Djigui Diarra aomba radhi Yanga, aandikia waraka mzito
Tangu Mabingwa wa Tanzania, Yanga wapokee kipigo katika mechi ya kwanza Hatua ya Makundi Ligi ya Mabingwa Afrika (CAF CL), mlinda mlango wa kikosi hicho Djigui Diara, ameandika waraka mzito kwa Wana Yanga, akiwaomba radhi kwa matokeo mabaya na kuwataka kuwa wavumilivu katika nyakati ngumu wanazopitia.
Yanga ilishuka dimbani Jumanne Novemba 26 kuumana na Al Hilal, ambapo walikubali kipigo cha mabao 2-0 ndani ya Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam na baada ya hapo karibu wachezaji wote wametumia kurasa za mitandao ya kijamii kuwapa pole mashabiki wa timu hiyo na kuwaomba radhi kwa vipigo mfululizo.
Katika tafsiri isiyo rasmi, Diara ameandika: "Habari Familia, ningependa kushiriki ujumbe huu muhimu na wewe kufuatia mfululizo wetu wa matokeo mabaya ya siku za hivi karibuni kupoteza michezo.
"Hamasa kwa timu, shauku na uungwaji mkono wa mashabiki ni vitu muhimu kwa mafanikio ya klabu yetu. Kila mwanachama wa timu yetu, awe mchezaji, kocha au mfanyakazi, anafanya jambo kuhakikisha tunazishinda changamoto hizi na kuinuka tena.
"Tunaelewa kuwa matokeo haya yanaweza kuwa ya kukatisha tamaa, lakini ni muhimu kudumisha imani kwa wachezaji na viongozi wa benchi la ufundi. Kila changamoto ni fursa ya kujifunza na kukua. Ni kupitia matatizo ambapo tunagundua nguvu ya kweli na umuhimu wa kushikamana pamoja.
"Tunawahimiza mashabiki wetu waendelee kupaza sauti zao kushangilia timu viwanjani, msaidie timu yetu, muwe na subira, uvumilivu. Njia ya mafanikio sio nyepesi kila wakati, lakini kwa pamoja tunaweza kuushinda wakati huu mgumu.
"Tukumbuke kwamba sisi ni zaidi ya timu: sisi ni familia. Sapoti yenu inayoendelea ni nyenzo muhimu. Tuwe wamoja na tudhamirie, kwa sababu kila mechi ni nafasi mpya ya kung'ara.
"Asante kwa uelewa wenu na kujitolea. Kwa pamoja tutashinda vikwazo hivi. Yangsc milele," 🔰🙏🤲🏻❤️ ameandika Diara ambaye katika mechi tatu mfululizo ameruhusu nyavu zake kutikiswa mara sita (1-0 dhidi ya Azam FC, 3-1 dhidi ya Tabora United na 2-0 dhidi ya Al Hilal zote wakipoteza kwenye viwanja vya nyumbani Azam Complex na Benjamin Mkapa.
Comments