MAYANGA KUWEKA REKODI TAIFA STARS LEO?


Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
KOCHA Salum Mayanga leo atajaribu kuwa kocha wa kwanza wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars kushinda mechi tatu mfululizo tangu Marcio Maximo kati ya 2006 na 2010.
Wadenmark Jan Polusen na Kim Poulsen ni makocha waliomfuatia Maximo na chini yao Taifa Starsv haikuwahi kushinda mfululizo zaidi ya mechi mbili, kama ilivyokuwa kwa Mholanzi Mart Nooij na mzalendo mwingine, Charles Boniface Mkwasa.  
Mayanga leo ataiongoza Taifa Stars katika mchezo wa kwanza wa Kundi L kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 2019 nchini Cameroon, itakapomenyana na Lesotho kuanzia Saa 2:00 usiku Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
Ataiingiza timu uwanjani leo ikitoka kushinda mechi mbili mfululizo za kirafiki mwezi Machi, 2-0 dhidi ya Botswana na 2-1 dhidi ya Burundi.
Salum Mayanga leo atajaribu kuwa kocha wa kwanza wa Taifa Stars kushinda mechi tatu mfululizo tangu Marcio Maximo  

Na ikumbukwe Taifa Stars inaingia katika mchezo wa leo ikitoka kuweka kambi ya wiki moja nchini Misri katika Jiji la Alexandria.
Mchezo huo umelazimika kupelekwa kwenye Uwanja wa klabu ya Azam FC kutokana Uwanja wa Taifa kuwa katika ukarabati mdogo na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limeahidi ulinzi mkali ndani na nje kuhakikisha mambo hayaharibiki leo.
Mayanga amewapata wachezaji wote wa Ulaya, kuanzia Nahodha Mbwana Samatta wa KRC Genk ya Ubelgiji, mshambuliaji mwenzake wa zamani wa TP Mazembe ya DRC, Thomas Ulimwengu wa AFC Eskilstuna ya Denmark na winga Farid Mussa wa DC Tenerife ya Hispania.
Na kwa hapa nyumbani amewarudisha nyota wote aliowatumia kwenye mechi za Machi dhidi ya Botswana na Burundi, wakiwemo chipukizi washambuliaji Mbaraka Yussuf Abeid na Abdulrahman Mussa.
Amemtema tu kipa Deo Munishi ‘Dida’ na kumchukua mchezaji mwenzake wa Yanga, Benno Kakolanya – na maana yake leo anaweza akadaka Aishi Manula wa Azam FC. Kipa mwingine ni Said Mohammed Mduda wa Mtibwa Sugar.
Mayanga, muumini wa mfumo wa 4-4-2 kikosi chake leo kinaweza kuwa; Aishi Manula, Shomary Kapombe, Mwinyi Mngwali, Abdi Banda, Salim Mbonde, Himid Mao, Muzamil Yassin, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Mbwana Samatta, Thomas Ulimwengu na Farid Mussa.     
Katika benchi watakuwapo; Said Mohammed, Hassan Kessy, Aggrey Morris, Erasto Nyoni, Said Ndemla, Simon Msuva, Shiza Kichuya, Mbaraka Yussuf, Ibrahim Hajib na Abdulrahman Mussa.
Kila la heri Taifa Stars. Mungu ibariki Tanzania. Amin.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

BREAKING: CAF YAIPOKONYA KENYA KUANDAA CHAN

BREAKING NEWSSSS. WABUNGE WAPATA AJALI

MONGELLA AWATEMBELEA HOSPITALI WALIOMWAGIWA TINDIKALI

π—₯π—”π—§π—œπ—•π—” 𝗬𝗔 π—¬π—”π—‘π—šπ—” 𝗬𝗔 π—žπ—¨π—™π—¨π—‘π—šπ—” 𝗠π—ͺπ—”π—žπ—” 2024 πŸ”°

GERSON MSIGWA AREJESHWA KUWA MSEMAJI MKUU WA SERIKALI

AUCHO, BACCA, BOKA WAJUMUISHWA KWENDA ALGERIA LEO

AHMED ALLY KULIPA BIL. 10 KWA KUIKASHIFU YANGA