WADAU wa elimu nchini Tanzania
wanaamini kwa kiasi kikubwa kwamba endapo elimu ya awali (chekechea)
nchini Tanzania itatolewa katika misingi inayostahiki itakuwa ni njia
moja wapo madhubuti ya kuimarisha ubora wa elimu. Hii ndiyo maana
wanaendelea kupaza sauti wakiitaka serikali kupitia vyombo husika
kuboresha kwanza elimu ya awali kabla ya kupanda ngazi nyingine za juu.
Huenda kilio hiki cha wadau wa
elimu kimeanza kusikika serikalini. Kwani tayari Wizara ya Elimu na
Mafunzo ya Ufundi iliagiza tangu mwaka 2010 kuwa kila shule zake za
msingi ni lazima lianzishwe darasa la awali ili kuwenza kuwaandaa
wanafunzi kuingia na darasa la kwanza. Awali elimu hii ilikuwa ikitolewa
kwa kiasi kikubwa na taasisi na vikundi mbalimbali na hata watu binafsi
nje ya shule za msingi, tena kwa hiyari. Kwa sasa sera na miongozo ya
elimu inatamka wazi kuwa nilazima kila shule ya msingi iwe na darasa la
awali kwa ajili ya elimu hiyo muhimu.
Changamoto kubwa iliyoibuka kwa
sasa baada ya utekelezaji wa agizo hilo ni namna elimu hiyo
inavyoendeshwa kwa kusuasua kwenye baadhi ya shule za Serikali. Hivi
karibuni mwandishi wa makala haya alitembelea baadhi ya shule za msingi
zilizopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru kuangalia hali ya
utekelezaji wa zoezi hilo.
Uchunguzi ulibaini zipo shule
ambazo licha ya kusajili wanafunzi wa awali kila mwaka hazina madarasa
ya kusomea kwa watoto hao, hali ambayo inafanya wanafunzi hao wadogo
kufundishwa katika mazingira magumu na kudhohofisha lengo zima la utoaji
wa elimu hiyo. Wapo wanafunzi ambao hulazimika kufundishiwa nje, yaani
chini ya mti ama kwenye magofu (majengo ya shule ambayo hayajakamilika)
iwe madarasa au nyumba za walimu.
Teckla Milanzi ni mwalimu wa
darasa la awali, Shule ya Msingi Nakayaya. Anasema kimsingi wanafunzi wa
darasa la awali shuleni hapo wanasomea chini ya mti kwa kuwa hawana
darasa maalum kwa wanafunzi hao. Anasema wakati wa mvua ama jua kali
mara nyingine hulazimika kuhairisha masomo kwa siku kutokana na hali ya
hewa.
Anasema anashukuru kwa sasa
wanajihifadhi kwenye jengo moja ambalo linaendelea na ujenzi shuleni
hapo, jengo ambalo hata hivyo mara baada ya ujenzi kukamilika na
wahusika kukabidhiwa darasa watarudi kusomea chini ya mti kama ilivyo
ada. Hata hivyo, anasema licha ya changamoto hiyo darasa hilo halina
vitabu kwa ajili ya kufundishia wanafunzi, bali kuna nakala moja moja
kwa baadhi ya masomo ambavyo vilitafutwa kwa jitihada za mwalimu
mwenyewe.
“Mfano kwa vitabu vya Kiswahili,
Kiingereza, Sayansi na Hisabati kuna nakala moja moja tu, ambazo
hutumiwa na mwalimu mwenyewe. Anasema darasa hilo licha ya kuwa na
changamoto kedekede hata kwenye mgao wa fedha zinazoletwa shuleni kila
mara halimo hivyo hakuna kinacholetwa tofauti na wanafunzi wengine,”
anasema Bi. Teckla Milanzi.
Kwa upande wake, Mwalimu Christina
Komba wa darasa la awali Shule ya Msingi Tunduru Mchanganyiko anasema
madarasa ya elimu ya awali Wilayani Tunduru yanakabiliwa na changamoto
nyingi. Anabainisha kuwa madarasa mengi likiwemo lake hawana vitabu wala
miongozo ya namna ya ufundishaji kabisa zaidi ya kila mwalimu
anayefundisha kubuni nini afundishe kila uchao.
“…Kwanza licha ya kutokuwa na
vifaa vingine hatuna chumba maalumu cha wanafunzi hawa (darasa) kwa sasa
tunatumia jengo la darasa ambalo bado linaendelea na ujenzi na hata
hivyo jengo hili halijengwi kwa ajili ya wanafunzi wa awali,” anasema
mwalimu Christina Komba.
“Madarasa ya elimu ya awali hayana
vitabu, hayana miongozo…huwa tunaanzima au ukipata hela yako wewe
binafsi unaenda kununua kitabu kimoja au viwili ili uweze kuwasaidia
watoto. Na baadhi ya masomo hayana vitabu kabisa hata ukienda madukani
katika Wilaya yetu (Wilaya ya Tunduru) vitabu kama Haiba na Michezo,
pamoja na Sanaa hazipo kabisa madukani. Anasema uongozi wa juu wilayani
unalitambua hilo.
Comments