RAIS KIKWETE AONGOZA MAZISHI YA CHIFU MKWAWA IRINGA LEO

 Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiwa na  Chifu mpya wa
Wahehe, Chifu Adam Abdu Mkwawa, Mtwa Adam wa Pili (14), wakati wa
mazishi ya baba yake aliyekuwa Chifu wa Kabila la Wahehe, Chifu Abdu
Mfwimi Adam Mkwawa leo  katika eneo la Nyumba ya Makumbusho ya Chifu
Mkwawa, Kijiji cha Karenga Februari 16, 2015.



 Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiweka udongo kaburini wakati wa
mazishi ya aliyekuwa Chifu wa Kabila la Wahehe, Chifu Abdu Mfwimi Adam
Mkwawa leo  katika eneo la Nyumba ya Makumbusho ya Chifu Mkwawa,
Kijiji cha Karenga Februari 16, 2015.
 Rais Jakaya Mrisho Kikwete akimfariji  Chifu mpya wa
Wahehe, Chifu Adam Abdu Mkwawa, Mtwa Adam wa Pili (14), wakati wa
mazishi ya baba yake aliyekuwa Chifu wa Kabila la Wahehe, Chifu Abdu
Mfwimi Adam Mkwawa  katika eneo la Nyumba ya Makumbusho ya Chifu
Mkwawa, Kijiji cha Karenga  leo Februari 16, 2015


 JK akitia saini kwenye kitabu cha maombolezao ya chifu
 Rais Jakaya Mrisho Kikwete akimpa pole mjane wa aliyekuwa Chifu
wa Kabila la Wahehe, Chifu Abdu Mfwimi Adam Mkwawa leo  Kijiji cha
Karenga Februari 16, 2015.



TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete leo, Jumatatu, Februari 16, 2015, ameungana na mamia ya waombolezaji kumlaza katika nyumba yake ya milele, Chifu wa Kabila la Wahehe, Chifu Abdu Mfwimi Adam Mkwawa.
Aidha, Rais Kikwete ameshuhudia kutawazwa kwa Chifu mpya, Chifu Adam Abdu Mkwawa, Mtwa Adam wa Pili, kijana wa miaka 14, ambaye yuko darasa la saba na ambaye anachukua nafasi ya baba yake ambaye aliaga dunia juzi, Jumamosi, Februari 14, 2015.
Mtwa Adam wa Pili ni mtoto pekee wa kiume na pia ni mtoto sita na wa mwisho wa Chifu Abdu Adam Mkwawa ambaye ameaga dunia akiwa na umri wa miaka 65.
Rais Kikwete amewasili katika eneo la Nyumba ya Makumbusho ya Chifu Mkwawa, Kijiji cha Karenga, kiasi cha saa saba kujiunga na mamia ya waombolezaji na kushuhudia kutawazwa kwa Mtwa Adam wa Pili, ambaye amekuwa chifu kwa kupewa mkuki na ngao, ambavyo vilitumiwa na Chifu Mkwawa mwenyewe, na baadaye kukalishwa kwenye kiti cha uchifu.
Kwa vile hajafikisha umri wa miaka 20 ambao ndio umri rasmi wa kuwa Chifu wa Wahehe, ameapishwa pia chifu wa muda, Chifu Hassan Adam Sapi (Mahinya), ambaye atashikilia kiti cha uchifu kwa niaba ya Mtwa Adam wa Pili, mpaka hapo atakapofikisha umri wa miaka 20, miaka sita kutoka sasa.
Wakati mmoja wakati wa sherehe ya kutawazwa, Rais Kikwete amelazimika kumbembeleza na kumtuliza Mtwa Adam Abdu Mkwawa, ambaye alizidiwa na hisia na kuanza kubujikwa na machozi.
Baada ya kutawazwa kwa chifu mpya, yameanza mazishi ya chifu aliyeaga dunia ambaye amezikwa kwa heshima na taratibu zote za dini ya Kiislam lakini pia akapigiwa risasi tatu kwa kutumia gobole kwa mujibu wa mila na tamaduni za Kabila la Wahehe.
Baada ya kumalizika kwa mazishi ya Marehemu Chifu Abdu Mfwimi Adam Mkwawa, Rais Kikwete amekwenda nyumbani kwa marehemu kutoa pole kwa wafiwa akiwemo mama mjane.
Rais Kikwete amewasili Mkoani Iringa asubuhi ya leo, akitokea Dar es Salaam, ambako anafanya ziara ya kikazi ya siku mbili. Rais Kikwete ataondoka Iringa kesho, Jumanne, Februari 17, kurejea Dar es Salaam.

Ends
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.

16 Februari, 2015

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

WAZIRI BASHE APIGA MARUFUKU WASIOSOMEA KILIMO KUUZA PEMBEJEO

BREAKING: CAF YAIPOKONYA KENYA KUANDAA CHAN

BREAKING NEWSSSS. WABUNGE WAPATA AJALI