Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete, amemlinganisha Rais Samia Suluhu Hassan na “askari wa mwamvuli” kutokana na kupokea kiti cha madaraka ya kuongoza Tanzania bila maandalizi, na kufanikiwa kuivusha nchi katika mazingira magumu yaliyokuwepo baada ya kifo cha Hayati Rais John Magufuli.
Akitoa salamu katika uzinduzi wa kampeni za uchaguzi za CCM kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, unaofanyika katika Viwanja vya Tanganyika Packers jijini Dar es Salaam, Kikwete amesema marais wengine wa Tanzania akiwemo yeye walijiandaa kuongoza nchi hadi wakaunda kamati, lakini haikuwa hivyo kwa Rais Samia, aliyepokea kijiti cha uongozi ghafla.
Amesema Rais Samia alipokea kijiti cha uongozi wakati nchi ikipita katika janga la UVIKO-19 lililokuwa likitikisa dunia, huku pia ikiwa imeanzisha miradi mikubwa iliyohitaji bajeti kubwa ya fedha.
“Ninamlinganisha Rais Samia na askari wa mwamvuli aliyeshushwa akipiga risasi,” amesema JK.
Kikwete ameeleza kuwa wengi hawakuamini kama Rais Samia angefanikisha kuendeleza miradi hiyo mikubwa kwa kasi ileile. Baadhi ya miradi aliyotaja ni pamoja na ujenzi wa Bwawa la Julius Nyerere la Kuzalisha Umeme (JNHPP), Ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR), na Ujenzi wa Daraja la Magufuli (Kigongo–Busisi), kutaja kwa uchache.
Amempongeza Rais Samia kwa ubunifu wake wa kuja na mambo kama Falsafa ya R4 (Maridhiano, Ustahimilivu, Mageuzi na Kujenga Upya), kunyanyua sekta ya utalii kupitia filamu ya Tanzania: The Royal Tour, pamoja na matumizi mazuri ya fedha za UVIKO-19, miongoni mwa mengine.
Kikwete amesema ni kutokana na hayo na mengine mengi yaliyodhihirisha kwamba Rais Samia ana maono makubwa, ndipo Mkutano Mkuu wa CCM ukaamua kumpitisha kuwa mgombea urais wa chama hicho bila kuchelewa.
Comments