TASWA YATOA TAMKO MWANDISHI WA TZ KUDHALILISHWA DRC CONGO

Mwenyekiti wa Taswa, Juma Pinto

CHAMA Cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA) kimesikitishwa na kinalaani tukio lililomkumba mwandishi wa habari za michezo wa gazeti la JamboLeo, Asha Kigundula wakati wa mchezo wa Kombe la Shirikisho kati ya Simba na DC Motema Pembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) Jumapili iliyopita.
Mwandishi huyo pamoja na Watanzania wengine waliokuwa Kinshasa, DRC kushuhudia mchezo wa Simba na DC Motema Pembe kwenye Uwanja wa Mashujaa ‘Stade des Martyrs’ walifanyiwa fujo ambazo hatukutarajia kama mashabiki wenye busara wangeweza kuzifanya.
Kilichotusikitisha zaidi ni hatua ya mashabiki hao kumdhalilisha mwandishi huyo bila kujali utu wake, heshima yake na thamani yake, kisa tu ni Mtanzania ambaye alikuwa uwanjani hapo kushuhudia timu ya Tanzania ikicheza.
Kamati ya Utendaji ya TASWA itakutana haraka iwezekanavyo kuhusiana na tukio hili ili kupata maelezo ya kina kwa vile Katibu Mkuu wa chama, Amir Mhando alikuwepo Kinshasa katika mchezo huo , hivyo atakuwa msaada mkubwa kueleza namna ya mambo yalivyokuwa.

Baada ya hapo TASWA itaangalia hatua ambazo kama chama na waandishi wa habari za michezo kwa jumla wanaweza kuchukua kwa jambo hili, kwani hata waandishi wa habari za michezo wa DRC, hawakutoa ushirikiano kwa wenzao wa hapa kama ambavyo wao walipewa wakati walipokuja Dar es Salaam na timu yao.

Kwa sasa Sekretarieti ya TASWA inafanya mawasiliano na Mwenyekiti wa klabu ya Simba, Ismail Rage pamoja na Asha kuhusiana na namna bora ya kuchukua hatua za kisheria kwa jambo hili.
Tayari Rage amesema hatua ya awali atamjulisha Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe kuhusiana na kudhalilishwa kwa mwandishi huyo na vurugu nyingine ambazo Simba ilifanyiwa Kinshasa na baada ya hapo tutaona hatua gani nyingine zifuatwe.
TASWA inaamini kama mashabiki wa DC Motema Pembe wangetumia kauli mbiu ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) inayosisitiza amani michezoni 'Fair Play', hakika baadhi ya mambo yasingejitokeza.
Watanzania ni watu waungwana sana, tumekuwa mara kwa mara tukifanya hivyo kwa wageni wetu, hatutaki kulazimika kuharibu sifa yetu nzuri, hivyo tunaamini mamlaka husika zitafuatilia jambo hili kwa umakini zaidi.


Ahsanteni
George John
Katibu Mkuu Msaidizi TASWA
22/06/2011

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAMBO YANAYOUA NDOA NA MAHUSIANO

RAIS SAMIA ANA KWA ANA NA ZUHURA YUNUS

KANUNI 10 ZA MAHUSIANO YENYE FURAHA

HAKI 13 ZA MWANAMKE LAZIMA MWANAUME AZIHESHIMU:

JINSI YA KUMSAHAU EX WAKO ALIEKUACHA;

RAIS DKT.MWINYI: ZANZIBAR KUWA KITUO CHA BIASHARA CHA KIMATAIFA

USHAURI WA BURE KWA KILA MFANYAKAZI

ACHENI KUWA CHANZO CHA CHOKOCHOKO NA VURUGU - ASKOFU CHANDE

JINSI BINTI HUYU MWANAFUNZI ANAVYOIPENDA MITI