BURIANI WHITNEY HOUSTON

Mwili wa aliyekuwa mwanamuziki nguli, Whitney Houston ukitolewa hotelini alikofia
Whitney Houston enzi za uhai wake

Whitney Houston akiwa na Bobby Brown
Whitney na Dionne
Whitney alipozuru Mto Jordan
Whitney akiwa na tuzo yake
Whitney Houston akiwa na Bobby Brown

* Akutwa amekufa chumbani hotelini
* Brown alimshawishi kutumia 'ung'a
* Amefariki akitia kibindoni tuzo 415

LOS ANGELES, Marekani

MWANAMUZIKI nguli wa muziki wa Pop na R&B nchini Marekani, Whitney Houston, amekutwa akiwa amekufa katika chumba kwenye Hoteli ya Beverl Hill.

Nyota huyo alifariki Jumamosi mchana, siku moja kabla ya tamasha la tuzo za Grammy zitakazofanyika Los Angeles akiwa na umri wa miaka 48, na baada ya kutolewa taarifa za kifo chake, waandishi na watu mashuhuri walikusanyika hotelini hapo na kuwasha mishumaa kumkumbuka.

Ofisa wa Polisi, Mark Rosen aliwaambia waandishi wa habari kuwa wakati wa kifo chake, hayati Houston alikuwa katika chumba kilichoko ghorofa ya nne ya hoteli hiyo, na alitangazwa kuwa alikuwa amefariki saa 9:45.

Maofisa Upelelezi wa Los Angeles waliuondoa mwili wa mwanamama huyo aliyetikisa ulimwengu kwa vibao vyake vikali, kupitia mlango wa nyuma wa hoteli hiyo ili kuwakwepa waandishi wa habari waliokuwa wamejazana nje kwa hamu ya kupata habari za kifo.

Maofisa hao wanatarajiwa kufanya uchunguzi ili kubaini chanzo cha kifo kama kilikuwa ni matumizi ya dawa za kulevya, pombe au la ingawa hawatatoa taarifa mpaka wafanye uchunguzi wa kubaini sumu mwilini ambao unaweza kuchukua wiki sita hadi nane.

Rambirambi kutoka kwa watu mbalimbali duniani zilimiminika huku wakimuelezea namna alivyokuwa mahiri kwa uimbaji hususan sauti yake iliyovuta hisia kali katika muziki hasa wimbo 'I Will Always Love You.'

Nje ya hoteli hiyo walionekana walinzi wakilinda lango la kuingilia ili kudhibiti wapenzi na wanahabari kuingia na wakati huo wengine wakiwa pembeni wakiimba nyimbo zake na kuwasha mishumaa.

Kutokana na kifo hicho, mtayarishaji wa tuzo za Grammy za mwaka huu, Ken Erhlich, alitangaza kuwa wanamuziki Jennifer Hudson na Chaka Khan wangeimba katika tuzo hizo Februari 12, na wangemuenzi.

Katika miaka 30 ya muziki, Whitney alijijengea umaarufu kwa kunyakua tuzo sita za Grammy na tuzo za America Music 22 ambapo alifyatua albamu saba na kuuza nakala za CD milioni 170 pamoja na video za nyimbo zake.

Atakumbukwa zaidi katika ngoma yake ya 'I Will Always Love You' aliyoitoa mwaka 1985 (mara ya kwanza aliuimba Dolly Parton) ambayo ilitumika katika filamu ya The Boardguard ambapo pia alitoa nyimbo nyingine kama How Will I Know.

Alitoa albamu ya pili mwaka 1987 aliyoipa jina la 'Whitney' ambayo ilikuwa ni ya kwanza kwa mwanamuziki wa kike kushika namba moja katika nyimbo 200 kwenye chati za Billboard.

Nyimbo zilizompatia umaarufu ni kama Saving All My Love for You ambao uliwavutia wanamuziki wa kike wa Kiafrika waliotamani kuwa kama yeye, nyingine ni How Will I Know, Greatest Love of All, I Wanna Dance with Somebody (Who Loves Me), Didn't We Almost Have It All, So Emotional and Where Do Broken Hearts Go.

Mbali ya muziki, pia alikuwa mwanamitindo na aliwahi kucheza filamu kadhaa kama Bodyguard mwaka 1992 ambayo ilichukua tuzo ya Grammy mwaka 1994 kwa albamu ya mwaka katika wimbo I Will Always Love You, Waiting to Exhale (1995) na The Preacher's Wife (1996).

Hakuishia hapo kimuziki, aliendelea kufyatua albamu nyingine ambapo mwaka 1998 alifyatua My Love Is Your Love (1998) katika studio ya Arista Records, alitoa albamu ya tano Just Whitney (2002) na The Holiday ilitumika katika Sikukuu ya Krismasi 'The Holiday Album' (2003) na ya mwisho mwaka 2009 aliyoiita I Look to You.

Historia yake

Hayati Whitney Elizabeth Houston alizaliwa Agosti 9, 1963 katika familia ya kawaida kwenye kitongoji cha Newwark, New Jersey akiwa wa tatu katika familia hiyo.

Baba yake, John Russell Houston Jr. aliyekuwa mwanajeshi na mama yake Cissy Houston aliyekuwa mwimbaji wa muziki wa injili, alivutiwa naye, waliimba kwaya kanisani New Jersey akiwa na binamu zake, Dionne Warwick na Dee Dee Warwick na baadaye kuimba katika klabu za usiku.

Alisoma katika shule ya wasichana ya Kikatoliki ya Mount Saint Dominic Academy ambapo alikutana na rafiki yake Robyn Crawford, ambaye alimchukulia kama dada yake.

Mama yake mlezi Franklin, na Warwick walimtambulisha kwa wanamuziki wengine kama Chaka Khan, Gladys Knight na Roberta Flack ambao walimfundisha uimbaji mzuri.

Mwaka 1990 alipewa hadhi ya umalkia wa Pop kutokana na kufanya vizuri katika muziki huo na miaka miwili aliolewa na aliyekuwa mwanamuziki wa New Edition, Bobby Brown ambaye alikuwa na sifa mbaya kutokana na matumzi ya dawa za kulevya.

Waswahili wanasema chema hakikosi kasoro, walipooana, wawili hawa walianza kutumia dawa kwa miaka 14 mfululizo na mwaka 2000 wote wawili walizuiwa uwanja wa ndege wa Hawaii baada ya kubambwa wakiwa na marijuana katika mabegi yao.

Mwaka 2002 walianzisha kipindi cha televisheni kuonesha maisha halisi walichokiita 'Being Bobby Brown' ambapo walikiri kutumia cocaine, pombe kali na marijuana. Miaka 10 ya maisha yake hadi kifo iligubikwa na matumizi ya dawa.

Kipaji chake cha muziki kiliharibiwa na matumizi ya dawa za kulevya zilizosababisha kuharibika kwa maisha yake na baadaye kuvunjika kwa ndoa yake iliyokuwa imejaa matatizo mengi na mumewe, Bobby Brown mwaka 2007.

Pamoja na matatizo yote ya kimaisha, Whitney anafariki akiwa ametia kibindoni tuzo 415 zikiwemo mbili alizotuzwa na Emmy Music.

Wadau wa muziki wamekuwa wakimkumbuka akiwemo Quincy Jones ambaye amesema alikuwa mwanamuziki mwenye kipaji.

Daima wapenzi wa muziki watamkumbuka mwanamama huyo na pia wataendelea kumpenda kama alivyoimba katika wimbo wake 'I will Always Love You'. Mungu ailaze roho yake mahali pema.

Ciao...

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATANZANIA WATAKAOVAA JEZI ZA MAMELODI AU AL AHLY

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

KOCHA BENCHIKHA AMESEPA

MASHUSHUSHU WA MAMELODI WALIKUJA KUTUPELELEZA: HERSI