KWELI SIMBA NI KIBOKO


  
WEKUNDU wa Msimbazi, Simba, ya jijini Dar es Salaam, jana iliendelea kudhihirisha umwamba wake katika michuano ya kimataifa, baada ya kuichapa Al Ahli Shendi ya Sudan kwa mabao 3-0 katika mechi ya kwanza hatua ya 16 bora ya Kombe la Shirikisho Afrika (CAF).

Mechi hiyo iliyopigwa kwenye Uwanja wa Taifa chini ya mwamuzi Nheleko Simanga, ilishuhudia kiungo Patyrick Mafisango akipoteza mkwaju wa penalti dakika ya 39, uliokuja baada ya mshambuliaji Emmanuel Okwi kufanyiwa madhambi ndani ya eneo la hatari na mlinda mlango wa Shendi Abdelrahman Ali kupangua.

Kabla ya penalti hiyo, Simba kupitia wakali wake kadhaa ilikosa nafasi za wazi kufunga mabao, zikiwamo zile za dakika ya 13 ambapo Felix Sunzu alishindwa kuitendea haki pasi ya Okwi, kabla ya Okwi naye kushindwa kufunga dakika ya 32, huku Shendi nao wakikosa bao dakika ya 19 kwa kipa wa Simba Juma Kaseja kuokoa shuti la wazi.

Hadi mapumziko, timu hizo zilitoka kwa sare ya 0-0, licha ya Mnyama kupoteza nafasi nyingi ambazo kama si ushindi wa kipindi cha pili, zingewafanya wajutie kupoteza nafasi hizo.

Kipindi cha pili Simba ilikuja juu na mnamo dakika ya 66, Haruna Moshi Boban akaipatia timu hiyo bao la kwanza, akimalizia kazi nzuri ya Sunzu na kuwainua mashabiki wao vitini. Dakika ya 77, Mafisango alifuta makosa ya awali kwa kuifungia Simba bao la pili akipokea pasi kutoka kwa Okwi.

Okwi akahitimisha kichapo hicho kwa kuipatia Simba bao la tatu dakika ya 87, bao lililotokana na pasi ya Mafisango na kuwanyanyua mashabiki wachache wa Yanga uwanjani hapo kuelekea makwao wakionekana dhahiri kutofurahishwa na matokeo hayo.

Hadi pambano linamalizika Simba ilitoka uwanjani hapo na ushindi huo ambapo Mafisango alikuwa ameelemewa na uchungu wa kupoteza penalti na kujikuta akilia.

Akizungumza baada ya kumalizika kwa mechi hiyo, aliyekuwa mgeni rasmi, Frederick Sumaye, aliwapongeza Wekundu hao kwa upiganaji uliozaa ushindi huo na kuwataka kuongeza juhudi ili kufika mbali zaidi.

Aliongeza kwa kuwaahidi kuwapa ushirikiano mkubwa na kwamba kama watamhitaji kwa safari ya Khartoum Sudan wiki mbili zijazo yuko tayari kuambatana nao huko ili kumaliza kazi iliyobaki.

Vikosi: Simba; Juma Kaseja, Nasoro Cholo, Amir Maftah, Shomari Kapombe, Kevin Yondani, Patrick Mafisango, Uhuru Suleiman, Mwinyi Kazimoto, Felix Sunzu, Haruna Moshi ‘Boban’ na Emmanuel Okwi.

Shendi; Abdelrahman Ali, Elnour Eltigan, Issac Malikh, Sadam Talib, Fareed Mohamed, Zakaria Nasu, Razak Yakub, Faris Abdallah, Hamouda Bashir, Nadir Altaues na Basiro Obamba.


 

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

DKT NCHIMBI AWAAHIDI MAKUBWA WANANCHI WA KWELA, RUKWA

DK NCHIMBI ATINGA MKOANI KATAVI

BASHASHA LATAWALA NCHIMBI ALIPOLAKIWA NA CHONGOLO SONGWE

MONGELLA AKABIDHIWA ‘MIKOBA’ RASMI YA NAIBU KATIBU MKUU CCM BARA*

NCHIMBI AFUNGUA KONGAMANO LA MAADHIMISHO YA KUMBUKIZI YA MWALIMU NYERERE

MAKALLA ASHANGILIWA BUNGENI