Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Itikadi, Uenezi na Mafunzo CPA. Amos Makalla, amebainisha kuwa hadi zoezi la uchukuaji na urejeshaji fomu ndani ya CCM linakamilika siku ya jana Julai 2, 2025, jumla ya wanachama 5,475 walichukua fomu za ubunge na ujumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar.
Akizungumza leo katika ofisi ndogo za makao makuu ya CCM, Lumumba jijini Dar es Salaam, CPA.Makalla amesema kuwa kwa nafasi ya wabunge wa majimbo yote 272 ya uchaguzi nchini, watia nia 3,585 wamechukua upande wa bara na 524 wamechukua upande wa Zanzibar ambapo kati ya watia nia hao 4,109 walioenda majimboni wanawake ni 263. Uwakilishi Zanzibar waliochukua fomu ni 503.
Kwa upande wa viti maalum ubunge kwenye jumuiya za chama 623 wamechukua kupitia Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT) Tanzania Bara ikiwemo 91 wa makundi maalum, huku kwa upande wa Zanzibar wamechukua 8 na viti maalum Baraza la Wawakilishi ni 9.
Kwa upande wa Jumuiya ya Wazazi Tanzania Bara ni 55 huku Zanzibar ni watatu na 4 wamejitokeza katika viti maalum uwakilishi, hivyo kufanya jumla ni 62.
Wanachama 161 wamejitokeza katika kinyang’anyiro cha ubunge wa viti maalum kupitia Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), ambapo kati yao 154 ni kwa upande wa Tanzania Bara na 7 upande wa Zanzibar.
Vilevile, kwa upande wa ngazi ya udiwani ambapo takribani kuna kata 3,960 bado CCM haijafanya majumuisho tunatarajia kuwa na watia nia takribani 15,000 nchi nzima katika nafasi hiyo, inayojumuisha madiwani na madiwani wa viti maalum.
Gharama za uchukuaji fomu kwa ngazi ya ubunge ilikuwa shilingi 500,000 huku kwa nafasi ya udiwani ikiwa ni shilingi 50,000. Hivyo kwa takwimu hizi kwa ngazi ya ubunge, CCM imeingiza shilingi bilioni 2.7 kutokana na ada za fomu.
Comments