WAZIRI KIJAJI: WATAKAOPANDISHA BEI ZA BIDHAA KIHOLELA WATACHUKULIWA HATUA

 

                                         
Waziri wa Uwekezaji, Biashara na Viwanda, Dkt. Ashatu Kijaji akizungumza na vyombo vya habari jijini Dodoma Agosti 15, kuhusu tathmini ya mwenendo wa bei ya bidhaa bidhaa muhimu nchini na hatua mbalimbali zilizochukuliwa na serikali kupunguza mfumuko wa bei.
Baadhi ya wanahabari wakiwa katika mkutano huo.


Baadhi ya maafisa wa serikali na wanahabari wakifuatilia kichozungumzwa na waziri katika mkutano huo.

PICHA ZOTE NA RICHARD MWAIKENDA

Mdau, nakuomba uendelee kusoma taarifa kamili hapo chini iliyotolewa na Waziri Dkt Kijaji...

TAARIFA KWA UMMA

_________________________________________________

 

TATHMINI YA MWENENDO WA BEI YA BIDHAA MUHIMU NCHINI

 

15/08/2021, DODOMA

 

1. UTANGULIZI

 

Ndugu Waandishi wa Habari;

Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara inashirikiana na Tume ya Ushindani (FCC) na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kutekeleza jukumu la kufuatilia na kufanya tathmini ya mwenendo wa bei za bidhaa muhimu nchini. Lengo la tathmini hiyo ni kumlinda mlaji kwa kuhakikisha anapata bidhaa bora kwa bei stahiki na kuzuia upandishwaji holela wa bei za bidhaa mbalimbali; pamoja na kuchukua hatua za kisheria kwa yeyote atakayebainika kupandisha bei za bidhaa kiholela bila kuzingatia gharama halisi za uzalishaji au uingizaji nchini wa bidhaa husika.

 

Matokeo ya tathmini zilizofanyika hivi karibuni yalionesha kuwa kuna uhimilivu mkubwa wa bei (price stability) kwa bidhaa zinazozalishwa hapa nchini, ambazo zilionesha ongezeko dogo la bei ikilinganishwa na bidhaa zinazoagizwa kutoka nje ya nchi ambazo zilionesha ongezeko kubwa zaidi la bei.

 

 

Ndugu Waandishi wa Habari;

Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imefanya jitihada kubwa za kuweka mazingira rafiki ya ufanyaji biashara nchini, kwa kuchukua hatua mbalimbali katika kudhibiti ongezeko la bei za bidhaa ikiwa ni pamoja na udhibiti wa upandishwaji holela wa bei. Kutokana na jitihada hizo, bei za bidhaa kwenye soko la ndani zimeendelea kuwa na utulivu huku bei za baadhi ya bidhaa hususan zinazotegemea malighafi kutoka nje ya nchi zikiongezeka kutokana na kupanda kwa bei za malighafi katika soko la dunia na gharama kubwa za usafirishaji. Hatua zilizochukuliwa na Serikali ni pamoja na kuimarisha uzalishaji wa ndani wa bidhaa mbalimbali ili kupunguza utegemezi wa kuagiza mahitaji muhimu kama vile vyakula kutoka nje ya nchi. Aidha, bei za baadhi ya bidhaa zimepanda kutokana na kupanda kwa bei ya nishati hasa mafuta ya petroli kwenye soko la dunia.

 

 

 

Ndugu Waandishi wa Habari;

Serikali inaendelea kuchukua hatua mbali mbali kwa lengo la kuwapunguzia Wananchi athari zitokanazo na kupanda kwa bei za bidhaa muhimu. Hatua hizo ni pamoja na kuwapunguzia gharama za uzalishaji au uagizaji na usambazaji wa bidhaa ili kuleta uhimilivu wa bei (price stability) kwenye soko. Hatua zilizochukuliwa na Serikali zimelenga kupunguza athari za mtikisiko wa uchumi duniani uliosababishwa na janga la UVIKO-19 na vita kati ya nchi za Urusi na Ukraine.

 

Baadhi ya hatua zilizochukuliwa na Serikali kupitia Bajeti Kuu ya Serikali ya mwaka wa fedha 2022/2023 na Sheria ya Fedha ya mwaka 2022 ni pamoja na hizi zifuatazo:

 

i)                 Serikali imeondoa (zero rate) Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwa wazalishaji wa ndani wa mafuta ya kupikia yaliyosafishwa (double refined edible oil) kwa kipindi cha mwaka mmoja kwa lengo la kupunguza gharama za uzalishaji wa bidhaa hiyo nchini na hivyo kuleta unafuu wa bei za mafuta ya kupikia kwa mlaji wa mwisho. Hatua hii imeanza kuonesha mafanikio kwani mwenendo wa bei ya mafuta ya kupikia unaonesha bei hizo zimeanza kushuka. Serikali pia inaendelea na jitihada za kuhamasisha uzalishaji wa mbegu za mafuta ya kupikia nchini hasa alizeti na chikichi kwa lengo la kujitosheleza kwa mahitaji yetu na kuuza ziada nchi jirani.

ii)               Serikali imeondoa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwa wazalishaji wa mbolea kwa kipindi cha mwaka mmoja ili kuwapunguzia wakulima gharama za uzalishaji na hivyo kuleta unafuu wa bei za mazao muhimu ya chakula.

iii)              Sheria ya Fedha ya mwaka 2022 pia imempa Waziri wa Fedha mamlaka ya kusamehe Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwa Wawekezaji Mahiri hususan watakao wekeza kwenye ujenzi wa viwanda kwa ajili ya kupunguza utegemezi wa nchi wa kuagiza bidhaa muhimu kutoka nje. Hatua hii ni ya kuweka uwiano kati ya Sheria ya VAT na Sheria ya Uwekezaji ili kuweka mazingira yanayotabirika kwa Wawekezaji, kuvutia uwekezaji, kuongeza uzalishaji wa ndani na hivyo kuleta uhimilivu wa bei.

iv)             Serikali imeanza kutoza ushuru wa asilimia 30 au Dola za Marekani 150 kwa Tani kwenye usafirishaji wa bidhaa za shaba na chuma chakavu nje ya nchi kwa lengo la kuwalinda wazalishaji wa ndani wa bidhaa za chuma, kwa kuwahakikishia upatikanaji wa malighafi za kutosha na hivyo kuleta unafuu wa bei za bidhaa za chuma hasa nondo kwenye soko la ndani.

v)               Serikali imepunguza ushuru kwa malori yanayosafirisha bidhaa (transit charges) kutoka Dola za Marekani 16 kwa kila kilomita 100 hadi Dola za Marekani 10 kwa kila kilomita 100 ili kupunguza gharama za usafirishaji wa bidhaa nchini na hivyo kuleta unafuu wa bei za bidhaa hizo.

vi)             Serikali imepunguza kiwango cha ushuru wa forodha kutoka asilimia 35 hadi asilimia 10 kwa waagizaji wa ngano ili kuwapunguzia gharama wazalishaji wa ndani wa unga wa ngano na hivyo kuleta unafuu wa bei ya unga wa ngano kwenye soko la ndani.

vii)            Serikali pia imeondoa ushuru wa forodha kwa kutoza kiwango cha asilimia sifuri (0%) badala ya asilimia 10 kwenye malighafi za utengenezaji wa sabuni (RBD Palm Stearin) kwa lengo la kuhamasisha na kupunguza gharama za wazalishaji wa ndani wa sabuni ili kudhibiti ongezeko la bei ya sabuni.

viii)          Serikali imeongeza kiwango cha juu cha ushuru wa forodha kwa bidhaa mbalimbali zinazozalishwa na viwanda vya ndani kutoka asilimia 25 hadi asilimia 35 ili kuwalinda wazalishaji wa ndani na kuongeza biashara miongoni mwa nchi za EAC. Hatua hiyo itawanufaisha wasindikaji wa ndani wa bidhaa za samaki, nyama, maziwa na mazao ya kilimo ikiwa ni pamoja na kahawa, chai, mboga na matunda, mafuta ya kupikia, saruji, chumvi,  sabuni, vifungashio, bidhaa za ngozi na samani za mbao kwa lengo la kuleta unafuu wa bei za bidhaa hizo.

 

 

2.     MWENENDO WA BEI ZA BIDHAA

 

i)         MAFUTA YA KUPIKIA

Serikali inatekeleza Mkakati wa kuongeza uzalishaji wa ndani wa mafuta ya kula ikiwa ni pamoja na kuhamasisha wakulima kutumia mbegu bora za alizeti na chikichi (mawese) ili kuongeza uzalishaji wa mafuta ya kupikia yatokanayo na mazao hayo. Ongezeko la bei ya mafuta duniani lina athari hasi kwetu Watanzania, kwani mahitaji ya mafuta ndani ya Taifa letu kwa mwaka ni tani 650,000 (MT) huku uwezo wetu wa kuzalisha mafuta ni tani 270,000 (MT), ambayo ni sawa na asilimia 41.5 tu ya mahitaji yetu kwa mwaka. Hivyo ongezeko lolote la bei ya mafuta ya kula kwenye soko la Dunia lina athari hasi za moja kwa moja kwenye bei ya bidhaa hiyo kwenye soko letu la ndani.

 

Wastani wa bei ya mafuta kwa mwezi Julai, 2022 ilikuwa Shilingi 5,000 kwa mafuta yaliyosafishwa mara moja na Shilingi 9,000 kwa mafuta yaliyosafishwa mara mbili (double-refined). Kwa mwezi Agosti, 2022 bei zimeshuka kidogo ambapo mafuta hayo yanauzwa kwa wastani wa bei ya Shilingi 4,500 na Shilingi 8,000 kwa mafuta yaliyosafishwa mara mbili (double-refined).

 

ii)       SABUNI

Bei za sabuni za kufulia za mche zimeongezeka katika kipindi cha mwezi Agosti kutokana na kuongezeka kwa bei ya malighafi za kutengeneze sabuni zinazoagizwa kutoka nchi za Indonesia na Malaysia. Bei zimepanda kutoka wastani wa Dola za Marekani 500 hadi 600 kwa tani hadi Dola za Marekani 1,800 kwa tani, hasa baada ya nchi ya Indonesia kuweka zuio la kusafirisha nje malighafi hizo. Kutokana na ongezeko hilo la bei ya malighafi bei kwa mche ni kati ya Shilingi 3,000 na 4,500.

 

Vilevile, sabuni ya kufulia ya unga inauzwa kwa shilingi 1000 hadi 4500/- kwa kilo moja (Doffi, Niceone, Killsoft) wakati Omo ikipatikana kwa Shilingi 8000 hadi 8200/- kwa kilo moja.

 

 

iii)        NGANO

Serikali inatekeleza Mkakati wa kuongeza uzalishaji wa zao la ngano nchini ili kukabiliana na upungufu wa tani 800,000 tunazoagiza kila mwaka huku kiasi kikubwa kikitoka katika nchi za Urusi na Ukraine. Mahitaji ya ngano

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

DKT NCHIMBI AWAAHIDI MAKUBWA WANANCHI WA KWELA, RUKWA

DKT NCHIMBI ASHIRIKI MAZISHI YA ASKOFU.GACHUMA WA KANISA LA NLGCC

𝙂𝘼𝙈𝙊𝙉𝘿𝙄 𝙆𝘼𝘾𝙃𝙀𝙕𝘼 𝙆𝙄𝘽𝙄𝙉𝙂𝙒𝘼.