NILIYOYABAINI KATIKA TRENI YA SGR DAR ,MORO HADI DODOMA … KADOGOSA REKEBISHENI MAMBO HAYA MTANIKUMBUKA
Nikiwa ndani ya treni hiyo ya SGR.
KWANZA kabisa napenda kuipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi mahiri wa Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa ya ujenzi wa treni ya kisasa ya umeme maarufu SGR ambayo imeanza kufanya kazi mwaka jana wa 2024, hivyo kurahisisha usafiri kati ya Dar es Salaam- Morogoro na Dodoma.
Usafiri huo wa SGR umepokelewa na wananchi kwa mikono miwili, kwani kila siku tangu uanze umekuwa ukijaa abiria wanaoenda maeneo mbalimbali ya nchi.
Ukipanda SGR kuna raha yake; haichoshi kutokana na muda mchache inaotumia, ina usalama zaidi tofauti na usafiri wa barabara, haina mitikisiko, huduma safi ya vinywaji na vitafunwa, huduma ya choo, luninga bila kusahau kiyoyozi na kusikia sauti nyororo ya Binti ikitangaza kila kituo cha kupanda na kushuka pamoja na huduma zinginezo.
Pamoja na sifa zote hizo kuna kasoro nilizozibaini niliposafiri na treni hiyo mara nne ambazo nisingependa kuacha kuzielezea ili wahusika wazifanyie kazi, yaani wazirekebishe.
UKAGUZI WA TIKETI
Mara zote niliposafiri, kazi ya ukaguzi wa tiketi hufanyika mara moja tu wakati wa kupanda treni. Licha ya kuwepo wahudumu ndani ya treni, hakuna ukaguzi wowote hadi mwisho wa safari, jambo ambalo linatoa mwanya kwa baadhi ya abiria wasiowaaminifu kukata tiketi ya 1000 kutoka Stesheni ya Magufuli Dar kwenda Pugu na asiteremke hadi Moro au Dodoma, kwani hata mwisho wa safari hakuna ukaguzi.
MSONGAMANO WAKATI WA UKAGUZI WA TIKETI
Tatizo lingine ni uwepo wa msongamano wakati wa kukagua tiketi kwa njia ya QR Code ya kuruhusu abiria kwenda kuingia kwenye mabehewa.Kwanza muda wa kufanya hivyo unakuwa mdogo sana,wakati huo huo sauti inasikika kwamba zimebakia dakika chache milango ya treni kufungwa tayari kwa kuondoka.
Ushauri wangu kwenu rekebisheni changamoto hiyo kwa kuweka utaratibu mzuri kwa abiria wanaowahi kufika kufanyiwa mapema ukaguzi wa tiketi ( kama inavyofanyika katika usafiri wa Ndege) waruhusiwe kuingia eneo la kusubiria Ili muda ukiwadia wa kuingia kusiwe na usumbufu mwingine wa kupoteza muda.
TENGENI NJIA TOFAUTI ZA ABIRIA WANAOWASILI, WANAONDOKA
Hapa napo nimebaini changamoto ya abiria kupigana vikumbo kati ya wanaowasili na wanaoondoka kunakosababishwa na kutokuwepo kwa mpangilio mzuri wa kutenganisha njia tofauti za kupitia abiria hao.
Kwa mfano Alhamisi Januari 2, 2025 , saa 3 asubuhi katika Stesheni ya Magufuli Jijini Dar, nikiwa miongoni mwa wasafiri tuliokuwa tukiondoka Dar kuekekea Morogoro na Dodoma, nilishuhudia vikumbo hivyo kwa abiria waliowasili na treni saa 2:50 na wanaoondoka na treni hiyo hiyo saa 3:30.
Lifti za mtelezo na za kawaida zilikuwa hazitoshi. Hali kama hiyo ilitokea pia Stesheni ya Samia Suhuhu Hassan jijini Dodoma.
LUNINGA ITUMIKE KUTANGAZA KAMPENI ZA KITAIFA
Pia nashauri luninga zilizomo ndani ya SGR ziwe zinatumika kutangaza kampeni za kitaifa badala filamu na muziki, mambo ambayo baadhi ya abiria hawavipendi.Hivyo nashauri zitumike kusaidia kutangaza vivutio vya utalii na mambo mengine muhimu katika Nchi.
ABIRIA ACHENI USHENZI HUU
Jambo lingine baya nililolibaini ni kwa upande wa abiria wasiowaaminifu wanaoharibu kwa makusudi vifaa ndani treni hiyo kwa kunyofoa vifaa vya kuwekea vinywaji (kama inavyoonekana pichani), vyakula, kushora nyuma ya viti na hata wengine wanadiriki kuchana viti kwa wembe.
Pia baadhi ya abiria wanaotumia vyoo hawazingatii usafi, licha ya wahudumu kutoa maelekezo ya mara kwa mara jinsi ya kutumia vyoo hivyo.
YANGU MACHACHE NI HAYA,NAAMINI YATAZINGATIWA NA KUFANYIWA KAZI.
NAWATAKIA KAZI NJEMA.
NI MIMI ABIRIA WA SGR
KAMANDA RICHARD MWAIKENDA
0754264203
Comments