VODACOM YATOA MSAADA WA ALAMA ZA USALAMA BARABARANI ZA WATU WENYE ULEMAVU

Ofisa wa Mfuko wa Kusaidia Jamii wa Kampuni ya Simu za Mikononi ya Vodacom Tanzania, Vodacom Foundation, Grace Lyon (kushoto) akimkabidhi Kamanda wa Kikosi cha Polisi cha Usalama Barabarani Tanzania, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, Mohamed Mpinga, alama za barabarani za watu wenye ulemavu katika hafla iliyofanyika, Dar es Salaam. Katikati ni Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama Barabarani ya Watu Wenye Ulemavu, Jutoram Kabatele. Kulia ni Mwakilishi wa Kampuni ya Compass, Mario Mpingirwa ambaye pia ni Mr Tanzania 2010/11. (PICHA NA RICHARD MWAIKENDA)


Kamanda wa Kikosi cha Polisi cha Usalama Barabarani Tanzania, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, Mohamed Mpinga, akitoa shukrani kwa Vodacom Tanzania, kuwapatia msaada.
Mwenyekiti wa Kamati ya Taifa ya Usalama Barabarani kwa Watu wenye ulemevu, Jtoram Kabatele, akitoa shukrani kwa Vodacom kuwapatia msaada wa alama hizo zenye thamani ya sh. mil 3.5 ambazo zitasambazwa barabarani katika Mkoa wa Dar es Salaam.
Mwakilishi wa Kampuni ya Compass, Mario Mpingirwa akielezea jinsi alivyoguswa na mateso wanayopata walemavu, hivyo kushawishika kwenda kuomba msaada huo kwa Kampuni ya Vodacom.

HABARI KAMILI

KAMPUNI ya Simu ya Vodacom, imekabidhi msaada wenye thamani ya Sh 3.5 milioni, kwa Kamati ya Taifa ya Watu wenye Ulemavu, ili zitumike katika kugharimia utengenezaji wa alama maalumu za barabarani kwa watu wenye ulemavu.

Alama hizo zilizobuniwa na mwenyekiti wa kamati hiyo, Jutoram Kabatele zitakuwa za kwanza kutumika barani Afrika na katika awamu ya kwanza, zitawekwa katika barabara za Jiji la Dar es Salaam na baadaye kote nchini.

Akizungumza katika makabidhiano ya alama hizo jana, jijini Dar es Salaam, Ofisa wa mfuko wa kusaidia Jamii wa Vodacom, Grace Lyon, alisema walemavu wanahitaji kuwa na alama za barabarani ili kuwawezesha kutumia barabara kwa usalama.Alisema alama hizo zinapaswa kuthaminiwa na kuheshimiwa na watu wote wanaotumia barabara.

“Ulemavu ni wa kila mtu, unaweza kuondoka nyumbani kwako mzima ukarudi ukiwa mlemavu, suala hili ni letu wote, tumewasaidia ndugu zetu walemavu ili nao watambue kuwa tuko pamoja nao na tunaheshimu mchango wao katika jamii,” alisema Lyon.

Akizungumzia msaada huo Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Mohammed Mpinga, alisema zitasaidia kwa kiasi kikubwa, kuepusha ajali zinazosababishwa na mazingira ya barabara.“Kabatele ndio aliyebuni alama hizi na zipo Tanzania tu, kinachotakiwa ni kumuunga mkono, zitasaidia kupunguza ajali zinazosababishwa na mazingira ya barabara kinachotakiwa kwa Watanzania ni kuzifuata,” alisema.


Alisema jukumu la usalama barabarani si la serikali peke na kwamba linahitaji juhudi za wananchi wote.Alisema juhudi zilizofanywa mpaka sasa ili kuhakikisha kuwa alama hizo zinatambuliwa ni pamoja na kuviagiza vyuo vyote vya udereva kufundisha alama hizo.

Kwa upande wake, Kabatele aliitaka serikali kuweka sheria kali dhidi ya madereva wanaovunja sheria kwa kuwa ndio njia pekee ya kupunguza kama sio kumaliza kabisa ajali za barabarani.“Kikubwa zaidi ni Vodacom kuhakikisha kuwa mradi huu unakuwa wa kudumu ili walemavu nao wajione kwamba ni sehemu ya jamii,” alisema Kabatele

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

BREAKING: CAF YAIPOKONYA KENYA KUANDAA CHAN

BREAKING NEWSSSS. WABUNGE WAPATA AJALI

MONGELLA AWATEMBELEA HOSPITALI WALIOMWAGIWA TINDIKALI

π—₯π—”π—§π—œπ—•π—” 𝗬𝗔 π—¬π—”π—‘π—šπ—” 𝗬𝗔 π—žπ—¨π—™π—¨π—‘π—šπ—” 𝗠π—ͺπ—”π—žπ—” 2024 πŸ”°

GERSON MSIGWA AREJESHWA KUWA MSEMAJI MKUU WA SERIKALI

AUCHO, BACCA, BOKA WAJUMUISHWA KWENDA ALGERIA LEO

AHMED ALLY KULIPA BIL. 10 KWA KUIKASHIFU YANGA