WAKULIMA WA MAZAO YA MISITU, CHAKULA NA BIASHARA WAPIGWA MSASA NA NMB KIJIJI DAY NJOMBE

WAKULIMA wa Mazao ya Misitu, Mazao ya Chakula na Biashara, vikiwemo Vikundi vya Kijamii, Vyama vya Ushirika wa Msingi (AMCOS), Vyama vya Akiba na Mikopo (SACCOS) na Vikundi vya Kuweka na Kukopa (VICOBA), katika Mikoa ya Nyanda za Juu, wametakiwa kulitumia vema Jukwaa NMB Kijiji Day ili kuharakisha ukuaji wao kiuchumi.
 
NMB Kijiji Day ni Jukwaa la Kujenga Uelewa wa Elimu ya Fedha na Huduma Jumuishi za Kibenki kwa wakazi wa vijiji visivyofikiwa na huduma hizo linaloendeshwa na Benki ya NMB, ambalo mwaka huu linatumika pia kutoa Elimu ya Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia, likilenga kuwafikia wakazi wa vijiji 2,000 kote nchini.
 
Wito huo umetolewa na Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Njombe, Frank Mganga, wakati wa NMB Kijiji Day iliyofanyika wikiendi hii katika Uwanja wa Shule ya Msingi Image, Kata ya Kidegembya, ikiwakusanya pamoja wanachi za kata hiyo na ile ya Katembwe, kushiriki semina na matukio mbalimbali, ikiwemo Bonanza la Michezo.
 
Akizungumza wakati wa bonanza hilo, Mganga aliiishukuru NMB kwa kupeleka Jukwaa la Kijiji Day katika kata hizo, ambazo zimesahaulika kwa masuala ya Huduma Jumuishi za Kibenki, licha ya uwepo wa wananchi wengi na wakulima wa mazao ya misitu (miti na mbao) na mazao ya chakula na biashara yakiwemo chai, mahindi na viazi mviringo
 
“Uwingi huu wa wananchi waliohudhuria katika kipindi ambacho wengi wako mashambani, unaashiria kuwa wamechagua kujielimisha kupitia jukwaa lenu hili muhimu kwa ustawi wa maisha yao. Wamefurahia kila kitu hapa kuanzia bonanza lililoanza na ‘jogging’, michezo na hata semina kwa vikundi vya kijamii.
 
“Wanatamani tamasha hili liendelee kufanyika hapa siku nyingine, ili kuwajengea uelewa zaidi wa huduma za kibenki zinazoweza kuharakisha ukuaji wao kiuchumi na ndio maana tunaipongeza NMB kwa kupachagua hapa na wito wa Serikali kwa wananchi wa Kata za Kidegembye na Matembwe, tumieni fursa zote zilizoletwa na NMB Kijiji Day kwa maendeleo yenu,” alisema Mganga.
 
Meneja wa NMB Kanda ya Nyanda za Juu, Wogofya Mfalamagoha, aliyeambatana na mameneja wa Matawi ya NMB Njombe, Mafinga, Makambako, Makete na Wanging’ombe, alisema katika kufanikisha lengo la kufikisha masuluhisho ya kifedha vijijini, benki yake imejipanga kuwafikia wananchi waliko, kupitia mawakala na kuwaalika wafanyabiashara kujitokeza.
 
“Ukiangalia hapa tunao wanafunzi wengi waliohudhuria NMB Kijiji Day, benki yetu inawajali na kuwathamini sana watoto ndio maana tunazo akaunti za Mtoto na Chipukizi na wito wangu kwenu wazazi, tumieni jukwaa hili kuwafungulia watoto wenu akaunti zisizo na makato ili kuwajengea utamaduni wa kujiwekea akiba maishani mwao.
 
“Pia tuna akaunti ya Kikundi inayohudumia vikundi mbalimbali vya kijamii, pia tuna akaunti ya NMB Pesa ambayo haina makato na hufunguliwa kwa ‘buku’ tu, tuko hapa kuhakikishwa haachwi mtu miongoni mwenu. Wafanyabiashara hapa waitumie fursa hii kwa kuja kujisajili kuwa mawakala wetu ili hawa wanaofungua akaunti leo, wapate huduma,” alisema Wogofya.
 
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kijiji cha Image, Felix Payovela, aliiomba benki hiyo kutoishia hapo, badala yake waendelee kuelimisha wakati za kijiji chake na vijiji jirani katika kuzitambua na kuzitumia fursa zilizomo katika Sekta ya Fedha na kwamba uwepo wa mawakala wa NMB kijijini kwake, utachochea kasi ya wananchi na vikundi kujiwekea akiba.
 
“Mahudhurio haya ya watu wengi na ufunguzi wa akaunti mbalimbali unaofanyika kwa wingi, unamaanisha kuwa tunaihitaji NMB iendelee kuja hapa mara kwa mara kama mlivyofanya leo na tukio hili, linamaamisha kuwa NMB sio tu wanajua kutunza fedha zetu, bali kutunza wateja wao kwa ukarimu waliotufanyia leo,” alisema Payovela katika kufunga tamasha hilo.
 
Katika NMB Kijiji Day hiyo, licha ya semina kwa vikundi vya kijamii, vyama vya akiba na mikopo na vile vya ushirika – iliyoendeshwa na Adamu Karazani, ambaye ni Meneja Mauzo na Vikundi wa NMB, jumla ya timu nane zilichuana katika mchezo wa soka, ambako Wanginyi FC kutoka Kijiji cha Wanginyi, Kata ya Matembwe waliibuka mabingwa wakiwachapa Mlangali FC bao 1-0.
 
Ukiondoa soka, michezo mingine iliyoshindaniwa ni pamoja na kuvuta kamba wanaume na wanawake, ambako mashabiki wa timu kongwe nchini za Simba na Yanga walitoana jasho, huku Watumishi wa Halmashauri ya Njombe wakiwaduwaza Wafanyakazi wa NMB. Pia kulikuwa na mbio za magunia, kufukuza kuku na burudani za kwaya na ngoma asilia.
 











 

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

TOFAUTI YA WATU WA DAR NA WA MKOANI NI HUU

NOTI MPYA KUANZA KUSAMBAZWA MWEZI UJAO

HUYU NDIYE DKT. NCHIMBI, MAKAMU WA RAIS AJAE

CHAKUHAWATA WANENA MAKUBWA--