Air Tanzania Yatambulika Kimataifa kwa Uzingatiaji Viwango
New Delhi, India – Julai 1, 2025
Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) imepata utambuzi wa kimataifa kutoka Serikali ya India kama mtoa huduma anayeaminika zaidi, hatua inayozidi kuimarisha hadhi yake katika masoko ya nje. ATCL imepongezwa kwa kuendesha shughuli zake kwa uwazi, uadilifu, na kwa kuzingatia kikamilifu sheria mbalimbali ikiwemo za kodi, jambo linalothibitisha utayari wake wa kushindana katika soko la kimataifa.
Utambuzi huo umetolewa na Wizara ya Fedha ya India kupitia Bodi Kuu ya Kodi za Ndani na Forodha (CBIC), kwa kuzingatia viwango vya juu vya uwajibikaji wa kimataifa pamoja na mchango wa ATCL katika ukuaji wa uchumi wa India kupitia ushirikiano wa kibiashara.
Air Tanzania imetajwa kuwa miongoni mwa mashirika machache ya ndege kutoka Afrika yaliyotekeleza kwa ufanisi masharti mbalimbali, ikiwemo ulipaji wa kodi kwa wakati na kwa uwazi.
Akizungumza kuhusu utambuzi huo, Meneja Uhusiano na Mawasiliano wa ATCL, Bi. Sarah Reuben amesema: “Tunajivunia kutambuliwa na Serikali ya India, kwani ni moja ya masoko makubwa ya kimataifa yanayojulikana kwa mifumo madhubuti ya usimamizi wa Sheria. Hii ni ishara kwamba Air Tanzania inafuata viwango vya kimataifa na ipo tayari kuhimili ushindani wa soko la kimataifa.”
Kwa sasa, Air Tanzania ina mtandao mpana wa safari za ndani ya nchi, ikihudumia kupitia viwanja vya ndege vya Dar es Salaam, Dodoma, Mwanza, Arusha, Kilimanjaro, Mbeya, Songea, Mtwara, Iringa, Tabora, Kigoma, Bukoba na Zanzibar. Aidha, Kampuni inaendesha safari za moja kwa moja za kimataifa kwenda miji mbalimbali ikiwemo:
Dubai (UAE), Mumbai (India), Guangzhou (China), Johannesburg (Afrika Kusini), Kinshasa na Lubumbashi (DRC), Nairobi (Kenya), Hahaya (Comoro), Ndola na Lusaka (Zambia), Harare (Zimbabwe), Bujumbura (Burundi), na Entebbe (Uganda).
Hivi karibuni, ATCL inatarajia kuzindua safari za moja kwa moja kwenda Lagos, Nigeria, ili kuwaongezea wateja machaguo ya safari, kupunguza changamoto za usafiri wa anga katika Afrika Magharibi, kuchochea ukuaji wa uchumi, na kuwaunganisha wananchi kupitia huduma za haraka, salama na za kuaminika.
Comments