HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...


 Siku moja Imam Ahmad bin Hanbal ndiye alikuwa imam wa msikiti ambao ulikua umefurika waumini wengi. Waumini wakamuuliza:


"Ewe Imam, wauona wingi huu wa watu waliokuja kuswali?"


Akasema: "Hapana, sijaona hata mtu mmoja".


Kwa mshangao mkubwa, mmoja wao akamuuliza:


"Je, wewe ni kipofu mpaka usiwaone?"


Swali lile lilikuwa na utovu wa adabu na heshima kwa Imam, lakini Imam Ahmad akawajibu:


"Kipofu ni yule anayefumba macho yake asimuone mjane aliyeelemewa na mzigo mzito.


Kipofu ni yule anayeelekea Qibla lakini akawageuzia mgongo yatima na masikini.


Kipofu ni yule anayemsujudia Allah, lakini akawafanyia kiburi waja wake.


Kipofu ni yule aliyesimama katika safu za wenye kusali lakini haonekani katika safu za wenye njaa na wasema kweli.


Kipofu ni yule anayetoa sadaka siku moja, wakati ana uwezo wa kutoa sadaka kila siku.


Kipofu ni yule anayefunga kuacha kula, lakini hafungi kuacha ya haramu.


Kipofu ni yule anayeizunguka Nyumba Tukufu ya Makkah, lakini anasahau kuwazungukia masikini wanaokufa kila siku kwa ukali wa uhitaji.


Kipofu ni yule anayenyanyua juu sauti ya adhana, lakini hajawanyanyua wazazi wake.


Kipofu ni yule anayesali na kufunga, lakini anafanya udanganyifu wakati wa kuuza na kununua.


Kipofu ni yule anayesimama mbele ya Allah huku moyo wake ukiwa umebeba kinyongo, chuki, inda na dharau dhidi ya ndugu zake Waislamu.


Kipofu ni yule ambaye kuna tofauti kubwa kati ya ibada zake, tabia zake na namna anavyoishi na watu.


Kipofu ni yule anayeswali, akasujudu na kufunga, lakini anadhulumu na kutetea dhulma na uonevu.


Kipofu ni yule anayesali na kufunga, lakini mikono yake imejaa damu za Waislamu.


Kipofu ni yule anayesali, lakini swala zake hazimfai.


Kipofu ni yule anayechukua baadhi ya mambo ya dini, akaacha mengine.


Amesema kweli Allah Mtukufu pale aliposema:


"Na aliyekuwa hapa (duniani) kipofu (kwa kutoiona haki) basi atakuwa kipofu Akhera, na atakuwa aliyeipotea zaidi Njia", (Surah, Al-Israai, 17: 72)."


Ukweli na ufasaha wa jibu hilo la Imam uliwafanya wote wakae kimya, kwa maana hakuna yeyote aliyesalimika na mapungufu au makosa.


Hii ndiyo hali halisi iliyopo hata leo. Kila mmoja wetu akisoma hapa atakubali kwamba kuna eneo ambalo yeye ni kipofu.


Tunamuomba Allah ayape nuru macho yetu, na ayafanye yale tunayoyajua kuwa mtetezi wetu  siku ya Mwisho na yasiwe kinyume chake dhidi yetu.


"Na miongoni mwenu kuwe na kundi linalolingania kheri na linaloamrisha mema na kukataza maovu. Na hao ndio waliofaulu," (Al-'Imran, 3: 104).

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

DKT NCHIMBI AWAAHIDI MAKUBWA WANANCHI WA KWELA, RUKWA

DKT NCHIMBI ASHIRIKI MAZISHI YA ASKOFU.GACHUMA WA KANISA LA NLGCC

π™‚π˜Όπ™ˆπ™Šπ™‰π˜Ώπ™„ π™†π˜Όπ˜Ύπ™ƒπ™€π™•π˜Ό π™†π™„π˜½π™„π™‰π™‚π™’π˜Ό.

DK NCHIMBI ATINGA MKOANI KATAVI