Rais Joyce Banda aliapishwa kuwa Rais wa 4 wa Malawi tarehe 7 Aprili, 2012 baada ya kifo cha Rais Bingu wa Mutharika akiwa madarakani. Awali Rais Banda alikuwa Makamu wa Rais na kwa mujibu wa Katiba ya Malawi alitakiwa kuwa Rais baada ya kifo cha Rais aliyeko madarakani.
Akiwa Makamu wa Rais, Joyce Banda alitengwa na Rais wake katika maamuzi makubwa na muhimu ya uendeshaji wa nchi. Inasemekana kutengwa kwake kulitokana pamoja na mambo mengine, kutofautiana na Rais Mutharika juu ya azma ya Rais Mutharika ya kumuandaa aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje, Mheshimiwa Peter Mutharika kugombea urais wa Malawi baada ya yeye kumaliza muda wake.
Kifo cha Rais Bingu wa Mutharika kilitibua mkakati huo wa kupokezana urais kifamilia. Waziri Peter Mutharika na genge lake wakiwemo maafisa waandamizi wa Serikali, na watu wao ndani ya Usalama wa Taifa na Polisi wakaanza mchakato wa kuzuia Makamu wa Rais Joyce Banda asiwe Rais. Mpango huo ulitibuliwa na aliyekuwa Mkuu wa Majeshi wa Malawi, Jenerali Henry Odillo aliyegomea mpango huo na kusimamia Katiba jambo lililopelekea Joyce Banda kuapishwa kuwa Rais.
Urais wa Joyce Banda ulikuwa mfupi sana. Mara baada ya kuingia madarakani, aliunda Tume kuchunguza kifo cha utata cha Rais Bingu wa Mutharika, na mambo yaliyoendelea nyuma ya pazia kati ya siku ya kifo na kupatikana kwa Rais mpya. Taarifa hiyo ilidhihirisha hujuma kubwa zilizofanywa. Hata hivyo, hakuchukua hatua madhubuti kwa kuchelea kuudhi kundi lenye nguvu la Hayati Rais Mutharika. Hatimaye, kundi lile liliendelea kujipanga na kuja kumwangusha katika Uchaguzi Mkuu uliofuata na akaachia madaraka tarehe 31 Mei, 2014 kwa mshindi wa urais ambaye ni Rais Peter Mutharika, mdogo wa Rais Bingu wa Mutharika, yule yule ambaye alitaka kumpokonya Urais kinyemela miaka miwili iliyopita.
Rais Banda akawa Rais wa kwanza mwanamke wa Malawi aliyeshika madaraka baada ya kifo akitokea kuwa Makamu wa Rais, na kuutema katika uchaguzi uliofuata. Kwa ufupi, Rais Banda alionekana kama Makamu wa Rais asiyetosha kuwa Rais, anayeshikilia tu kiti kwa muda akisubiriwa Rais anayefaa, ambaye ni mwanaume kukishika kiti hicho.
Hapa nyumbani, santuri hii ilitaka kurejewa. Alipofariki Rais John Pombe Joseph Magufuli akiwa madarakani, imeelezwa kuweko kwa jitihada za kundi la watu wakishirikiana na viongozi ndani ya CCM, Serikali na vyombo vya usalama kutaka kuzuia aliyekuwa Makamu wa Rais wakati huo, Samia Suluhu Hassan kuwa Rais. Sababu ni zile zile kuwa ni mwanamke na hakuwa mshirika wa karibu wa Rais Magufuli. Inaelezwa Mkuu wa Majeshi wa wakati huo, Jenerali Venance Salvatory Mabeyo
ndiye aliyeokoa jahazi kwa kuvunja mpango huo na kuwezesha Rais Samia kuapishwa kuwa Rais.
Kama ilivyokuwa Malawi, kikundi kile kilichopewa jina lisilo rasmi la 'Sukuma Gang' liliendelea na jitihada za kumhujumu na kutaka kumuangusha Rais Samia. Tofauti na Rais Joyce Banda, Rais Samia hakuunda Tume ya Kuchunguza Yaliyotokea Nyuma ya Pazia kufuatia Kifo cha Ghafla cha Rais John Pombe Magufuli. Yeye aliamua kuwakabili kimya kimya kama mtu anayemkimbiza mgoni wake. Akawajaribu kwa kuwapa fursa ya kufanya nae kazi, na wakajichuja wenyewe mmoja baada ya mwingine kwa kukosa kwao uaminifu na nidhamu kwa mamlaka iliyowateua.
Mbali na kundi hilo, walikuwepo na wahafidhina wengine ambao hawakupenda kuona Samia Suluhu Hassan akiwa Rais, ama kwa uanauke wake, ama kwa Uzanzibari wake, au kwa uislamu wake. Wakajiapiza kuhakikisha atakuwa Rais wa awamu moja. Wakajaribu kumzuia asigombee ndani ya CCM wakashindwa. Wakaunganisha nguvu na baadhi ya vyama vya upinzani vyenye mrengo wa kihafidhina, wakawavuta karibu na wanaharakati walio nje na ndani ya nchi. Wakatumia njia za wazi za kutumia mitandao ya kijamii, na hujuma za kificho kutaka kufifisha taswira yake katika jamii, na kuchochea vurugu na uasi.
Ushuhuda wa hilo unauona kwa namna ambavyo jitihada zake za ujenzi wa Taifa kwa kuleta maridhiano, kuleta mageuzi ya mfumo wa haki jinai na kufungulia uhuru wa habari na kuandamana ulivyogeuzwa kuwa silaha ya kumchapia. Akawanyooshea kitambaa cheupe kwa kuja na dhana ya 4R, wakamputa mkono. Waliokimbia nje wakati wa awamu ya Rais Magufuli akafungua milango wakarejea. Waliokuwa na kesi Mahakamani zikafutwa. Yote hayo hayakutosha kuonyesha dhamira njema kwa mioyo iliyojiapiza kumuangusha.
Hatimaye Rais Samia hakuwa na jinsi zaidi ya kwenda nao kwa mwendo walioutaka wao, ambao ndio ulikuwa mwendo wa mtangulizi wake Rais Magufuli, ambao inaonekana ulieleweka vyema sana na wapinzani na wanaharakati wetu. Sasa kila kona ni mayowe. Ni dhahiri kuwa mayowe haya ni matokeo ya jitihada na hujuma zao wenyewe. Lawama ni juu yao. Kwa upande wake, Rais Samia amelishinda jaribio hili lililomshinda Rais Joyce Banda, na anarudi katika awamu ya pili ya urais kwa kishindo.
Mkakati wa pili wa wasiomtaka Rais Samia Suluhu Hassan ni kuanzisha machafuko kwa njia ya maandamano kama ilivyotokea nchi jirani ya Kenya. Machafuko hayo hatimaye yapelekee ama Rais Samia kujiuzulu, au yaiweke serikali yake matatani ilazimike kukubaliana na matakwa ya wanaharakati, na wale walio nyuma yao.
Majaribio haya yalijaribiwa kwa kuanzisha vuguvugu kupinga uwekezaji wa DP World katika bandari ya Dar es Salam bila mafanikio. Wakajaribu tena kutumia mgogoro wa wafanyabiashara wa Kariakoo hawakufanikiwa. Wakajaribu kutumia kesi ya Mheshimiwa Tundu Lissu kwa kuleta wanaharakati wa Kenya na Uganda hawakufanikiwa. Wakajaribu kuanzisha vuguvugu kupitia changamoto za usafiri wa mwendokasi nako hawakufanikiwa.
Sasa tunaona mara michoro kwenye kuta na miundombinu ya umma, na matumizi ya mitandao ya kijamii kusambaza taarifa na video za maandamano na machafuko katika nchi za Madagascar, Ivory Coast, Sri Lanka na kwingineko. Kilicho dhahiri ni kuwa matendo yote haya yanaratibiwa. Iweje kila tukio linaloitwa la utekaji linalotokea nchini, watu wa kwanza kupata taarifa hizo na kuturipotia mtandaoni wawe ni wao wanaharakati walio Nairobi na Marekani? Tukio lolote la mgomo taarifa wapate wa kwanza wao? Kila eneo jipya la umma lillochorwa taarifa za maandamano picha wazipate wao? Tena wazipate kwa haraka sana ilihali wako nje ya nchi?
Uratibu huu mzuri na wa hali ya juu lazima uwe na fedha za kutosha na mtandao wa kutosha ikizingatiwa kuwa waratibu wenyewe, wanaishi nje ya nchi, tofauti na wanaharakati wa Kenya ambao wanaipinga serikali ndani ya nchi yao. Ndio kusema matukio haya hayatokei hewani na wala si kuwa hayahusiani. Kitu walichopatia, ni sanaa ya kujigeuza kuwa wao ndio wahanga na sio wachokozi. Inakumbusha utotoni ambapo yule mtoto mchokozi wa chini chini huwa ndio wa kwanza kupiga yowe.
Bahati nzuri Tanzania sio Kenya. Msuko wake na mfumo wake unafanya kuwa ngumu sana kwa kikundi fulani kutumia agenda ya dini, kabila, ukanda au tabaka kuunganisha umma kuuingiza kwenye maandamano. Watanzania kwa sababu ya historia yao ya ujamaa ambayo ilijenga jamii ya udugu, umoja na usawa wamejikuta hawana nongwa za moja kwa moja dhidi ya dola, kabila, dini ama dhidi ya Rais kwa sababu tu anatoka kabila fulani au dini fulani au upande fulani wa muungano.
Uzoefu wa Kenya nao ulisaidia sana kwa vyombo vya ulinzi na usalama vya Tanzania kujifunza, na kujielekeza kwenye kinga dhidi ya machafuko badala ya kusubiri machafuko yatokee ndio yadhibitiwe. Wananchi pia waliona namna ambavyo maandamano hayo ya Kenya yalivyoathiri maisha ya mtu mmoja mmoja, kuwatia vilema, umasikini n hata vifo. Isitoshe uharibifu wa biashara na miundombinu. Mbaya zaidi, hata baada ya machafuko hayo, mabadiliko hayakupatikana Kenya. Rais William Ruto ameendelea kuwa Rais wa Kenya, na hata mwanasiasa mkongwe Raila Odinga maarufu kama 'Baba' naye akaungana na upande wa serikali dhidi ya maandamano hayo. Sana sana aliyefaidika na maandamano na machafuko hayo ni Raila Odinga. Wakenya kwa ujumla wao watalazimika kulipa gharama ya uharibifu wa miundombinu uliosababishwa na maandamano kwa kodi zao wenyewe. Watanzania hawatauingia mtego huo.
Historia itamuandika Rais Samia kuwa shujaa aliyepindua meza. Aliyekataa kurudia makosa ya Rais Joyce Banda ya kuruhusu kuhujumiwa na kuondoshwa madarakani, na makosa ya kiusalama na kiulinzi ya Kenya ya kuchelea wanaharakati hadi kuleta machafuko makubwa yaliyoleta hasara kubwa kwenye maisha ya watu na uchumi wa Kenya. Hakika, Rais Samia anastahili mitano tena!
Comments