MGAHAWA UNAOUZIWA CHAKULA KWA KULIPA TAKA

 

Katika jiji la Ambikapur, jimbo la Chhattisgarh, India, watu wenye njaa hupata mlo kamili bila kulipa pesa bali kwa kubadilisha taka za plastiki walizozikusanya. Mgahawa huu maalum, unaoitwa Garbage Cafe au Mgahawa wa taka, ulizinduliwa mwaka 2019 ukibeba kauli mbiu "taka zaidi, ladha bora zaidi".

Kila siku watu huleta mifuko ya plastiki, chupa na vifungashio vilivyotupwa. Kwa kilo


moja ya taka za pplastiki hupata mlo kamili wenye wali, mboga mbili, chapati, saladi na achari. Nusu kilo ya plastiki hubadilishwa kwa kifungua kinywa kama sambusa au kitafunwa jamii ya maandazi.

Kwa kina mama kama Rashmi Mondal, Mgahawa huu umekuwa mwokozi. Awali aliwahi kuuza taka za plastiki kilo moja kwa rupia 10 pekee kiasi kisichotosha kabisa kumsadia kimaisha. Sasa anaweza kulisha familia yake moja kwa moja kupitia taka za plastiki anazokusanya mitaani.

Kutatua njaa na taka kwa pamoja

Wengi hupata chakula hapa kwa kulipa taka Kwa mujibu wa Vinod Kumar Patel, msimamizi wa mgahawa huo kwa niaba ya Halmashauri ya Jiji la Ambikapur (AMC), lengo lilikuwa kutatua matatizo mawili: njaa kwa masikini na taka za plastiki mitaani. Wengi wanaonufaika ni wasio na makazi na wakusanyaji taka. Kwa wastani, watu zaidi ya 20 hulishwa kila siku.

Tangu kuzinduliwa, mgahawa huo umekusanya karibu tani 23 za plastiki. Kiasi hiki si kikubwa kulinganisha na taka zote za plastiki za jiji (tani 226 mwaka 2024), lakini kimepunguza kiasi kinachoishia dampo, kutoka tani 5.4 mwaka 2019 hadi tani 2 pekee mwaka 2024..

Mfumo wa usimamizi wa taka

Ambikapur imejipatia sifa kama moja ya miji safi zaidi India. Mwaka 2016, dampo kubwa la ekari 16 liligeuzwa kuwa bustani na mfumo wa "zero-waste" ukazinduliwa.

Plastiki inayokusanywa mgahawani hupelekwa kwenye vituo maalum vya ukusanyaji taka (SLRMs). Kuna vituo 20 ambavyo hutenga taka katika zaidi ya makundi 60 kwa ajili ya uchakataji ili kutumika tena. Vituo hivi huajiri wanawake 480 wanaoitwa swachhata didis (ndugu wa usafi), wanaokusanya taka nyumba kwa nyumba na kulipwa rupia 8,000–10,000 kwa mwezi.

Taka za plastiki huchakatwa na kugeuzwa chembe chembe kwa ajili ya ujenzi wa barabara au kuuzwa, huku taka mbichi zikichimbiwa chini kama mbolea. Takribani 50,000 tani za taka kavu (plastiki, karatasi, chuma, taka za elektroniki) zimekusanywa tangu 2016. Mfumo huu umepewa jina "mfano wa Ambikapur" na sasa unatumika kote jimboni Chhattisgarh

Changamoto na mafanikio
Kuna vituo 20 ambavyo hutenga taka katika zaidi ya makundi 60 kwa ajili ya uchakataji ili kutumika tena.

Ingawa wafanyakazi wa vituo wanapewa vifaa vya kujikinga, wakusanyaji taka wengi hawana kinga dhidi ya maambukizi na taka hatarishi, jambo linaloleta wasiwasi wa kiafya. Wataalamu kama Minal Pathak wa Chuo Kikuu cha Ahmedabad wanaona juhudi hizi ni mwanzo mzuri, lakini wanasema mabadiliko makubwa zaidi yanahitajika ili kupunguza tatizo la taka za plastiki.

Mafanikio ya Ambikapur yamechochea miradi mingine kote India. Siliguri (Bengal Magharibi) ilizindua mpango wa chakula bure kwa taka za plastiki mwaka 2019. Mulugu (Telangana) ilibadilisha kilo moja ya taka za plastiki kwa kilo moja ya mchele. Mysuru (Karnataka) mwaka 2024 ilianzisha ubadilishanaji wa taka za plastiki kwa kifungua kinywa au chakula cha mchana kwenye migahawa ya serikali. Huko Uttar Pradesh, taka za plastiki hubadilishwa kwa taulo za kike.

Hata hivyo, si kila mahali pamefanikiwa. Delhi ilifungua migahawa ya taka zaidi ya 20 mwaka 2020, lakini mingi imefungwa kutokana na ukosefu wa uelewa wa umma, uchakataji hafifu wa taka na miundombinu duni. Wataalamu wanasema tofauti na Ambikapur, mji mkubwa kama Delhi una watu wachache wanaotegemea mfumo huu ili kujikimu, hivyo hamasa imekuwa ndogo.

Mgahawa wa taka wa Ambikapur unaonyesha jinsi ubunifu mdogo unaweza kushughulikia matatizo mawili makubwa njaa na plastiki. Ingawa kiwango cha taka kinachokusanywa bado ni kidogo ukilinganisha na taka za jumla katika jiji, mpango huu umechangia usafi wa mji, umetengeneza ajira na umesaidia watu wasiojiweza kupata chakula. Kama ambavyo Pathak anasema, "Ni mwanzo mzuri, lakini tunahitaji mabadiliko makubwa zaidi".

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

WALIOKUWA WABUNGE WALIOPITIWA NA MKASI WA WAJUMBE

NENO KUNTU LA UMMY MWALIMU ALILOLITOA BAADA YA KUTEMWA KUGOMBEA UBUNGE

SPIKA MSTAAFU NDUGAI AFARIKI DUNIA

WAGOMBEA WALIOENGULIWA CCM LICHA YA KUONGOZA KURA ZA MAONI

MWENYE MASIKIO NA ASIKIE....