Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt Dotto Biteko, ametoa onyo kali kwa Shirika la Umeme Tanzania TANESCO kufuatia kusuasua kwa Mradi wa Ujenzi wa Njia ya Kusafirisha Umeme wa msongo wa kilovoti 400 kutoka Chalinze hadi Dodoma.
Akizungumza alipokuwa ametembelea mradi huo Leo Agosti 20, 2025, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema kuwa mradi huo wa kusafirisha umeme kutoka Chalinze Hadi Dodoma umefikia asilimia 24 pekee badala ya asilimia 31 iliyopangwa kufikia Tangu mradi huo ulipozinduliwa.
Pia,Naibu waziri Mkuu Dkt. Biteko amesema kuwa kusuasua kwa mradi huo kunahatarisha mpango wa taifa wa kuunganisha umeme kutoka Bwawa la Kufua Umeme la Mwalimu Julius Nyerere kwenda mikoa mbalimbali nchini.
Tusizuie miradi hii, kwa sababu viwanda na wananchi wanahitaji umeme wa uhakika. Tunaongeza vyanzo vingine vya umeme kwenye gridi ya Taifa ili kuhakikisha nchi inakuwa na umeme wa kutosha kwa maendeleo ya viwanda na huduma za kijamii,” amesisitiza.
Pia Dkt. Biteko amewaomba wananchi wa Manchali na Dodoma kwa ujumla kushirikiana na Serikali na kujitokeza kwa wingi katika mikutano ya kampeni mwaka huu, akisisitiza umuhimu wa kuchagua viongozi wanaoeleza yale waliyoyatekeleza badala ya matamanio pekee” Amesema
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Bi. Rosemary Senyamule, amesisitiza kuwa serikali ya mkoa huo itahakikisha mradi huo unasimamiwa kikamilifu hadi kukamilika.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TANESCO Lazaro Twange, ameahidi kushughulikia mapungufu yote yaliyochangia kuchelewesha utekelezaji wa mradi huo.
Aidha, Baadhi ya wananchi wa kijiji cha Manchali, ambapo mradi huo unatekelezwa, wametoa maoni yao wakiiomba serikali kuharakisha mradi huo ili waweze kupata huduma ya umeme mapema.
Nasson Tunjeletona, Mkazi wa Manchal , amesema kuwa Mradi wa Chalinze Dodoma unatajwa kuwa kiunganishi muhimu katika usafirishaji wa umeme wa uhakika kutoka mradi wa Bwawa la Nyerere, hatua inayotarajiwa kuchochea maendeleo ya viwanda na uchumi wa taifa.
Comments