HATIMAYE KABURI LA KIYEYEYU LANG'OKA

 Nyaya na nguzo za umeme zikiwa zimekata denge kuepuka kupita juu ya makaburi yaliyo kando ya barabara kuu kilomita chache toka Iringa ukitokea Mbeya. Kuna hadithi zinasema Tanseco walishindwa kupitisha nyaya hizo juu ya hayo makaburi kwa sababu ambazo awali hazikuwa zinafahamika. Kuna hadithi zingine pia zilidai kwamba ukipiga picha hapo huwa hazitoki
                            Makaburi hayo kama yanavyoonekana yakiwa kandoni mwa barabara
 Jumla ya makaburi nane ndio ambayo yameondolewa katika eneo hilo na hakuna tukio lolote la ajabu lililopata kujitokeza pamoja na kuwepo kwa maneno mengi toka eneo hilo. Picha na mdau Francis Godwin.
Mabaki ya mwili wa Kiyeyeu yakiwekwa katika jeneza tayari kwa kwenda kuzikwa upya baada ya eneo la awali kuchimbwa kaburi lake ili kupisha upanuzi wa barabara kuu ya Iringa -Mbeya



HATIMAYE kaburi la kihistoria la Martine Kiyeyeu lililokuwa katika eneo la Isimila, kijiji cha Ugwachanya limeondolewa katika hifadhi ya barabara ya Tanzania-Zambia, Mkoani Iringa kwa ajili ya kupisha upanuzi wa barabara hiyo.
Kaburi hilo ambalo lilikuwa pembezoni mwa barabara hiyo, limeondolewa katika oparesheni iliyoendeshwa na Wakala wa barabara (Tanroads) kwa akiwashirikisha wananchi wa kijiji hicho.
Kaburi la Kiyeyeu linalokadiriwa kuwa na umri wa miaka kati ya 40 hadi 50, lina  historia ndefu kutokana majaribio ya kuliondoa mara kadhaa kushindikana.
Moja ya maajabu ya kaburi hilo ni kushindwa kupitishwa kwa umeme kupita juu ya yake na pia linadaiwa kushindikana kuondolewa mara mbili na kusababisha vifo vya watu wawili akiwemo aliyeuawa kwa nyuki na mwingine kufariki ghafla akiendesha tingatinga alipokuwa akijaribu kuling’oa.
Lakini jana kaburi hilo na mengine 21 yaliyokuwa kwenye eneo hilo yaliondolewa na kuhamishiwa upande wa pili wa barabara, ambako kulikuwa na kaburi moja la mtoto wa kike wa Kiyeyeu, ambaye hakuzikwa katika eneo lililokuwa na makaburi ya ndugu zake.
Wakizungumza na Mwananchi, baadhi ya watu walioshiriki katika zoezi la kuondoa kaburi hilo walisema kazi haikuwa ngumu kama walivyodhani.
 “Tumeondoa ‘kiulaini’, hakuna mila wala desturi iliyofanywa kabla ya kuliondoa, na ndugu wa Kiyeyeu wanasema watakuja kazi ikimalizika kwa ajili ya kumaliza mila zao,” alisema Gaitan Utenga.
Alisema kazi hiyo imefanikiwa kutokana na ushirikiano walioupata kutoka Tanroads ambao waligharamia shughuli nzima ya kuondoa kaburi hilo ilyowashirikisha vijana zaidi ya 30.
 “Tumelipwa pesa yetu vizuri, wamenunua sanda na masanduku kwa ajili ya mazishi na hatimaye kaburi limeondolewa tofauti na imani iliyokuwa imezagaa miongoni mwa wengi kwamba ingeshindikana,” alisema.
Mwenyekiti wa kamati ya kuondoa kaburi hilo ambaye ni mmoja wa wanafamilia wa Kiyeyeu, Pulo Kikoti alisema hakuna tatizo lililotokea wakati wa kuondoa kaburi hilo. Kazi hiyo alizanza jana saa nne asubuhi na kumalizika majira ya jioni.
Alisema ugumu ulikuwa katika kulibomoa kutokana na aina ya ujenzi wake, lakini baada ya kubomolewa  kazi ya kulihamishia upande wa pili wa barabara haikuwa ngumu.
Hata hivyo walisema tayari makaburi yote 22 yaliyokuwa katika eneo hilo yameondolewa na kwamba kazi ya kuzika mafuvu ya marehemu ambao wote ni familia ya Kiyeyeu inatarajiwa kumalizika leo mchana.
“Ndugu wanasema mwishoni baada ya mazishi kukamilika na makaburi mapya kujengwa, watakuja kufanya mila zao, lakini mpaka sasa tumemaliza shughuli nzima ya kuondoa kwa kaburi hilo ambalo lilikuwa gumzo kwa miaka mingi,” alisema.
Mzee huyo alisema wengi waliamini kuwa eneo hilo lilikuwa la maajabu, kutokana na ukweli kwamba lilishawahi kujaribiwa kuondolewa zaidi ya mara mbili na ikashindikana.
“Kulikuwa na imani nyingi hapa, lakini tulijitosa kuhamisha na kweli hakuna kilichotokea hapa, naweza kusema imani hizi hazikuwa za kweli, mbona tumefanikiwa?” alihoji Kikoti.
Kuondolewa kwa kaburi la Kiyeyeu kumekuwa gumzo kwa watu wengi wakiwemo abiria wanaopita katika barabara hiyo ambapo kila mmoja amekuwa akishangaa jinsi kazi hiyo ilivyofanyika.
Awali mkazi wa Mafinga, Sadick Mhomanzi alijitokeza akidai kuwa anaweza kuliondoa kaburi hilo la  Kiyeyeu na kwamba hakuna madhara yoyote ambayo yangeweza kumpata.
Hata hivyo mapema jana, Mhandisi aliyeshiriki operesheni ya kupitisha umeme kwenye kaburi hilo mwaka 2006, Eliasante Mwakalinga, alionya kuwa Sadick asithubutu kwani angeweza kupatwa na balaa.
Akizungumza na gazeti hili kutoka mkoani Mtwara jana, Mwakalinga ambaye sasa ni mwalimu wa Chuo Cha Mafunzo Stadi Veta mkoani Mtwara, alisema maajabu yanayofanyika kwenye kaburi hilo, yanatisha na yanaweza kuwa hatari kwake.
"Mimi sijui atatumia mbinu gani lakini lazima iwe ushirikina au nguvu za kiroho. Hata hivyo ni vema akatafakari kwa kina uamuzi huo kwani unaweza kumgharimu na akaongeza historia ya kaburi hilo kwamba sasa, wamekufa watu watatu badala ya wawili," alisema Mwakalinga.
Alisema wakati wanatengeneza laini ya umeme eneo la kaburi hilo mwaka 2006, umeme uligoma kupita juu yake na wakalazimika kuhamisha njia ndipo walipofanikiwa.
Mwakalinga alipendekeza serikali kulifanyia uchunguzi kaburi hilo na ikiwezekana litangazwe kivutio cha watalii kwani kuna mambo mengi ya ajabu mbali na watu wawili kufariki dunia walipokuwa wanajaribu kuliondoa.
"Ukiwa huku Iringa utapata maelezo mengi kuhusu wazee wetu hawa, wengine walikuwa wanazikwa na vitu vyao, wengine walizikwa wakiwa wamekalishwa chini na hata baadhi yao walikuwa wanazikwa kwa kupakatwa na vijana wenye nguvu. Hayo yote ni historia yetu ambayo ni vyema tukaienzi,"alisema
Siku moja baada ya gazeti hili kuripoti maajabu ya kaburi hilo mkazi wa Mafinga, Sadick lijitokeza na kusema anaweza kuliondoa bila wasiwasi wala madhara yeyote tofauti na maelezo ya watu kwamba watu kadhaa wameshapoteza maisha kwa kujaribu kufanya hivyo.
Mhomanzi alitoa kauli hiyo wakati ambapo taarifa za uhakika kutoka katika eneo la kijiji hicho zikidai juhudi za kuliondoa kaburi hilo ili kupitisha barabara  eneo hilo  zimekuwa zikishindikana hata pale ilipotumika familia ya Marehemu Martin Kiyeyeu mwenyewe.
Lakini Mhomanzi kwa kujiamini alisema atakwenda yeye mwenyewe na kutumia jembe lake la mikono kuchimba na kuondoa udongo huo  hadi mifupa ya marehemu Kiyeyeu na kuihamisha bila ya kudhurika.
"Amini maneno yangu kuona kaburi linashindikana kuondolewa, hakuna mtu anayeweza kushindwa, kaka mimi niko tayari nitafanya kazi hiyo kwa mkono wangu kabisa,"alisema Mhomanzi.
Mhomanzi alihoji "Kama  ndugu wa marehemu wameridhia kuondolewa kwa kaburi hilo na kupatiwa eneo mbadala  ni kitu gani kinaweza kuzuia? mimi siamini hivyo,Tanrods waniwezeshe mimi kuifanya kazi hiyo, nitakwenda na jembe langu pamoja na koleo kuifanya kazi hiyo nitakachokosa ni trekta la kubebea udongo na mifupa"alisema .

HABARI KAMILI KWA HISANI YA GAZETI LA MWANANCHI

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MUSTAFA MKULO AFARIKI DUNIA

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

DKT NCHIMBI AWAAHIDI MAKUBWA WANANCHI WA KWELA, RUKWA

MAKALLA ASHANGILIWA BUNGENI

DK NCHIMBI ATINGA MKOANI KATAVI

BASHASHA LATAWALA NCHIMBI ALIPOLAKIWA NA CHONGOLO SONGWE

NCHIMBI AFUNGUA KONGAMANO LA MAADHIMISHO YA KUMBUKIZI YA MWALIMU NYERERE

DKT NCHIMBI AKARIBISHWA KIMILA NYUMBANI RUVUMA