Mbunge wa jimbo la Kalenga Bw Godfrey Mgimwa akizungumza na wanafunzi wa shule ya sekondari Ifunda Tech
Picha na habari na Francis Godwin Blog
UONGOZI wa shule ya sekondari ya Ifunda Teck sec School umempongeza mbunge wa jimbo la kalenga Bw Godfrey Mgimwa kwa kutekeleza ahadi yake ya fedha taslim kiasi cha Tsh milioni 2 kwa ajili ya kusaidia ununuzi wa mashine ya Printa katika shule .
Mkuu wa shule hiyo Maddy Kissuo alitoa pongezi hiyo jana mbele ya mbunge Mgimwa baada ya kupokea msaada huo wa Tsh milioni 2 zilizoombwa na uongozi wa shule hiyo mwanzoni mwa mwaka huu wakati wa mahafali ya kidato cha sita .
Alisema kuwa mbunge huyo ameonyesha mfano wa kuigwa na viongozi wengine katika kutekeleza ahadi zao kwa wakati na kuwa bila msaada huo uwezekano wa shule hiyo kupata fedha za kununua mashine hiyo ulikuwa mgumu zaidi hasa ukizingatia na hali ya uchumi wa sasa shuleni hapo.
"Jitihada hizi za mbunge kutusaidia mashine hii ya printa ni kubwa sana na kuifanya shule hiyo kwa sasa kuwa na uhakika wa kuchapa mitihani mbali mbali na kuiprinti hapo hapo shuleni tofauti na awali tulivyokuwa tukisafiri hadi mjini Iringa umbali wa kilomita zaidi ya 50 kwenda kuprinti mitihani ....kweli tunakuombea zaidi na zaidi ili uzidi kuendelea kuwatumikia wananchi wa kalenga "alisema
Huku Mbunge Mgimwa akidai kuwa amelazimika kuomba ruhusa mara moja ya siku moja bungeni Dodoma ili kurudi jimboni kutimiza ahadi yake hiyo ambayo alikuwa ameahidi kuitimiza ndani ya mwezi huu wa Septemba.
Akizungumza na wanafunzi wa shule ya sekondari Ifunda baada ya kukabidhi msaada huo alisema kuwa amelazimika kutekeleza ahadi hiyo ya fedha za kununua mashine ya kuprinti mitihani shu;leni hapo kama ambavyo uongozi wa shule hiyo ulivyomuomba wakati wa mahafali ya kidato cha sita shuleni hapo mwaka huu.
Hivyo alisema isingependeza kama ahadi hiyo ingeendelea kuchelewa kutolewa shuleni hapo hasa ukizingatia kuwa mashine hiyo ina mchango mkubwa katika maendeleo ya taalum shuleni hapo.
Kwani alisema kuwa shule kama hiyo kukosa mashine kama hiyo ni aibu kubwa na ni mwanzo wa taalum shuleni hapo kushuka kwa walimu kupoteza muda kwenda mjini zaidi ya kilometa 50 kutoka shuleni hapo kwenda kupata huduma hiyo ya mashine ya kuprinti mitihani ya wanafunzi .
Alisema kuwa wakati yeye kama mbunge anatimiza ahadi yake katika shule hiyo kwa ajili ya wanafunzi hao ni vema kwa upande wao wanafunzi kuendelea kudumisha nidham na kujituma zaidi katika masomo ili ikiwezekano shule hiyo kujakutoa kiongozi bora wa nchi mbeleni.
" Nawaombeni sana wanafunzi someni kwa bidii na epukeni sana vurugu zisizo na maana katika maisha yenu .....mimi kama mbunge wajibu wangu kwenu ni kuwawakilisha bungeni ila pia kuwa karibu na shule yenu hii pale mnapokwama mimi nipo tayari kuwasaidia"
Pia alisema mategemeo yake kuona shule zake katika jimbo la kalenga zinaendelea kufanya vema katika mitihani mbali mbali ya kitaifa ili ikiwezekano jimbo la kalenga kuwa kitovu cha elimu kwa mkoa wa Iringa .
|
Comments