHUSHUSHU WA MAMELODI WALIKUJA KUTUPELELEZA: HERSI

KOCHA WA AL.AHLY ASEMA YANGA NI TIMU BORA NA NGUMU