TANZANIA NA CHINA ZAKUBALIANA KUBORESHA RELI YA TAZARA

TANZANIA na China zimekubaliana kuikarabati, kuifufua, kuiimarisha na kuifanya ya kisasa zaidi Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA) kwa haraka iwezekanavyo ili kuiwezesha reli hiyo kutoa mchango mkubwa zaidi katika chumi za nchi za Tanzania na Zambia.
Uimarishaji wa Reli ya Tazara ikiwa ni pamoja na kuboresha menejimenti na uongozi wake ni jambo lililotawala mazungumzo kati ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete na Naibu Waziri wa Biashara wa Jamhuri ya Watu wa China, Mheshimiwa Li Jinzao yaliyofanyika Ikulu, Dar es Salaam, leo, Ijumaa, Machi 23, 2012.
Mheshimiwa Jinzao ambaye aliwasili nchini jana kwa ziara ya siku nne amemwambia Rais Kikwete kuwa China iko tayari kugharamia ufufuaji, ukarabati, uimarishaji na hatua zote za kuifanya ya kisasa zaidi reli hiyo kati ya Tanzania na Zambia iliyojengwa katika miaka ya 1970 kwa msaada kutoka China.
Wakati inajengwa, reli ya TAZARA ndio ulikuwa mradi mkubwa zaidi kugharimiwa na Jamhuri ya Watu wa China nje ya nchi hiyo, na reli hiyo iliendelea kushikilia nafasi hiyo hadi majuzi wakati China ilipogharimia ujenzi wa Makao Makuu wa Umoja wa Afrika (AU) mjini Addis Ababa, Ethiopia.
Mheshimiwa Jinzao amemweleza Rais Kikwete kuhusu mapendekezo maalum na mahsusi ya nchi yake ya jinsi ya kuimarisha na kuiboresha reli hiyo ambayo katika miaka ya karibuni imekabiliwa na matatizo kadhaa yaliwemo ya menejimenti, ya kifedha, ya operesheni na ufundi.
Rais kikwete amekubali kuwa mwenyekiti wa kikosikazi maalum cha kusimamia uimarishaji na uboreshaji wa reli hiyo “ili mradi tuhakikishe kuwa reli hiyo inafufuliwa na kufanya kazi kama ilivyokusudiwa kwa sababu ni dhahiri kuwa kwa sasa TAZARA ni mgonjwa ambaye anahitaji matibabu ya uangalizi wa karibu.”
Viongozi hao wawili pia wamejadili maeneo mengine ya uhusiano na ushirikiano kati ya nchi hizo mbili na Rais Kikwete ameishukuru China kwa misaada yake katika maeneo mengine ya maendeleo.
Miongoni mwa maeneo hayo ni pamoja na China kukubali kutoa fedha za mkopo wa ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam na kutoa mkopo unaoiwezesha Tanzania kutandaza mkongo wa mawasiliano wa taifa nchi nzima.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

HATUTOPAKI BASI DHIDI YA YANGA-MOKWENA

“PEMBA SALUTI KWENU” DK. NCHIMBI*

DKT NCHIMBI AWAAHIDI MAKUBWA WANANCHI WA KWELA, RUKWA