CHELSEA YAIBANJUA ARSENAL 2-1 DARAJANI
Nyota waliochukuliwa kama kielelezo cha upinzani wa mechi ya London
Derby kati ya Chelsea na Arsenal jana kwenye Uwanja wa Stamford Bridge.
Kushoto ni Demba Ba wa Chelsea, kulia ni Jack Wilishere wa Arsenal.
Vita dimbani ikawa hivi, haikuwa lelemama hata kidogo kwa dakika zote
90 za mpambano huo Darajani. Beki wa Gunners, Francis Coquelin kushoto
akichuana na Fernando Torres wa Chelsea.
Frank Lampard kulia akishangilia baada ya kufunga kwa mkwaju wa penati,
iliyotolewa na mwamuzi Martin Atkinson, baada ya kipa wa Gunners,
Wojciech Szczesny kumwangusha Ramires ndani ya boksi.
Hapa 'Winga Teleza' Theo Walcott wa Arsenal kulia akiifungia timu yake
bao la kufutia machozi, huku jitihada za beki Branislav Ivanovic kushoto
kuzuia Walcott aasimtungue mlinda mlango Petr Cech, zikigonga mwamba
Kiungo Jack Wilshere wa Arsenal kushoto, akiungana kushangilia na
Walcott baada ya kufunga bao la kufutia machozi kwa Washika Bunduki.
Soka sio lelemama. Ndivyo unavyoweza kusema pindi unaposhuhudia mtifuano
kama huu kwenye dimba lolote. Hii ilikuwa moja ya hekaheka tu za
pambano hilo, ikimuhusisha Torres kama anavyoonekana.
LONDON,
England
MABAO mawili yaliyowekwa nyavuni na viungo Juan Mata na
Frank Lampard, jana yaliipa Chelsea ushindi wa
2-1 dhidi ya Arsenal, katika pambano kali la Ligi Kuu la mahasimu wa jiji la London, kwenye dimba la Stamford Bridge.
Mata aliifungia Chelsea bao
la uongozi, wakati shambulizi tata lilipoonesha kama
beki Francis Coquelin wa Arsenal akimchezea rafu Ramires, kisha mpira kumfikia Oscar
aliyetoa pasi maridadi kwa Mata liyemtungua mlinda mlango Wojciech Szczesny.
Kuingia kwa bao hilo kuliwapa
ujasiri mkubwa Chelsea,
huku Gunners wakionekana kupoteana, ambapo dakika ya 15 kipa Szczesny
alimwangusha Ramires ndani ya boksi na mwamuzi Martin Atkinson kumpa kadi ya
njano huku akiamuru ipigwe penati.
Lampard aliipiga kwa ustadi penati hiyo, kuipa Chelsea bao la pili
lililowapeleka mapumziko wakiwa mbele kwa matokeo ya 2-0.
Kipindi cha pili kilianza kwa Arsenal kupigania kusawazisha
mabao hayo, juhudi zilizoanza kupata mafanikio baada ya Theo Walcott kuifungia
bao la kufutia machozi.
Walcott alifunga bao hilo
dakika ya 58 kwenye kona ya kulia ya lango na kumshinda kipa Petr Cech, baada
ya kupokea pasi maridadi kutoka kwa Santi Cazorla.
Kwa ushindi huo Chelsea
imebaki katika nafasi ya tatu ya msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na pointi 45, huku
Gunners nayo ikisalia nafasi ya sita na pointi zao 34, pointi 21 nyuma ya
vinara Manchester United ambao walikuwa wakicheza na Tottenham jana usiku.
Chelsea; Cech, Azpilicueta, Cahill, Ivanovic, Cole, Ramires,
Lampard, Oscar/ Bertrand, Hazard/Marko Marin, Mata, Torres/Demba Ba.
Comments